Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, May 12, 2014

MUENDELEZO WA KESI YA MBUNGE WA BAHI KUOMBA NA KUPOKEA RUSHWA"OMARY BADWEL"

NA MIRIAM MOSSES
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imetupilia mbali pingamizi la awali la upande wa utetezi kuhusu kusitisha kusikiliza kesi  inayomkabili  Mbunge Omary Badwel  (pichani) ya kuomba na kupokea rushwa kutokana na kesi ya Kikatiba iliyofunguliwa na mshtakiwa huyo kutokuwa na uhusiano na tuhuma za jina zinazomkabili.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Mhe. Hellen Riwa, kwamba kesi ya jinai inayomkabili Badwel haina uhusiano na kesi ya Kikatiba aliyofungua katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

Hakimu Riwa alisema kesi inayomkabili mshtakiwa iliyopo mbele yake itaendelea kusikilizwa kutokana na kesi hizo mbili kutokuwa na uhusiano.

"Mahakama imekataa pingamizi la awali la utetezi na itaendelea kusikiliza kesi hii ya jinai haina uhusiano na kesi ya Kikatiba aliyofungua mshtakiwa Mahakama Kuu... "alisema Hakimu Riwa.

Alisema ushahidi wa upande wa Jamhuri utasikilizwa Juni 12, mwaka huu.

Mapema mahakamani hapo, wakili wa utetezi Mpale Mpoki, alidai kuwa wamefungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu Tanzania kwa hiyo kesi hiyo isiendelee kusikilizwa Mahakama ya Kisutu, hadi ile ya Kikatiba itakapotolewa uamuzi.

Alidai kesi hiyo ya Kikatiba ilifunguliwa Desemba 5, mwaka jana na kusajiliwa kwa namba 48/2013, wanaiomba Mahakama Kuu, kutengua sheria namba 25 ya mwaka 2002 iliyofanyiwa marekebisho sheria namba 372 kifungu kidogo cha cha (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa Jinai (CPA).

Alisema sheria hiyo inakataza mtu yoyote kupinga uamuzi unaotolewa ndani ya usikilizwaji wa kesi na kwamba sheria hiyo inakinzana na Ibara ya 136 (a) ya Katiba inayosema mtu yoyote ana haki ya kukata rufaa ya aina hiyo.

Hata hivyo, Mwendesha Mashitaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Lizy Kiwia alidai kuwa kesi ya Kikatiba haihusiani na kesi ya tuhuma za rushwa inayoendelea kusikilizwa dhidi ya mbunge huyo hivyo mahakama itupilie mbali ombi la utetezi.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa  mshtakiwa akiwa kama Mbunge wa Jimbo hilo, Mjumbe LAAC na mtumishi wa umma, alitenda kosa hilo kati ya Mei 30 hadi Juni 2, mwaka 2012 jijini Dar es Salaam.

Ilidaiwa kuwa,  kinyume na Sheria ya Kupambana na Kuzuia Rushwa, Mbunge huyo alishawishi kutolewa kwa  rushwa ya Shilingi milioni nane kutoka kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga, mkoani Pwani, Sipora Liana, ili awashawishi  wajumbe wa kamati hiyo wakati wa kupitia ripoti ya bajeti ya halmashauri hiyo ya mwaka 2011/12.

Ilidaiwa katika shitaka la pili kuwa, Juni 2, mwaka 2012, katika Hotel ya Peacock, jijini Dar es Salaam, mshitakiwa alipokea rushwa ya Shilingi milioni moja kutoka kwa Liana kwa ajili ya kuwashawishi wajumbe wa LAAC kupitisha ripoti ya bajeti ya halmashauri hiyo ya mwaka 2011/12 bila vikwazo.

Hata hivyo, Mbunge huyo alikana mashtaka dhidi yake na yuko nje kwa dhamana.

No comments:

Post a Comment