STORI: MAKONGORO
Kwa kweli duniani kuna mateso, lakini ya mtoto huyu yatima ni makali na maisha yake yapo hatarini kama hatawahi kupata matibabu. Fuatilia mkasa wake hapa chini ambao naamini utakuhuzunisha.
Kijana Twaha Sultan (16) ambaye ni yatima mkazi wa Kipawa Karakata, Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam akisimulia mkasa wake alikuwa na haya ya kusema:Akionyesha nyama ya ajabu iliyomuota kijana.
“Ndugu zangu, kufuatia maradhi ya ajabu yanayonisumbua sina raha ya maisha, niheri ningewafuata wazazi wangu waliotangulia mbele ya haki nikapumzike.“Nimekuwa mtu wa maumivu wakati wote, kulala na kula kwangu ni shida tupu mbaya zaidi ndugu ninaoishi nao hawana uwezo.
“Naamini kama wangekuwa na uwezo huenda ningekuwa nimepona maradhi haya yaliyoanza kama utani baada ya kunipeleka katika hospitali kubwa na kupatiwa tiba ya uhakika, kwa kweli nateseka jamani!
“Naumia zaidi ninapowaona vijana wa umri wangu wakiwa wanasoma na wenye furaha, wakati mimi nateswa na haya maradhi ambapo nisipopata tiba hatima yangu itakuwa kifo.
“Kabla ya kuanza kuugua, nilikuwa naishi na wazazi wangu huko Majengo, mkoani Tanga, bahati mbaya mwaka 2000 walitengana.
“Kufuatia kutengana kwao, mama alinichukuwa tukaja hapa jijini Dar kwa mama mkubwa tukaanza maisha mapya bila baba.“Tukiwa tunaendelea na maisha, Desemba mwaka huo, mama mkubwa aliugua na kufariki dunia, kifo chake kilikuwa pigo kubwa kwetu kwani tulikuwa tukimtegemea kwa kila kitu.
“Kufuatia tuliyekuwa tukimtegemea kufariki, mimi na mama tulianza kuishi maisha ya kubangaiza, ilipofika Mei 21, 2002 mama naye akafariki dunia baada ya kuuguwa kwa muda mfupi.
“Nilibaki peke yangu, babu alinichukuwa tukaenda kuishi Banana, Ukonga lakini haukupita muda mrefu aliugua na kufariki dunia na kuniacha nikiwa darasa la tano katika Shule ya Msingi Kitunda.
“Baada ya babu kufariki, nilikosa pa kuishi ilibidi nichukuliwe na babu mwingine aliyekuwa akiishi Korogwe, Tanga. Hata hivyo, babu huyo hakuwa na uwezo kwani alikuwa mzee sana, alifariki akiwa na umri wa miaka 78.
“Wakati babu anakufa ndipo nilianza kupata uvimbe kiunoni kwa nyuma.
“Awali nilidhani ungeisha lakini kadiri siku zilivyosonga mbele uliongezeka.
“Nikawa napata maumivu makali na kushindwa kujisaidia haja ndogo, kwani mkojo ulikuwa hautoki. Siku moja nilikwenda kwa mwenyekiti wa kijiji chetu cha Mgombezi ili anisaidie matibabu. Aliniandikia barua ya kuomba fedha kwa watu lakini sikufanikiwa.
.....akizidi kuonyesha kwa ukaribu.
“Nilipoona hali si nzuri na sina fedha, niliamua kwenda Hospitali ya Wilaya Korogwe (Magunga), nikalazwa kwa wiki mbili. Walitoboa tumbo na kuniwekea mpira wa kutolea haja ndogo, cha kushangaza maumivu yakazidi kuwa makali zaidi.
“Ndipo mtoto wa marehemu mama mkubwa, Salha Magamba alisikia kilio changu akanitumia nauli na kuja tena hapa kwake Dar.“Nilimkuta anaishi maisha duni kwa kutembeza biashara ya mkononi huku akiishi katika chumba kimoja na mwanaye. Mei 14, mwaka huu alinipeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili kutibiwa ambapo madaktari waliangalia jinsi ya kuweka mpira vizuri. Wakati huo uvimbe nao ulikuwa mkubwa karibia kilo mbili na nusu.
“Nililazwa Jengo la Kibasila Wadi ya 14, nilifanyiwa kipimo cha CT Scan lakini vipimo vingine niliambiwa vibovu. Dada alinipeleka Hospitali ya Tumaini (Dar) ambapo kipimo kilikuwa shilingi 200,000 kwa hiyo sikufanyiwa kwa kukosa fedha hizo.
“Kuanzia hapo nimekuwa nikibadilishiwa mpira kila baada ya wiki mbili kwa shilingi 30,000. Kwa upande wa uvimbe mgongoni ambao unaniuma kupita kiasi bado matibabu yake kwani nasubiri majibu, sijui itakuwa shilingi ngapi!”
Ndugu msomaji, bila shaka umesikia kilio cha kijana Twaha. Kwa kifupi anahitaji sana msaada ili kuokoa maisha yake. Kama umeguswa msaidie fedha kupitia namba 0713-970 491 au 0789-288 743.
No comments:
Post a Comment