Jumanne Ngoma: Mgunduzi wa tanzanite anayetaabika
- Pia amegundua madini ya jasi yanayotengeneza saruji
- Apigania kupata sehemu ya mauzo yake bila mafanikio
- Mkubwa serikalini alimpora sarafi yake Soko la Dunia
- Ahoji iweje Williamson alipwe kwa kugundua almasi?
Tanzanite ni
madini ghali duniani yanayozalishwa nchini Tanzania pekee. Mwandishi
Wetu MAYAGE S. MAYAGE amefanya mahojiano na mgunduzi wa madini hayo,
Jumanne Ngoma kijijini kwake Makanya, Same, Kilimanjaro. Katika sehemu
hii ya kwanza ya makala, pamoja na mambo mengine, Ngoma anaeleza jinsi
alivyodhulumiwa haki yake na jitihada anazoendelea kufanya ili walau
familia yake ifaidike na sehemu ya mauzo ya madini hayo.
“MAONI yangu ni kuwa utundu na uvumbuzi popote duniani, hulipwa na
unatiliwa thamani sana katika nchi za kikabaila na kijamaa. Pendekezo
langu, alipwe haki zake zote anazostahili.”
Hilo ni dokezo la aliyekuwa Msaidizi wa Rais (Uchumi), Profesa Simon
Mbilinyi, katika jalada lililokuwa na barua ya Jumanne Mhero Ngoma,
ambayo alikuwa akiiomba Serikali imlipe haki yake ya kuwa mgunduzi wa
madini ya tanzanite ambayo yametokea kuwa na thamani kubwa sana katika
soko la dunia.
Ngoma, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 68, ndiye mgunduzi wa madini
hayo ambayo kama Serikali ingekuwa makini tangu ayagundue mwaka 1967,
yangekuwa yameiweka nchi hii katika ramani nyingine kabisa ya kiuchumi.
Hata hivyo, pamoja na dokezo hilo la Ikulu, la Oktoba 8, 1980, tena
kutoka kwa Mshauri wa Rais katika Masuala ya Uchumi, Ngoma aliambulia
hundi ya Sh 352,448.25 tu kutoka serikalini, ambayo ililipwa kutokana na
ushauri huo.
Kana kwamba Serikali inatambua, na wala haina shaka juu ya ugunduzi wake
huo, iliendelea kumuenzi Ngoma kwa kazi yake nzuri hiyo, kwa kuwa
miongoni mwa watu waliotunukiwa tuzo ya ngao na cheti, pamoja na fedha
taslimu Sh 50,000 katika sherehe za Mei Mosi, zilizofanyika kitaifa
mkoani Mbeya mwaka 1984.
Kwa mujibu wa Ngoma, heshima hiyo aliyopewa na Serikali ilikuwa
inaambatana na safari ya nje, ya kwenda kutembelea soko la dunia la
tanzanite pamoja na kuzuru viwanda maarufu duniani vinavyotengeneza
bidhaa zinazotokana na madini hayo ya tanzanite.
Hata hivyo, katika hali ya masikitiko makubwa, Ngoma anasema safari hiyo
hakuwahi kuipata, na badala yake mjanja mmoja mkubwa tu katika Serikali
hiyo ya Awamu ya Kwanza, tena anayemtaja kwa jina, ingawa kwa sasa ni
marehemu, aliipora safari yake hiyo kimya kimya, na akampeleka mtoto
wake wa kiume, ambaye bila aibu alisafiri kwa jina halisi la Jumanne
Ngoma, kama mgunduzi wa tanzanite.
Ngoma aliugundua vipi ujanja wa mtu huyo? Anasimulia: “Baada ya
kukabidhiwa ngao, cheti na kiasi hicho cha fedha (Sh 50,000) na Mzee
Rashid Kawawa kule Mbeya, aliniambia nikishafika nyumbani nijiandae,
Serikali ilikuwa imeniandalia safari (tour) ya kwenda kutembelea nchi
mbalimbali zinazosifika kwa kuwa na migodi ya madini huko Ulaya, soko la
dunia la tanzanite na viwanda vinavyotengeneza bidhaa zitokanazo na
tanzanite.
“Nilifika nyumbani kwangu hapa Makanya (Same, Kilimanjaro), nikajiandaa
nikisubiri barua ya kuitwa Dar es Salaam tayari kwa safari. “Siku moja
nikiwa shambani, alikuja mtu mmoja akaacha barua hapa. Nilipotoka shamba
watoto wakaniambia; baba kuna barua yako hapa…nikajua, safari yangu
imeiva. Niliingia ndani nikatulia, na kisha nikaifungua. Humo nikakuta
boarding ticket (kipande kinachomruhusu abiria kuingia ndani ya ndege)
zilizokwishatumika, kadi ya chanjo ya homa ya manjano na vikorokoro
vingine vinavyoelezea nchi na mahali mtu huyo alikotembelea, vyote
vikiwa na jina langu.”
