skip to main |
skip to sidebar
Jopo la usuluhishi Katiba Mpya latoa ripoti ya utafiti wa kukwama kwa mchakato wa katiba mpya
JOPO la wataalamu wa masuala ya katiba na usuluhishi wa migogoro,
limesema chimbuko la matatizo yaliyojitokeza kwenye Bunge Maalumu la
Katiba ni kutozingatia misingi ya Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na
Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Limeshauri Bunge hilo linalotarajia kuanza tena Agosti 5, mwaka huu
kuheshimu Rasimu ya Katiba na kuifanya kuwa ndio msingi wa
mjadala
katika bunge hilo ili kunusuru mchakato huo na baadaye Tanzania iweze
kupata katiba iliyo bora.
Jopo hilo linalofanyakazi chini ya Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA),
linaundwa na maprofesa watatu wakiongozwa na Profesa Patrick Lumumba,
kutoka Shule ya Sheria ya Kenya, Bertha Koda wa Taasisi ya Taaluma na
Maendeleo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na Gaudens
Mpangala kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Ruaha Iringa.
Mbali na hilo, pia wameshauri Umoja wa vyama vinavyotetea Katiba ya
Wananchi (Ukawa) kurudi bungeni katika kikao kinachotarajiwa kuanza
Agosti 5, mwaka huu na kuendelea na majadiliano kwa msingi wa Rasimu ya
Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Profesa Lumumba alisema, Tanzania ni nchi ya mfano katika kulinda
amani na utulivu katika nchi zote za Afrika hivyo kushindwa kupata
katiba bora kunaweza kuiondolea sifa hiyo.
Profesa Lumumba ambaye alizungumza Kiswahili fasaha na mifano kadhaa,
alisema jambo muhimu walilobaini katika utafiti wao ni kwamba,
Watanzania wengi wanataka Katiba Mpya yenye kulinda maslahi yao.
Akitoa ripoti ya utafiti kuhusu kutofautiana kwa wajumbe na
kusababisha tishio la kukwama kwa mchakato wa Katiba Mpya, Mwenyekiti wa
JUKATA, Deus Kibamba, alisema chimbuko la matatizo hayo ni Bunge
Maalumu kuibeza na kuiponda Rasimu iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko
ya Katiba.
Tatizo lingine alisema lilitokana na mazingira ya uzinduzi wa Bunge
lenyewe, mjadala kugubikwa na lugha zisizostahili zikiwemo za matusi,
kukebehiana, kubaguana na kukashifiana pamoja na upungufu katika sheria
ya Mabadiliko ya Katiba hususan muundo wa Bunge Maalumu la Katiba.
Katika utafiti huo, jopo hilo limeshauri kanuni zilizopo za kuendesha
Bunge hilo ziangaliwe upya ili ziweze kusaidia kuendesha vikao kwa
ufanisi.
“Kamati ya Maridhiano ndani ya Bunge imeonekana kuwa na upungufu,
hivyo tunashauri liundwe jopo la watu 15 nje ya bunge wanaoheshimika na
kuaminika kitaifa, wanaweza kuchaguliwa kutoka makundi ya wanasiasa
wastaafu, viongozi wa dini, asasi za kiraia na wanataaluma.
“Kazi yake itakuwa ni kusaidia kutatua matatizo yanayojitokeza bungeni
na ambayo bunge lenyewe litashindwa kutatua,” alisema Kibamba.
Katika hatua nyingine wataalamu katika ripoti yao wameshauri Bunge la
Katiba lirejee kwenye sheria ya mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2012,
kifungu cha (37) kinachotamka wazi kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
itavunjwa na Rais baada ya kura ya maoni.
source: gazeti Mtanzania
No comments:
Post a Comment