Kamanda wa Polisi mkoani humo Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACP) Ulrich Matei akionyesha silaha na mavazi ya kijeshi waliyokamatwa nayo Watuhumiwa hao.
Na John Gagarini, Kibaha
JESHI la Polisi mkoani Pwani limefanikiwa kuwakamata watu watatu akiwemo mtu Daniel Mtalisi mkazi wa Kisemvule wilaya ya Mkuranga ambaye alipitia mafunzo ya kijeshi kwa tuhuma za kufanya tukio la uhalifu wa kupora silaha na vitu mbalimbali.
Mtuhumiwa huyo ambayealiwahi kupata mafunzo ya kijeshi kwenye Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kikosi namba 833 Oljoro Arusha na namba yake ni MT. 95150.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kwa waandishi wa habari mjini Kibaha, kamanda wa Polisi mkoani humo Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Polisi (SACP) Ulrich Matei alisema kuwa tukio hilo lilitokea Juni 17 mwaka huu majira ya saa 2 usiku huko Kijiji cha Kisemvule kata ya Vikindu kata ya Mkuranga wilaya ya Mkuranga.
Kamanda Matei alisema kuwa watuhumiwa hao wengine wakiwa ni Khalfan Abas (25) mkazi wa Mwanambaya na Mashaka Masanja (24) mkazi wa Mwongozo Kigamboni Jijini Dar es Salaam walikamatwa baada ya polisi kufanya msako mkali na kumkuta mtuhumiwa huyo akiwa na silaha hiyo ambayo walimpora Musa Kambangwa ambaye ni mfanyabiashara wa Mwanambaya.
“Watu hao walimvamia mlalamikaji ambaye alikuwa akirejea nyumbani kutoa kwenye biashara zake walimteka kisha kumpiga na walimwamuru awapeleke nyumbani kwake na kuichukua silaha hiyo bastola yenye namba A 569542 aina ya Browning, Carriber 7.65 mm, magazine 2 na risasi 23, chaja 1 ambavyo alikuwa amehifadhi nyumbani kwake,” alisema Kamanda Matei.
Aidha Kamanda Matei alisema kuwa kabla ya kukamatwa watuhumiwa hao walifanya tukio hilo Juni 11 mwaka huu huko Kijiji cha Mwanambaya ambapo walimvamia mlalamikaji akiwa na mke wake.
“Walimjeruhi kwa kutumia silaha mbalimbali za jadi na kumsababishia maumivu makali kisha kumtaka awape funguo ya nyumba yake ili waingie ndani lakini alikataa wakaendelea kumpiga hadi alipopoteza fahamu na kuichukua funguo na kuingia ndani na kuchuakua silaha hiyo na simu 2 aina ya Nokia, Inveta , deki 1 ya Dvd na viatu pea moja kisha kutoweka na ndipo walipokuja kukamatwa Juni 17,” alisema Kamanda Matei.
Alisema kuwa baada ya tukio hilo ndipo walipofanya msako na kufanikiwa kuvikuta vitu hivyo ambapo mtuhumiwa wa kwanza alikutwa na sare za Jeshi.
Alibainisha kuwa mlalamikaji anaendelea vizuri na kuwataka watu kutoa taarifa za uhalifu ili kuzuia matukio hayo ambayo yameanza kuibuka kwa wingi na watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani mara upelelezi wa tukio hilo utakapokamilika.
No comments:
Post a Comment