Kwa hakika, ukimsikiliza Ngoma katika masimulizi yake juu ya vitimbi
alivyofanyiwa na mamlaka zinazohusika na madini pamoja na Serikali kwa
ujumla, kama ni mtu unayeguswa, unaweza ukatokwa machozi.
Katika muda wote wa mazungumzo haya yaliyofanyika nyumbani kwake,
kijijini Makanya, Same, mkoani Kilimanjaro, Ngoma alikuwa ni mtu wa
kulaani, kulalamika na kujiapiza.
Na hafichi kuonyesha ghadhabu yake kwa michezo yote michafu anayofanyiwa na wasiomtakia mema.
Anasema kwa mfano: “Kwa bahati nzuri sana, wote walionifanyia vitimbi na
kunizibia riziki yangu, wamekufa vifo vibaya. Wengi wao hawapo duniani.
Mungu ananilipa, anawaadhibu na naamini ataendelea kuwaadhibu wote
wanaokalia haki yangu.”
Hata baada ya kupata taarifa ya kufikiwa na Rai, ili pamoja na mambo
mengine azungumzie ugunduzi wake huo, Ngoma hakuwa na hamu ya kufanya
hivyo, akisema haoni faida yoyote ya yeye kuendelea kuzungumza na vyombo
vya habari juu ya ugunduzi wake huo, kwa maelezo kwamba hafaidiki
chochote, si tu kutoka kwenye vyombo vyenyewe vya habari, bali hata
serikalini.
Kwa mfano, katika moja ya karatasi alizokuwa ameandika maelezo yake kwa mkono wake tayari kwa mahojiano haya, Ngoma anaandika:
“Karibu sana kijijini kwetu hapa Makanya, jisikie uko nyumbani. Mimi
ndiye Jumanne Mhero Ngoma mgunduzi wa madini ya tanzanite. Nimehojiwa
mara nyingi sana na magazeti mbalimbali nchini pamoja na Radio Tanzania
Dar es Salaam (RTD), lakini sijaona faida ya mahojiano hayo.
“Nimehojiwa na waandishi wa habari wa BBC (Shirika la Utangazaji la
Uingereza) mwaka jana, nikiwa Arusha, ambao ni Abdallah Majura na Tido
Mhando, na mahojiano hayo yakarushwa hewani na BBC, London. Nawe leo
unanifuata. Je, ni kwa faida ya kuuza magazeti yenu tu au na mimi
nitafaidikaje juu ya mahojiano haya?”
Kwa ufupi, Ngoma alitaka kwanza ahakikishiwe ni kifuta jasho kiasi gani
ambacho angelipwa kwa mahojiano haya. Na kwa kuwa mwandishi hakuwa
amejiandaa kwa hilo, na kutokana na ukweli kwamba swali lenyewe hilo la
malipo lilikuwa ni la kiutawala, ilibidi ifanyike juhudi kidogo
kumshawishi ili kufanikisha mahojiano haya.
Kwa wanaokifahamu kijiji cha Makanya, wanatambua kwamba moja ya sifa za
kijiji hicho ni kuwa na madini mengi ya jasi (gypsum), ambayo ni muhimu
sana katika viwanda vya saruji nchini kwa uzalishaji wa saruji. Aidha,
madini hayo hutumika katika utengenezaji wa chaki na POP zinazotumika
hospitalini.
Mgunduzi wa madini hayo ya jasi kijijini hapo si mwingine, bali ni
Ngoma. Huyo ndiye alikuwa msambazaji (supplier) wa kwanza wa madini hayo
wakati Kiwanda cha Saruji cha Wazo Hill kilipoanza uzalishaji wa bidhaa
hiyo miaka ya katikati ya sitini.
Kutokana na ugunduzi wake huo wa jasi, madini ambayo ndiyo tegemeo la
kiuchumi kwa wakazi na pato la Kijiji cha Makanya, uongozi wa kijiji
hicho, katika kumuenzi Ngoma, umemsamehe kushiriki katika shughuli
yoyote ya uchangiaji wa miradi ya maendeleo kama vile shule, zahanati
na/au miradi ya maji.
Anasema: “Nashukuru sana, uongozi wa kijiji na wanakijiji wenzangu
wanatambua mchango wangu katika maendeleo ya hapa. Katika kuenzi
ugunduzi wangu wa madini ya jasi, wamenisamehe nisishiriki aina yoyote
ya ‘msaragambo’ (harambee ya kuchangia maendeleo).”
