Dar es Salaam. Waziri Mkuu Mstaafu, Dk Salim Ahmed Salim
amesema hakutarajia kusikia kauli za Rais Jakaya Kikwete alizozitoa bungeni
kukosoa Rasimu Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa sababu walikuwa wanampa taarifa
kwa kila hatua waliyokuwa wanafikia kabla ya kutoa rasimu hiyo.
Dk Salim alitoa kauli
hiyo katika mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Masaki, Dar es
Salaam wiki iliyopita.
“Hatukutarajia kama hali ingefikia hatua iliyofikia,”
alisema Dk Salim na kuongeza: “Lakini Rais ana uamuzi wake na anazingatia mambo
mengine mengi.”
Akilihutubia Bunge maalumu la Katiba Machi 21, mwaka huu
Rais Kikwete aligusia mambo saba ya msingi yaliyomo katika Rasimu ya Katiba na
kutaka yatazamwe kwa kina, huku akibainisha kuwa mengine hayawezekani
kutekelezeka. Miongoni mwa mambo hayo ni muundo wa Serikali. Alipinga waziwazi
pendekezo la serikali tatu lililopendekezwa na Tume na kuegemea katika muundo
wa serikali mbili na idadi ya watu walioupendekeza akionyesha kuwa ilikuwa ni
ndogo.
Pia alisema ni vigumu kutenganisha uwaziri na ubunge kama
ilivyokuwa imependekezwa na Tume kwa maelezo kuwa mawaziri wanatakiwa kuwepo
bungeni ili kujibu hoja za Serikali.
Jambo lingine alilokosoa katika Rasimu ni pendekezo la mtu
kupoteza ubunge kwa sababu ya kuugua kwa miezi sita mfululizo huku akisema
baadhi ya vifungu vya Katiba vinayopendekezwa vimekuwa na mambo mengi ambayo
hayapaswi kuwamo katika Katiba, bali katika sheria zinazotafsiri utekelezaji wa
Katiba yenyewe.Katika mahojiano hayo maalumu, Dk Salim alisema baada ya
kuteuliwa kuwa Mjumbe wa Tume aliacha kuhudhuria vikao vya chama chake ili
aweze kufanya kazi hiyo kwa usahihi na alimtaarifu Mwenyekiti wa CCM ambaye ni
Rais na katibu mkuu wake na walimwelewa.
Alipoulizwa anaitazama vipi Tanzania iwapo Katiba Mpya
haitapatikana, Dk Salim alisema ana wasiwasi kwa kuwa suala hilo limeingizwa
siasa na Bunge Maalumu limegeuka la kisiasa hivyo linaweza kuleta matatizo.“Tuko
katika hali ambayo si nzuri inayohitaji uongozi thabiti, viongozi wote watambue
umuhimu wa zoezi hili kwa lengo la kulinda amani na utulivu wa nchi yetu,”
alisema.
Alisema kunahitajika ufumbuzi wa kudumu na hicho ndicho
kipimo cha uongozi kwa CCM, Chadema na wengine kwa kutafakari masilahi ya
Watanzania wa leo, kesho na keshokutwa.
Nini kifanyike?
Dk Salim alisema jambo muhimu sasa ni pande mbili
zinazoshindana kuhusu idadi ya Serikali kutumia mwezi ujao wa Julai kukaa
pamoja na kumaliza tofauti zao ili Bunge la Katiba liendelee bila misuguano.
No comments:
Post a Comment