Watu wengi wangetamani kuona hawazeeki, wanabakia na nguvu za ujana na kwa sababu hiyo wanasayansi wanatafiti kupata ufumbuzi.
Vyuo vikuu vitatu maarufu duniani vimekuja na matokeo ya utafiti ambao unaweza kukata kiu ya wengi ambao hawatamani kamwe kuzeeka. Siku hizi kumekuwapo na usemi kuwa uzee mwisho Chalinze, jijini (Dar es Salaam) kila mtu ‘baby’ (mtoto). Hii ikiashiria watu hawapendwi kuitwa wazee ingawa umri wao ni mkubwa. Wamekuwa na kauli hiyo ili kulazimisha mazingira kwamba bado wana uwezo wa kufanya yote kama wenye damu changa lakini katika uhalisia si kweli.
Utafiti wa vyuo vya Harvard na California vya nchini Marekani vikishirikiana na Cambridge nchini Uingereza, unajenga mazingira ya kuifanya ndoto ya wenye mawazo ya kuukataa uzee kuwa kweli. Watafiti hao walichukua damu ya panya mchanga na kumuingizia kwa aliyezeeka. Walichobaini ni kwamba panya yule mzee alichangamka na kurejewa na nguvu za ujana.
Matokeo ya utafiti huo yanatoa mwanya kwa wanasayansi kukaa kitako na kutengeneza dawa ambayo mtu akitumia anaweza kutozeeka. Kutozeeka huko ni kuendelea kuwa na dalili za ujana kama vile kutokuwa na makunyanzi usoni na viungo kuendelea kuwa na nguvu ya kutekeleza mambo yote kama kawaida hata wenye umri wa zaidi ya miaka 70.
Utafiti ulivyofanyika
Timu ya watafiti hao wiki hii walitangaza kuwa wamegundua namna ambayo wanaweza kumfanya panya mzee kutokuwa na dalili zinazofanana na umri huo. Wanasema kwenye utafiti huo kuwa mara baada ya kuchukua damu ya panya mchanga na kumuingizia aliyezeeka ghafla alibadilika na kurejewa na nguvu zilizomfanya achangamke na kutenda kama vile bado hajazeeka.
Walichobaini ni kwamba ile damu ilienda kuchangamsha ubongo kiutendaji na kuwezesha kuimarika kwa utendaji wa mwili kwa jumla.Kwa kawaida mambo yote yanayotendeka mwilini huongozwa na ubongo kwa kuhamasisha homoni fulani kulingana na jambo husika.
Wanasema kwenye damu ya panya mdogo kuna aina ya protini ijulikanayo kama GDF11, ambayo wanahisi ndiyo iliyochochea jambo hilo. Wakasema wanachofanya ni kuchunguza kama hii protini ndiyo inayochochea ujana.
Mtaalamu wa Tanzania
Akizungumzia juu ya utafiti huo, mtaalamu wa Afya ya Jamii katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Dk Alex Mwita anasema hakuna haja ya watu kujipa matumaini kutokana na ugunduzi huo kwa sababu hadi kupatikana dawa itakayotumika kwa binadamu inaweza kuchukua miaka zaidi ya 10.
“Huu ni ugunduzi kwa panya. Hadi kufikia mafanikio kwa binadamu, ni utafiti utakaochukua miaka mingi,” anaonya Dk Mwita. Alisema zipo tafiti nyingi kuhusukile kinachosababisha uzee na kujaribu kutafuta njia za kuuzuia lakini bado mafanikio hayajapatikana.
Nini kinasababisha uzee
Wataalamu wanasema kuwa ni jambo ambalo liko wazi kwamba uzee unapozidi, mwili hushindwa kujimudu na hatimaye kusababisha kifo. Utafiti uliosimamiwa na mtaalamu wa Elimu ya Viumbe katika Chuo Kikuu cha Michigan nchini Marekani, Dk John Langmore ulibaini kuwa mtu anakufa kwa umri kutokana na viungo vya mwili kushindwa kutekeleza kazi zake kikamilifu.
Hali hiyo inachangiwa na kasi ya seli za mwili kuzaliana kupungua kwa kiwango kilichopindukia huku zinazokufa zikiwa nyingi. Mfumo huo uko hivi, mtoto anapozaliwa ukuaji wake ni wa kasi sana. Hii inatokana na uwiano wa seli zinazokufa kuwa kidogo zaidi ukilinganisha na zile zinazozalishwa. Uwiano wa seli zinazokufa na zinazozalishwa hufikia mahali ukalingana. Ikifikia kiwango hicho mtu huwa hakui tena.
Uzee unaanza pale uwiano wa seli zinazokufa kuwa wa juu zaidi kuliko zile zinazozalishwa. Hali hiyo huanza kuusababisha mwili kusinyaa na kusababisha mikunjo sehemu mbalimbali za mwili. Kasi ya seli zinazokufa ukilinganisha na zinazozaliwa huendelea kuongezeka na hali hiyo huendelea kuongeza makunyanzi na hata baadhi ya viungo kupoteza uwezo wake wa kawaida.
Kinachosababisha seli kutozaliana
Dk Langmore na timu yake wanaamini kufa kwa seli ni jambo la kawaida lakini sababu ya kasi ya kuzaliana kupungua kulingana na umri, ni jambo muhimu pia.Waliamini ufumbuzi huo ndiyo utakaowapa sababu ya mtu kuzeeka na pingine kutafuta namna ya kuzuia uzee.
Walibaini kuwa DNA ndani ya seli ndiyo inayohusika katika kuwezesha seli kuzaliana au kutozaliana.
Wakabaini kuwa ina kichocheo ambacho kinasababisha mazingira hayo ya seli kutozaliana hasa mtu anapofikia umri mkubwa. Dk Mwita anasema kulingana na tafiti mbalimbali zilizofanyika kuna kitu kinachojulikana kisayansi kama Telomere.
Anasema Telomere inauhusiana na seli kudumu muda mrefu ikiwa na uwezo wa kuzaliana au la. “Telomere ni kama kamba ya kufunga viatu. Inapomalizika unakua mwisho wa seli kuendelea kuzaliana,” anasema Dk Mwita. Anafafanua kuwa watu wanaokuwa na Telomere ndefu ndiyo wanaishi muda mrefu na wale wanaokuwa na fupi, maisha nayo yanapungua.
Mtafiti mwingine wa Marekani, Dk Ronald Klatz anaonya wanasayansi kutojikita tu katika kuchunguza sababu za uzee kwa kutumia jeni na mfumo wa seli za mwili. Akasema ipo haja pia kuchunguza mienendo ya mwili unavyoguswa na namna za ulaji, mazingira na misongo ya mawazo. Akasema hali hizo kwa namna moja au nyingine zinachangia mwili kuchoka na hata kupunguza kiwango cha kawaida cha mtu kuishi.
Imeandikwa kwa msaada wa mitandao
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment