Wizara ya Maliasili na Utalii inapenda kuujulisha umma
matokeo ya sensa ya tembo iliyofanyika mwezi Oktoba na Novemba mwaka huu ili
kuiwezesha Serikali kutambua hali ya rasilimali ya wanyamapori ndani na nje ya
maeneo yaliyohifadhiwa.
Wizara kwa kushirikiana na wataalamu wa ndani na nje ya nchi
imefanya sensa katika Maeneo ya Mfumo ikolojia wa Selous – Mikumi na Ruaha –
Rungwa pekee kwa kuwa ni maeneo yenye tembo wengi nchini.Matokeo ya sensa hii
yanaonyesha kwamba Mfumo wa ikolojia wa Selous-Mikumi kwa sasa una tembo
wapatao 13,084 na Ruaha–Rungwa una tembo wapatao 20,090. Takwimu hizi
zinaonesha kupungua kwa idadi ya tembo na hasa katika mfumo ikolojia wa
Selous-Mikumi ikilinganishwa na Sensa za awali.Takwimu za muda mrefu zinaonesha
kwamba mwaka 1976 katika mfumo ikolojia wa Selous–Mikumi kulikuwa na tembo
109,419. Idadi hii ilipungua kufikia 22,208 mwaka 1991 kutokana na wimbi la
ujangili uliokuwepo katika kipindi cha mwaka 1984 -1989. Hata hivyo, idadi hiyo
iliongezeka na kufikia 70,406 mwaka 2006 baada ya Operesheni Uhai iliyofanyika
mwaka 1989 na 1990 na juhudi za kimataifa za uhifadhi ikiwemo kusitisha
biashara ya meno ya tembo
Aidha, idadi ya tembo nchini ilipungua hadi kufikia jumla ya
tembo 38,975 mwaka 2009 na kuendelea kupungua hadi kufikia tembo 13,084 hivi
sasa.
Hali kama hiyo inaonekana pia katika mfumo wa ikolojia wa
Ruaha-Rungwa ambapo sensa ya mwaka 1990 ilionesha kuwa na tembo 11,712 kutokana
na wimbi la ujangili. Idadi hii iliongezeka na kufikia 35,461 mwaka 2006. Hata
hivyo, idadi hiyo imepungua na kubakia tembo 20,090 hivi sasa.
Kwa matokeo haya inaonesha kuwa katika mfumo ikolojia wa
Selous-Mikumi idadi ya tembo imepungua kwa asilimia 66 ikilinganishwa na idadi
ya mwaka 2009 ambapo kulikuwa na jumla ya tembo 38,975. na katika Mfumo ikolojia
wa Ruaha–Rungwa Tembo wamepungua kwa asilimia 36.5 ikilinganishwa na idadi ya
mwaka 2009 ambapo kulikuwa na jumla ya tembo wapatao 31,625.
Kupungua huku kunathibitishwa na idadi ya mizoga ya tembo
iliyohesabiwa wakati wa zoezi la sensa. Jumla ya mizoga 6,516 na 3,496
ilihesabiwa katika mifumo ikolojia ya Selous-Mikumi na Ruaha–Rungwa. Katika
zoezi hili Wizara ilitumia vigezo vya uwiano wa mizoga na tembo hai
waliohesabiwa (carcass ratio) kubaini vyanzo vya vifo hivyo. Katika hali ya
kawaida, uwiano wa asilimia 7 – 8 unaashiria vifo vya asili kama vile ugonjwa
na uzee. Zaidi ya asilimia hiyo inaashiria vifo visivyo vya asili.
Sensa iliyofanyika mwaka huu imeonesha uwiano wa asilimia 30
kwa mfumo ikolojia wa Selous-Mikumi na asilimia 14.6 kwa Ruaha–Rungwa. Kwa
mujibu wa matokeo hayo, idadi kubwa ya vifo vya tembo vimetokana na vifo
visivyo vya asili.
Uchambuzi wa kina umebainisha kuwa asilimia 95 na 85 ya
mizoga iliyoonekana katika mifumo ikolojia ya Selous-Mikumi na Ruaha–Rungwa ni
ya zaidi ya miezi 18 iliyopita.
Hii inaonesha kuwa juhudi za makusudi zilizofanywa na
serikali ikiwa ni pamoja na kuimarisha doria na operesheni maalum mbalimbali za
hivi karibuni zimesaidia kupunguza wimbi la ujangili kwa kiasi kikubwa.
Aidha, kukamatwa kwa meno ya tembo yenye uzito wa kilogramu
32,987 ndani na nje ya nchi katika kipindi cha 2008 hadi Septemba 2013 ni
ishara tosha kuwa ujangili ni mojawapo ya sababu kubwa za kupungua kwa idadi ya
tembo nchini.
Sababu nyingine ni kuongezeka kwa mifugo katika maeneo
yaliyohifadhiwa na shoroba za wanyamapori. Mathalan, katika Pori Tengefu la
Kilombero ambalo ni sehemu ya ikolojia ya Selous – Mikumi, mwaka 2002 lilikuwa
na tembo 2,080, katika sensa ya mwaka huu, hukukuwa na tembo hata mmoja.
Ongezeko la bei katika masoko ya biashara haramu ya meno ya
tembo hususan katika nchi za Mashariki ya mbali ni kichocheo na kisababishi
kikubwa.
Kufuatia hali hii, Wizara inaimarisha ulinzi wa wanyamapori
kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama na taasisi nyingine za kanda
na kimataifa pamoja na kuelimisha na kushirikisha wananchi katika masuala
mbalimbali ya uhifadhi.
Ili kuimarisha na kuboresha shughuli za uhifadhi, Wizara iko
katika hatua za mwisho za kuanzisha mamlaka mpya ya wanyamapori. Vilevile
sheria za uhifadhi zinapitiwa ili kuruhusu kuanzishwa kwa mfumo wa kijeshi kwa
watumishi wa sekta ya wanyamapori.
Wizara inapenda kuwatambua na kuwashukuru wafadhili wote
waliofanikisha sensa hii iliyogharimu kiasi cha dola za kimarekani 160,000
ikiwa ni fedha za serikali na wafadhili. Wafadhili hao ni Shirika la Misaada ya
Kiufundi la Ujerumani (GIZ) kupitia Frankfurt Zoological Society (FZS) na
Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) kupitia Mradi wa TANAPA wa
SPANEST.
Imetolewa na
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii
Mhe. Lazaro Nyalandu (MB)
10/01/2014
No comments:
Post a Comment