Ugunduzi huo mpya katika Kisima Piri-1 umefanyika katika
eneo lenye kiwango kidogo cha mawe ya mchanga kama ilivyokuwa wakati
ilipogunduliwa gesi katika Kisima cha Zafarani-1 mwaka 2012
Kampuni ya Statoil ya Norway na mshirika wake ExxonMobil
wamegundua kiasi kingine kikubwa cha gesi katika Bahari ya Hindi nchini
Tanzania.
Kiwango hicho kinakadiriwa kufikia futi za ujazo trilioni
mbili mpaka tatu (sawa na lita trilioni 56.6 hadi trilioni 84.9).
Ugunduzi huu unafanya jumla ya ujazo wa gesi iliyogunduliwa
na washirika hao kufikia
takriban futi za ujazo trilioni 20 (lita trilioni
566.25) kwenye Kitalu Namba 2, ambako washirika hao wanafanya shughuli za
utafiti na uchimbaji.
‘’Tangu mwaka 2012 tumekuwa tukipata mafanikio ya asilimia
100 nchini Tanzania na eneo hilo limekuwa kitovu cha utafiti ndani ya muda
mfupi. Ni kwa haraka tulitoka kwenye kuchimba kisima kimoja hadi kuwa na
mkakati wa kuchimba visima vingi,’’ alisema Makamu wa Rais wa Shughuli za
Utafiti za Statoil Ukanda wa Magharibi, Nick Maden.
Ugunduzi huo mpya katika Kisima Piri-1 umefanyika katika
eneo lenye kiwango kidogo cha mawe ya mchanga kama ilivyokuwa wakati
ilipogunduliwa gesi katika Kisima cha Zafarani-1 mwaka 2012.
Ugunduzi katika kisima hicho unakuwa wa sita katika Kitalu
Namba 2.
Uchimbaji wa gesi katika kisima hicho ulifanywa na meli ya
Discoverer Americas, usawa wa mita 2,360 za kina cha maji. Meli hiyo sasa
inachimba kisima kingine cha Binzari katika Kitalu namba 2.
“Eneo lingine la utafiti limeshaandaliwa na litajaribiwa
ndani ya mwaka 2014 na 2015. Tunatarajia kuchimba visima zaidi na tunatumaini
kuwa matokeo ya visima hivi yataongeza kiasi cha ujazo wa gesi kwa ajili ya
miundombinu ya mradi mkubwa wa gesi hapo baadaye,’’ alisema Maden.
Statoil ambayo imekuwapo nchini tangu 2007, inatafiti na
kuchimba gesi katika kitalu namba mbili kwa niaba ya Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania (TPDC) ikiwa na hisa ya asilimia 65 katika kitalu hicho wakati
ExxonMobil Exploration and Production Tanzania Limited ina asilimia 35.
Chanzo;Mwananchi
No comments:
Post a Comment