Mjumbe wa Bunge la Katiba, Ali Mohamed Kessy ambaye pia ni
Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM) akiwatangazia waandishi wa habari kuunga mkono
muundo wa serikali tatu uwepo katika Katiba Mpya, mjini Dodoma jana. Katikati
ni Mwenyekiti wa Kamati namba moja ya bunge hilo, Ummy Mwalimu na Makamu wake,
Prof Makame Mbarawa ambao walimwita Kessy kumtaka kukanusha kuhusu taarifa yake
ya kuwapo tatizo la akidi kwenye vikao vya
Habari hii kutoka kwenye gazeti la Mwananchi
Jana ilikuwa kama sinema pale viongozi wa Kamati Namba Moja
ya Bunge Maalumu walipojikuta wakibishana na mjumbe wao mbele ya waandishi wa
habari, huku siri za mambo ya ndani ya vikao zikianikwa hadharani.
Kamati hiyo inaongozwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Makamu wa
Rais, Ummy Mwalimu na makamu wake ni Waziri wa Sayansi na Teknolojia, Profesa
Makame Mbarawa, huku ikiwa imesheheni vigogo wengine wakiongozwa na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda.
Viongozi wengine katika kamati hiyo ni Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Uhusiano na Uratibu), William Lukuvi, Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Rais (Utawala Bora), George Mkuchika na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga
Taifa, Dk Hussein Mwinyi.
Wamo pia Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid,
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka na Naibu Waziri wa Maendeleo ya
Jamii, Jinsia na Watoto, Dk Pindi Chana.(P.T)
Jana asubuhi, Mwalimu na Profesa Mbarawa walifika mbele ya
waandishi wa habari katika Hoteli ya St Gasper wakiwa wameambatana na mmoja wa
wajumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Nkasi Kaskazini (CCM), Ally
Keissy.
Lengo la mwenyekiti na makamu wake lilikuwa ni kumbana
Keissy ili akanushe taarifa aliyoitoa juzi kwenye moja ya televisheni kwamba
kamati hiyo inaongoza kwa kuvunja kanuni hasa katika suala la akidi ya vikao
kutotimia.
Sinema ilivyoanza
Walipofika mbele ya waandishi wa habari, Keissy alipewa
fursa ili akanushe taarifa yake, lakini alibadili mada na kuanza kuzungumzia
masuala ya muundo wa Serikali na Bunge, huku akisema yeye ni muumini wa
serikali tatu na siyo mambo ya serikali mbili zinazopendekezwa na wengi kutoka
katika chama chake.
Kauli hiyo iliwashtua Mwalimu na Profesa Mbarawa ambao
walianza kumkatisha ili asiendelee.
"Keissy sikukuitia mambo hayo, huu ni mkutano wangu,
naomba ukanushe nilichokuitia, hayo utazungumza baadaye tafadhali sana,"
alisema Mwalimu.
Wakati huo Profesa Mbarawa na waandishi wa habari
waliokuwapo walivunjika mbavu kwa vicheko, huku yeye akiendelea kusisitiza
kwamba ni muumini wa Tanganyika.
Wakati akisema hayo, Profesa Mbarawa naye aliingilia kati na
kumtaka Keissy kueleza kilichompeleka hapo huku akimtaka aache kelele za
kupotosha wananchi kwa kuwa anachosema siyo kweli.
Alipopewa nafasi ya kuzungumzia jambo hilo, Keissy alisema:
"Jana (juzi), mimi nilihesabu mara mbili nikaona Zanzibar hawajatimia
lakini kumbe mmoja nilimfanya akawa mtu wa Tanganyika, kwa hilo nilighafilika,
lakini mle ndani mambo siyo mazuri," alisema Keissy.
Kabla hajaendelea Mwalimu alidakia na kumtaka anyamaze kimya
kwa kuwa huo haukuwa mkutano wake, ili yeye (Mwalimu) aendelee kueleza mambo
yaliyojiri ndani ya kamati.
"Jamani waandishi si mnaona amekanusha, huu ni mkutano
wangu na yeye sitaki azungumze mambo ya mle ndani kwa kuwa msemaji ni mimi au
makamu wangu au mtu yeyote atakayeteuliwa na mwenyekiti, sasa
tunaendelea," alisema Mwalimu.
Mara baada ya Mwalimu kutoa taarifa ya kamati yake kwa
waandishi wa habari na kumaliza kujibu maswali, alinong'ona na Profesa Mbarawa
na hapo wakampa nafasi Keissy ili azungumze kwa ufupi mambo yake lakini
palepale mbele yao.
Kauli za Keissy
Akitumia fursa hiyo, Keissy alisema: "Kuna mambo
yanafanywa mle ndani ambayo mimi na wenzangu wengine tunalazimishwa,
hatukubaliani nayo likiwamo suala la kuizika Serikali ya Tanganyika wakati wa
upande wa pili (Zanzibar) wanapewa nafasi na kunufaika na rasilimali za nchi
hii, ndugu zangu huu ni uonevu."
Alisema uonevu huo umekuwa mkubwa kwa wabunge wa Tanzania
Bara ukilinganisha na wenzao wa Zanzibar ambao alisema wanakula fedha nyingi za
bure ilihali hawafanyi kazi za Tanganyika.
"Ndugu zangu, hapa tusidanganyane, we fikiria watu
zaidi ya 50 wanatoka kule Zanzibar na kuja kutuamulia mambo yetu, hii si halali
hata kidogo. Haiwezekani mtu wa Zanzibar akaja kuzungumzia masuala ya Nkasi
wakati hayajui," alisema.
Alisema kuwa msimamo wake siku zote ni serikali tatu na
kwamba hatayumbishwa na vitisho au jambo la aina yoyote hata kukiwa na
kulazimishwa.
Mbunge huyo alisema kuwa kutakuwa na urahisi wa kuongoza
Serikali kama Tanganyika itapewa hadhi yake kuliko ilivyo sasa kwa serikali
mbili zinazopigiwa upatu.
Kwa mapendekezo yake alisema ni vyema likawepo Bunge la
Tanganyika, Bunge la Zanzibar na kisha miongoni mwa wabunge hao, wachaguliwe
wachache kuunda Bunge la Muungano.
Aliendelea kusisitiza kuwa wabunge kutoka Zanzibar
wanawanyonya wenzao wa Tanzania Bara kwa kila kitu kauli ambayo ilionekana
kumkera Profesa Mbarawa na kuamua kumkatisha asiendelee kuzungumza.
Wakati akiendelea kuzungumza, viongozi hao walimkatisha tena
na kumwambia akubali waondoke pamoja kuendelea na vikao vya kamati. Baada ya
hapo, Mwalimu na Profesa Mbarawa walinyanyuka na kuanza kuondoka, lakini Keissy
alisimama na kuendelea kuzungumza na waandishi wa habari.
Baada ya kuona anaendelea, Profesa Mbarawa alirudi na
kumshika mkono Kessy huku akisema; "Mheshimiwa Keissy twende bwana, maana
ukimwacha huku huyu atazungumza mambo mengi."
Wakati akiondoka eneo hilo, Keissy alipaza sauti akiwaambia
waandishi wa habari: "Angalieni tunavyodhibitiwa, lakini msimamo ni huo
wala sitayumba ngoja tukaendelee lakini mimi ndiyo mtoa habari namba
moja."
Msimamo wa serikali tatu ni wa Umoja wa Katiba ya Watanzania
(Ukawa) waliosusia Bunge.
Chanzo:Mwananchi
No comments:
Post a Comment