Mahakama ya hakimu mkazi Kinondoni jijini Dar es salaam
imesitisha kwa muda shughuli zake baada ya zomeazomea iliyosababishwa na umati
mkubwa wa watu waliofika mahakamani hapo kushuhudia kesi inayomkabili Amina
Maige aliyeshitakiwa kwa kosa la kumjeruhi binti kwa kumng'ata na kumuunguza
kwa pasi.Ndivyo hali ilivyokuwa katika mahakama hiyo mara baada ya mtuhumiwa
huyo kufikishwa mahakamani hapo akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi ambapo
kabla ya kuteremka
kutoka ndani ya gari alifunika uso wake na mtandio hali
iliyosababisha umati huo kuanza kupiga kelele wakitaka afunuliwe ili aonekane.Hata
mara baada ya kuhifadhiwa katika chumba cha maabusu ya mahakama hiyo wakati
akisubiri kupandishwa kizimbani baadhi ya wanaharakati waliofika mahakamani
hapo nao walisikika wakilaani kitendo cha polisi kumsaidia kufunika uso.
Zoezi la kuwatuliza wananchi hao lilionekana kuwashinda
askari wa jeshi la polisi hali iliyowalazimu askari magereza kuingilia kati na
kusaidiana nao ili shughuli za mahakama ziweze kuendelea kama askari Mmoja
alivyosikika akiwaomba waondoke katika eneo hilo.
Akisoma shitaka linalomkabili mtuhumiwa huyo wakili wa
serikali Mohamed Salum mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya Kinondoni Yohana
Yongolo amesema mtuhumiwa Amina Maige anakabiliwa na kosa la kumjeruhi vibaya
Binti Eusta Hashim kinyume na kifungu kidogo cha sheria 225, kosa
alililolitenda huko eneo la Mwananyamala Manjunju.
Wakili Mohamed amesema upelelezi umekamilika ambapo
mshitakiwa amekana shitaka hilo na kurudishwa rumande baada ya mwendesha
mashitaka huyo kumuomba hakimu asimpatie dhamana kwa ajili ya usalama wake,
ombi ambalo hakimu alikubaliana nalo ambapo mtuhumiwa amerudishwa rumande hadi
June 26 mwaka huu kesi hiyo itakapotajwa kwa ajili ya masikilizo ya awali.
No comments:
Post a Comment