Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, April 15, 2014

TEMBO WA RUAHA KUFUNGIWA VIFAA MAALUMU DHIDI YA MAJANGILI

tembo 1f0d9
Tembo wakivinjari hifadhi ya Taifa ya Ruaha
Viongozi wa makundi ya tembo kati ya 20 na 30 waiishio kwenye ikolojia ya Ruaha wanatarajiwa kufungwa vifaa maalumu kwa ajili ya kufuatilia nyendo zao ikiwa ni mkakati wa kuwalinda dhidi ya ujangili.
Ikolojia ya Ruaha inayojumuisha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha (RUNAPA) ndio yenye tembo wengi kuliko eneo jingine kwa Tanzania kwa sasa hivyo zinahitajika juhudi za pamoja katika kuwalinda tembo hao.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mratibu wa Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Godwel Ole Meing'aki alisema eneo hilo lina tembo wanaofikia 20,090 ambao ni wengine kuliko eneo jingine.


Mpango huo utakaotumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano ya setilaiti ya utambuzi wa jiografia ya maeneo (GPS) na kompyuta utatekelezwa kupitia SPANEST ikiwa ni mkakati wa kuimarisha ulinzi dhidi ya majangili.
"Kwa kawaida tembo huongozwa na jike mkubwa ambaye anajua njia na kuelekeza kundi zima na ndio watakaofungwa vifaa hivyo. Zoezi hili linahitaji gharama kubwa kwa kuwa litahusisha wataalamu wengi" alisema.
Alisema awali Selous ndio iliyokuwa ikiongoza kwa kuwa na makundi makubwa ya tembo hapo awali lakini kutokana na zoezi la kuhesabu lililofanyika mwaka jana kwa ufadhili wa mradi huo imebainika kuwa Ruaha inaongoza.
"Kwa mujibu wa Taasisi ya Utafiti wa Wanyama Tanzania (TAWIRI) ambao waliendesha zoezi la kujua idadi ya tembo eneo la Ruaha ni tembo 20,090 waliopo idadi ambayo huenda miaka michache iliyopita ilikuwa zaidi ya 30,000", alisema.
Alisema tembo hao watafungwa 'Color' ambazo zitakuwa na vifaa maalumu vitakavyokuwa vikionesha mahali walipo kwa nyakati tofauti.
Alisema sambamba na kufanya zoezi hilo Shirika la Maendeleo la Kimataifa (UNDP) kupitia SPANEST litaimarisha mfumo wa mawasiliano kwenye hifadhi hizo ili iwe rahisi kwa askari, kituo na kituo kuweza kuwasiliana kwa urahisi.
Mwenyekiti wa Mpango wa Matumizi Bora ya Maliasili Idodi na Pawaga (MBOMIPA), unaojumuisha vijiji vyote vinavyozunguka RUNAPA, Philip Mkumbata alisema mpango huo ni mzuri na utasaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti ujangili hasa dhidi ya tembo.

No comments:

Post a Comment