Rashid Mvungi akimuangalia mtoto wake Nasrah Rashid (4) ambaye ni
mlemavu wa viungo aliyefungiwa chumbani na kufichwa kwenye boksi bila ya
kufanyiwa usafi tangu akiwa na umri wa miezi tisa. Picha na Hamida
Shariff
POLISI
mkoani Morogoro, inaendelea kuchunguza kilichotokea mpaka mtoto mkoani
hapa, akateswa na mzazi mlezi kwa kuwekwa katika boksi tangu akiwa na
miezi tisa, mpaka alipotimiza miaka minne.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Morogoro, Leonard Paul, amesema, baba mzazi wa mtoto huyo, Rashid Mvungi
ambaye ni mtumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro alitakiwa
kwenda kutoa maelezo kituoni jana lakini hakutokea.
Kamanda Paul alisema jana kuwa,
walimtafuta mzazi huyo kwa simu ili kumkumbusha umuhimu wa kufika
Polisi kutoa maelezo, lakini simu zake zilikuwa zimezimwa.
Habari Leo ilifika kwa mwajiri
wake katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, ambako hakuwepo
kwa kuwa aliaga kwamba amekwenda katika Kituo cha Ustawi wa Jamii,
alikodai kuwa aliitwa.
Hata hivyo, mwandishi alipofika
katika ofisi hiyo, lilihakikishiwa na Ofisa Ustawi wa Jamii, Oswin
Ngungamtitu, kuwa Mvungi hakuwa amefika katika eneo hilo, wala hakukuwa
na mwito wa yeye kufika katika ofisi hiyo.
Katika tukio lingine la kutia
shaka, Habari leo lilipohojiana na Mvungi katika nyakati tofauti juzi,
alitoa taarifa mbili tofauti, kuhusu sababu za kumuacha mwanaye kwa mama
mkubwa wake, Mariam Said, aliyemuweka katika boksi kwa zaidi ya miaka
mitatu.
Katika mahojiano ya awali,
Mvungi alidai baada ya mzazi mwenzake, Mwasiti Ramadhan kufariki dunia,
alishindwa kumchukua mtoto wake kwa sababu tayari alishakuwa na mke.
Alidai kwa kuwa alikuwa ameoa,
alikubaliana na upande wa pili wa familia ya marehemu, kuwa mwanaye huyo
alelewe na mama yake mkubwa, Mariamu.
Katika mahijiano na mwandishi
mwingine juzi hiyo hiyo, Rashid alidai mwanae huyo alichukuliwa na Mama
yake mkubwa ili kumlea akiwa na umri ndogo na mara zote alikuwa
akipeleka fedha za matumizi.
Alidai kwa mara ya mwisho
alimwona mwanae huyo miezi miwili iliyopita akiwa na afya ya kuridhisha,
wakati taarifa zilizotolewa na Mariam, zilidai kuwa mtoto huyo
hajaogeshwa tangu Julai mwaka jana.
“Kila
nikienda kumwona nyumbani kwao sikubahatika kumwona , nilikuwa
nikiambiwa amelala ama ametoka na watoto wezake...isipo kuwa miezi
miwili iliyopita,” alidai Rashid kauli inayoonesha kuwa mtoto huyo
alikuwa akitoka na wenzake wakati majirani walitoa ushahidi kuwa
hawakuwahi kufahamu uwepo wa mtoto katika nyumba hiyo.
Taarifa kutoka katika Hospitali
ya Rufaa mkoani Morogoro, zimeeleza kuwa baada ya uchunguzi wa awali wa
afya ya mtoto huyo, alibainika kuwa na niumonia, ulegevu wa viungo
ikiwa ni pamoja na baadhi ya mifupa katika mwili wake kuvunjika.
Daktari Mshauri wa watoto,
Hores Msaky alipozungumza na Habari leo jana, alisema walimpokea mtoto
huyo juzi akiwa katika hali ya uchafu usio wa kawaida.
Msaky alisema waliamua
kumfanyia vipimo vya awali pamoja na picha za X ray, wakagundua kuwa
mifupa yake si ya kawaida, inaonekana imevunjika ingawa hawajajua nini
kimemvunja.
“Tunachokifanya hivi sasa ni kujaribu kujua tatizo hilo limetokana na nini,” alisema
daktari huyo .Hata hivyo Msaky alisema kuwa hospitali hiyo haina vifaa
vingi vya kupimia mifupa, hivyo imeshauriwa apelekwe Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam kwa ajili ya uchunguzi zaidi .
Muandishi wa habari hizi
alifanikiwa kuingia wodi aliyolazwa mtoto huyo na kumkuta akiwa
amechangamka, na alipoulizwa anaendeleaje alisema anasikia maumivu
katika sehemu ya kifua .
Mtoto huyo alikuwa akidhulumiwa
haki yake ya utu na kuteswa kwa zaidi ya miaka mitatu, kwa kufungiwa
ndani ya boksi kama mnyama, ili asiamumbukize mama mlezi virusi vinavyosababisha Ukimwi.
Unyama huo wa kusikitisha,
ulikuwa ukifanyika muda wote huo kwa mtoto huyo Morogoro mjini katika
mtaa wa Azimio bila kuripotiwa popote, huku wakazi na majirani wa nyumba
hiyo wakisikia akikohoa na kulia usiku, na baba yake mzazi akiendelea
na maisha kwa kumuogopa mkewe. Wakizungumza na gazeti hili juzi majirani
hao walidai Mariam alihamia katika nyumba hiyo mwaka 2010, lakini
hawakuwahi kumuona akiwa na mtoto.
Hata hivyo majirani hao
walikiri kwamba walikuwa wakisikia mtoto akikohoa na kulia hasa nyakati
za usiku, lakini walikuwa na wasiwasi kuwa huenda mtuhumiwa alikuwa
mshirikina anayefuga watu waliouawa kishirikina au kwa jina linguine
misukule.
Hatimaye juzi mateso ya mtoto
huyo yalipungua, baada ya msamaria mmoja kupata taarifa sahihi, kwamba
ndani ya nyumba hiyo kuna kiumbe asiye na hatia aliye katika mateso na
kutoa taarifa kwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwanja cha Ndege, Dia
Zongo.
Zongo akiwa katika kazi za
kawaida katika mtaa huo, alipata taarifa kutoka kwa majirani kuwa kuna
mwanamke, Mariamu Said, amemficha mtoto ndani ya boksi na hamfanyii
usafi wala kumtoa nje.
Baada ya kupata taarifa hizo,
Zongo alimtafuta mwenyeji wake, Mwenyekiti wa mtaa huo, Tatu Mgagalana
na kuongozana naye hadi kwenye nyumba hiyo ambapo walimkuta mtuhumiwa,
Mariamu na kuanza kumuhoji kuhusu tuhuma hizo.
Kwa mujibu wa Zongo, wakati
mtuhumiwa akijibu maswali aliyoulizwa huku akibabaika, ghafla mtoto huyo
alipiga chafya na kuanza kukohoa hali iliyowapa wasiwasi na kuamua
kuingia chumbani kwa Mariamu kwa nguvu, hatua iliyomuokoa mtoto huyo
kutoka katika mateso ya zaidi ya miaka mitatu.
Ofisa huyo na mwenyeji wake
walimkuta mtoto huyo ametapakaa uchafu uliotokana na kinyesi na mkojo,
kwa kuwa boksi hilo lilikuwa chumba chake cha kulala, meza yake ya
chakula na maji na choo kwa ajili ya haja ndogo na kubwa.
Credit: Habari Leo
No comments:
Post a Comment