Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Wednesday, May 14, 2014

MWENYEKITI WA CCM KIJIJI CHA KILIMANI MASHARIKI ALIWA NA MAMBA

 
Mtoto wa marehemu aliyeokolewa katika ajali hiyo akiwa na shangazi yake
Mvua inaweza kuwa neema pale inaponyesha kwa wastani, lakini ikawa karaha pale inapokuwa kubwa, hasa kwa watu wanaoishi mabondeni au kandokando ya mito.
Mikoa mingi nchini imepata adha ya mafuriko kutokana na mvua zilizoanza kunyesha mwezi uliopita. Lakini kwa wakazi wa vijiji vilivyopo kandokando ya Mto Rufiji, mvua zimewaletea wageni hatari katika maeneo yao.
Wageni hawa ni viumbe hatari; ni mamba waliowageuza wenyeji wao kuwa kitoweo na kuwafanya waishi kwa wasiwasi wakihofia usalama wao.
Wakazi hawa wanashindwa kuendelea na maisha yao kama kawaida, ikiwemo shughuli za kilimo ambazo huzifanyia ng’ambo au pembezoni mwa mto huo.

Kwa muda mrefu sasa mnyama huyo amekuwa tishio kwa wakazi wa Wilaya ya Rufiji. Wanyama hao wengi huishi katika mabwawa yaliyopo katika Hifadhi ya Selous, lakini mvua  inaponyesha na maji kujaa mtoni, mamba hurahisishiwa kazi ya kuwinda binadamu.
Wakazi wa vijiji vya Utete, Chemchem, Mkongo, Ngorongo, Nyaminywili, Mloka na Mwaseni hujishughulisha na kilimo cha mazao ya mahindi, mpunga, ndizi na matikitimaji kando ya mto huo.
Wengi wao hulazimika kuvuka mto huo ili kwenda ng’ambo ya pili kulima, au kuwinda ndege na usafiri wao mkubwa ni mitumbwi ambayo siyo salama katika kipindi hiki.
Hivi karibuni, mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi tawi la Lumumba katika kijiji cha Kilimani Mashariki, Saidi Simba (60) aliliwa na mamba wakati akivuka mto huo.
Akiwa na mwanawe  wa kiume, Seif Saidi (5) mtumbwi waliokuwa wakisafiria ulijaa maji na kumlazimu kushuka ili ayaondoe.
Aliposhuka tu alipokelewa na mamba ambaye alimzamisha na kutoweka naye huku mtoto wake akibaki na taharuki na kulazimika kupiga kelele kuomba msaada.
Ofisa mtendaji wa Kijiji cha Kilimani Mashariki, Masudi Mminge anasema kuwa katika eneo hilo, mamba huweka makazi hasa wakati wa mvua.
 Anasema tatizo la wanyama hao ni kubwa katika kijiji chake na vijiji vya jirani,  hasa katika kipindi  cha masika.
Anasema kuwa mamba hao wakishaona maji yamekuwa mengi nao hutumia mwanya huo kutafuta chakula karibu na makazi ya watu au mashamba.
Mminge anasema kuwa maeneo alipozama marehemu Simba kuna mamba wengi wenye urefu wa hadi futi 15.
“Juzi tu hapa wamekamata ndama wa mfugaji mmoja ambaye aliwapeleka kunywa maji,” alisema.
Dada wa marehemu, Khadija Ali anasema marehemu kaka yake aliagiza familia nzima kwenda shambani kwa ajili ya kuhamia ndege na wanyama wengine waharibifu wa mazao.
Anasema alitanguliwa na mtoto wake Seif, huku baadhi ya ndugu na wake zake wakiwa nyuma kwenda katika mashamba kwa ajili ya kulinda shamba dhidi ya ndege na wanyama.
“Alitangulia katika mtumbwi mdogo na sisi ilikuwa tupande mwingine, lakini kwa bahati mbaya alichukuliwa na mamba na mpaka sasa hatujaupata mwili wake,” anasema Khadija.
Mtoto Seif Saidi (5) anasema kuwa aliondoka na baba yake wakiwa na chakula, makuti kwa ajili ya kujengea dungu (aina ya nyumba) na jamvi.
Anasema kuwa alipoona baba yake anazama,  alianza kupiga kelele za kuomba msaada lakini hakuuona tena mwili wa baba wake.
“Nilimwona akivutwa kwa nguvu na hakuibuka tena, nilipiga kelele kuomba msaada. Nasikitika sijamuona tena baba yangu,” anasema.
Kwa upande wake, Hamisi anasema kuwa baada ya kusikia kelele za kuomba msaada, naye alipiga kelele watu wakaongezeka na kuingia katika mkondo huo kwa mitumbwi na kufanikisha kumuokoa  mdogo wake.
Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Ali Mwegio aliyeoongoza kikosi cha uokoaji kwa kutumia mitumbwi eneo hilo, anasema kuwa wametafuta mwili wa marehemu bila mafanikio.
“Kuna kipindi tulikuwa tukisikia harufu kali tukaaamini kabisa ni ndugu yetu mpendwa, lakini eneo panaposikika harufu hiyo kuna mamba wengi, tumeshindwa kusogelea eneo hilo kwa sababu ya usalama wetu,” alisema.
“Mamba akishakuchukua, hukuficha kwanza halafu ukioza ndio hula nyama,” alisema Mwegio.
Uamuzi wa Serikali
Ofisa mtendaji wa kijiji hicho, Masudi Mminge anasema kuwa hatua ya kwanza aliyochukua kama Serikali ni kuwatangazia wananchi kutokwenda mabondeni kipindi hiki cha mvua.
Anasema kuwa wakazi hao wasiende kabisa maeneo ya bondeni katika kipindi hiki cha mvua kubwa, licha ya kwamba wanatakiwa kwenda kwa ajili ya kulinda mazao yao.
Mminge alisema kuwa anatambua kuwa uwezekano wa wakazi hao kunyemelewa na njaa ni mkubwa, lakini amechukua tahadhari mapema kwa kuanza kutembelea kaya ambazo anaona ziko katika hatari ya kukumbwa na njaa.
Hatua ya pili ni kwamba mbunge wa Jimbo la Rufiji,  Dk Seif Rashid ambaye ni Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii alifika katika msiba wa Said Simba ambapo wananchi wamemuomba asaidie kuwapatia mtumbwi mkubwa utakaosaidia kuwavusha wananchi hao kuvuka vijito vinavyounganisha mto.
Anasema kuwa wakazi wa maeneo hayo hawavuki Mto Rufiji bali wanalima pembeni mwa mto huo, ambao ukifurika maji mamba huzagaa hadi katika mashamba yao wameomba mtumbwi mkubwa wa kuwasaidia kuvuka vijito, jambao ambalo waziri huyo ameahidi kulifanya.
Matukio ya mamba kula watu
  Ni matukio ya kawaida kama anavyosimulia meya wa mji mdogo wa Utete, Masudi Jaha anayesema kuwa wakazi wa wilaya hiyo waache mazoea ya kuamini kuwa maji wameyazoea.
  Aliyekuwa diwani wa Kata ya Mgomba  wilayani hapa kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Kasimu Mlekeni alinyofolewa tako la kulia na mamba wakati akioga katika dimbwi lililopo karibu  na shamba lake lililopo eneo la Nyamaruba.
“Kumbukumbu zangu zinaonyesha kuwa kila mwaka mamba anakula mtu, lakini watu wengi hupotea zaidi ya ninavyofahamu,” alisema Jaha
Mkuu wa Wilaya ya Rufiji,  Nurdin Babu anasema kuwa Mto Rufiji  umefurika na maji ni mengi mno na kwamba mafuriko hayo yameharibu mazao mashambani na hivyo kukwamisha mawasiliano kati ya kata moja na nyingine.