Hata hivyo, pamoja na Ngoma kuenziwa na wanakijiji wenzake kuhusu
ugunduzi wake huo wa madini ya jasi, madini ambayo kwa kiasi kikubwa
yamechangia katika kukua kwa uchumi wa wanakijiji cha Makanya, ana
malalamiko mengi kwa watawala wa nchi hii kwa kutotaka afaidike na
ugunduzi wake madini ya tanzanite.
Anasema juhudi zake zote za kutaka Serikali imsaidie kumpatia Hati ya
Ulindaji wa Kazi za Kigunduzi (Intellectual Property Protective – IPP),
ambayo ingemsaidia kutambuliwa kimataifa na hivyo kufaidika na ugunduzi
wake huo kama ambavyo mgunduzi wa almasi ya Mwadui, Williamson
anavyofaidika, zimegonga mwamba.
Katika kilio hicho, anasema: “Kama familia ya Williamson, mgunduzi wa
almasi Mwadui, inavyofaidika na ugunduzi huo, nami naomba Serikali
isimamie kwa kuwapo maandishi yanayosema kwamba nitakuwa napata asilimia
fulani ya mapato yanayotokana na mauzo yote ya tanzanite kwa maisha
yangu yote na kizazi changu hadi madini hayo yatakapokwisha.
“Msajili wa Kulinda Haki za Ugunduzi, aliniandikia barua akisema
ugunduzi tu wa madini katika ardhi, hauwezi kupewa Hati ya Kulinda Kazi
za Ugunduzi. Sawa; lakini mbona Williamson yeye alipewa? Yeye aligundua
almasi ya Mwadui angani, kwenye mwezi au baharini? Si ni katika ardhi
hii hii ya Tanzania, ambamo nami nimegundua tanzanite?”
Ni katika mkanganyiko huo, Ngoma alitumia fursa hii kuiomba rasmi Kamati
ya Madini ya Rais, chini ya Jaji Mark Bomani, kabla ya kuhitimisha kazi
yake hiyo, imwite mbele ya kamati hiyo ili aweze kuwasilisha maoni yake
juu ya nini kifanyike katika sekta ya madini.
Lakini pia, Ngoma haachi kulaani baadhi ya kauli za viongozi waandamizi
serikalini ambao wamekuwa wakimwekea ‘ukuta’ kila anapofuatilia haki
zake, wakisema ni mtu asiyetosheka hata akipewa fedha inayolingana na
Mlima Kilimanjaro.
“Hivi Sh 352,448.25, nilizopewa na Serikali ndizo ninazosimangiwa kwamba
sitosheki hata nikipewa fedha zinazolingana na Mlima Kilimanjaro? Kama
ni kutosheka, kwa nini viongozi hao hao wao hawataki kutosheka na
madaraka yao?
“Mbona wamestaafu, lakini juzi tumewaona wakichukua fomu za kuomba
uongozi wa juu katika chama?” anahoji Ngoma bila kutaja jina la kiongozi
wa ngazi ya juu katika Serikali ya Awamu ya Tatu, ambaye alipata
kumwambia kwa ukali kwamba hatosheki hata akipewa fedha zinazolingana na
Mlima Kilimanjaro.
Ngoma aliyagundua vipi madini ya zoisite, ambayo baadaye yalikuja
kubadilishwa jina na kuitwa tanzanite kutokana na ushauri wa kampuni
moja ya Kimarekani, iliyokuwa ikifanyia biashara yake mjini Arusha,
ikijulikana kwa jina la Tiffany kwa Serikali?
Je; unayajua maisha anayoishi mgunduzi huyo wa tanzanite, na ndoto zake
alizonazo katika umri wake wa sasa, juu ya ugunduzi mwingine wa madini,
yakiwamo hayo ya tanzanite?
Unafahamu kama Ngoma ana kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya
Dar es Salaam dhidi ya kampuni ya kigeni ya AFGEM, kwa sasa Tanzanite
One, akitaka kampuni hiyo imlipe fidia ya Sh bilioni mbili taslimu kwa
madai kwamba kampuni hiyo, kwa makusudi tu, imepotosha katika jarida lao
linalochapishwa nchini Afrika Kusini, kwa kuandika kwamba mgunduzi wa
tanzanite ni mtu mmoja anayetajwa kwa jina la Ali juu ya watu, na si
yeye Jumanne Ngoma? Soma yote hayo katika toleo letu lijalo la Rai.
Chanzo: Gazeti la RAI |
http://monthlyyouth.com/?ref=413286
ReplyDelete