Mwanafunzi Norat Rashid akipatiwa matibabu katika Taasisi ya
Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) iliyopo Hospitali ya Taifa Muhimbili.
MATESO ya mwanafunzi Norat Rashid (16), anayesoma kidato cha
pili katika Shule ya Sekondari Mtoni Relini, Wilaya ya Temeke, Dar es Salaam ni
ya kuhuzunisha na kutia huruma kutokana na ajali ya pikipiki aliyoipata miezi
nane iliyopita wakati akienda shuleni.
Norat alimuambia mwandishi wetu hivi karibuni katika Taasisi
ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) katika Hospitali ya Muhimbili Jengo la
Mwaisela chumba namba mbili kuwa ajali hiyo aliipata maeneo ya Mtoni kwa Azizi
Ally saa za asubuhi wakati akivuka barabara akienda shule.
Alisema mara baada ya ajali alipoteza fahamu na alipozinduka
alijikuta amezungukwa na madaktari wa Muhimbili. Katika mahojiano hayo, Norat
alikuwa na haya ya kusema:
“Najua huu ndiyo mwisho wangu wa kusoma, ndoto ya kufika
chuo kikuu imezimika ghafla kama taa, sikutegemea kama leo hii ningekuwa hivi,
nilizaliwa nikiwa sina matatizo, nilikuwa natembea kwenda shule leo hii
siinuki, nalishwa kama mtoto mdogo,“Mama ndiye ananiogesha, kila kitu juu yake
wakati hana kazi ya kufanya, namuhurumia sana, bora baba angekuwa hai
wangesaidiana kunitunza, pole mama…”
Muonekano wa jeraha la mguu baada ya kupata ajali ya
pikipiki.
ICU MIEZI MITANO
“Ajali niliyopata ilikuwa mbaya sana, sikutegemea kama leo
hii ningekuwa hai, kinachoniuma ni kuona niko kitandani siinuki wala kukaa,
nimevunjika mguu, kiuno na mbavu napata maumivu kupita kiasi, nipo hapa wodini
lakini ni baada ya kukaa katika chumba maalum cha wagonjwa mahututi (ICU) ambao
wako chini ya uangalizi wa madaktari kwa miezi mitano.
“Najua muda si mrefu nitaruhusiwa na madaktari kwenda
nyumbani, naamini nitakufa, sitachukuwa muda mrefu kutokana na umaskini wetu,
mahitaji muhimu sitayapata kwa vile mama hana kazi, tutakula nini, nitavaaje,
nitapataje dawa na tutaishi wapi, nyumba yenyewe ni ya kupanga na kodi imeisha,
tutaelekea wapi sisi jamani!
“Wakati nikiwa mzima mama alikuwa akizidiwa na majukuma na
sasa nimekuwa mlemavu wa kitandani tena wa kutazamwa muda wote! “Bora
ningebakia Muhimbili kuliko kumhangaisha mama, sijui kodi ya chumba atapata
wapi kwani kabla sijaugua alikuwa akihangaika kufanya biashara ndogondogo na
kupata fedha ya matumizi.”
Norat Rashid akiwa katika jengo la Mwaisela chumba namba
mbili katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
WALIMU, WANAFUNZI WENZAKE WAMSUSA
“Nikiwa shule wanafunzi wenzangu walikuwa wakinipenda sana,
nikiwa Muhimbili walikuja mara moja tu kuniona nilivyoumia, mpaka leo
sijawaona. Walimu nao walikuja mara moja kwa sasa hawaonekani, anayenitembelea
ni mama peke yake, hata mjomba naye haji sijui kwa nini, au wananiona kama
mzigo kwao?
“Kuna wagonjwa wanatembelewa na ndugu zao kuwafariji wakati
mwingine kuwaletea chakula lakini kwa upande wangu hakuna wa kunijulia hali,
lakini siyo tatizo kubwa kwangu, yote namwachia Mungu.
“Nawaombeni wananchi mlio na moyo wa huruma mnisaidie,
mniombee niweze kutembea, nirudi shule nisome kama wenzangu,” alisema Norat
huku akitokwa na machozi.
Kwa kuwa Norat hana simu, watakaopenda kumsaidia wakawaone maofisa wa ustawi wa jamii
Muhimbili watawaunganisha naye.
No comments:
Post a Comment