Babu anasema kuwa baadhi ya makazi ya watu katika eneo la Daraja la Mkapa yamemezwa na maji,  hivyo kuhatarisha usalama wa wananchi wanaoishi mashambani na kuwataka kuwa waangalifu katika maeneo yao.
Anasema kuwa maeneo hayo  yanafuga mamba wengi na wakati kunapotokea mafuriko, mamba hao huzagaa kila mahali kwa lengo la kutafuta chakula na hivyo amewaomba wakazi hao kuchukua tahadhari hususan wanaokwenda kuvua, kuogelea na kuteka maji.
“Sisemi msiende mtoni lakini mchukue tahadhari hasa kipindi hiki kigumu cha mafuriko kuna mamba wengi jamani,”anasema na kuongeza katika kipindi cha Januari hadi sasa watu wanne wamechukuliwa na mamba na hadi leo hawajaonekana.
Anaongeza kuwa katika kipindi cha Januari hadi mei, jumla ya watu wanne wamechukuliwa na mamba na mpaka sasa miili yao haijapatikana.
“Kutokana na maji kuwa mengi ni vigumu kuipata miili ya watu wanaochukuliwa na mamba, ndio maana ninawasihi watu waache tabia ya kukaribia mto huu,” anasema Babu.
Athari za mafuriko
Babu anasema kuwa  mafuriko yamesababisha hasara kubwa kwa mazao mashambani na wapo katika mchakato wa kujua ni kaya ngapi zimeathirika na mafuriko ili watume taarifa ofisi ya waziri mkuu kitengo cha maafa kwa ajili ya msaada wa chakula.
Pia anasema kuwa mawasilino kati ya baadhi ya kata na kata vijiji na vijiji yamekatika kutokana na makaravati kusombwa na maji.
Anasema kuwa hakuna mawasiliano kati ya Kata ya Ngorongo na Mwaseni, huku   maeneo mengi yakijaa maji jambo ambalo limewafanya wakazi kukwama kufika katika baadhi ya maeneo.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment