Wezi wa vyuma chakavu wameiba karibu kilomita 10 za mataruma
ya reli katika njia ya reli inayofanya kazi, na kusababisha hasara ya takriban
dola milioni 2.3.
Mataruma hayo yaliibwa katika reli inayopitisha treni kutoka
Johannesburg kwenda katika karakana zilizopo kwenye mji wa Nigel, limeripoti
gazeti la The Star. Watu watano wamefikishwa mahakamani baada ya "kukutwa
kwenye eneo la tukio" na walinzi waliokuwa wakifanya doria katika reli
hiyo.
"Ni wataalam, hawafanyi makosa," amesema Thumbu
Mahlangu, mjumbe wa kamati ya usafiri. Msemaji wa idara ya reli Mike Asefovitz
amesema: "Hawa si watu wadogo. Kuchukua uzito kama huu na kukata vyuma,
unahitaji vifaa maalum." Vyuma hivyo vimeripotiwa kuwa na thamani ya dola
120,000 katika soko la vyuma chakavu.
Wizi huo umesababisha treni mpya 34 kukwama katika karakana,
ambapo zilitakiwa kuanza kazi hivi karibuni, na wafanyakazi karibu 700 wapo
hatarini kupoteza ajira zao. Wizi wa vyuma ni tatizo kubwa Afrika Kusini
linalosababisha hasara ya kiuchumi ya mamilioni ya dola kila mwaka.
No comments:
Post a Comment