Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, September 19, 2014

Baadhi ya vigogo Simba, Yanga watajwa Kuihujumu Taifa Stars

                    Kikosi cha Taifa stars.

Na Mwandishi wetu

SIRI za kushindwa kwa timu ya soka ya taifa kufuzu katika michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON).

Siri hiyo ya kukwama kwa timu ya taifa kwenye michuano ya (AFCON), inadaiwa kutokana na   hujuma zilizofanywa na kundi la watu wachache kwa lengo la kumwonesha Rais wa TFF, Jamal Malinzi hawezi kuongoza shirikisho hilo na kuipa mafanikio Stars.


Wahujumu hao wa soka nchini, wanadaiwa kutoka katika vilabu vikubwa vya soka nchini ambao kwa sasa majina yao yamehifadhiwa.

Uchunguzi uliofanywa tangu timu ya soka ya taifa ilipotolewa kwenye michuano hiyo na timu ya soka ya Msumbiji, unaonyesha kuwa hilo limeapa kufanya hujuma dhidi ya timu ya taifa ili kumkomoa Malinzi kwa sababu ya chuki na minyukano ya makundi yaliyoibuka wakati wa uchaguzi wa Rais wa TFF.

Habari kutoka ndani ya TFF zinasema kuwa katika mechi mbili na timu ya soka ya taifa ya Msumbuji, waasi hao waliwatumia baadhi ya wachezaji wa stars kucheza chini ya kiwango, wengine kucheza rafu za makusudi na kumwaga fedha kwa mmoja wa waamuzi na matokeo ya mchezo huo yaliishia kwa sare ya bao 1-1.

Katika mchezo wa marudiano uliofanyika wiki mbili baadaye mjini Maputo, Stars ilitolewa kwa kufungwa bao 2-1, huku ikinyimwa penalti na kukataliwa bao lingine katika mazingira ya kutatanisha.

“Katika mechi zote mbili, kundi hilo liliwatumia baadhi ya wachezaji kucheza chini ya kiwango na kumhonga mmoja wa waamuzi fedha. Fedha hizo zilikabidhiwa kwa mchezaji mmoja wan je anayecheza soka la kulipwa katika moja ya vilabu vikubwa nchini ambaye naye alimkabidhi mwamuzi huyo aliyeiua Stars,” alisema mtoa habari wetu.

Uchunguzi umebaini kuwa tayari Serikali imeagiza kuunda tume ya kuchunguza kashfa hiyo na kuapa kuwachukua hatua dhidi ya watakaobainika kuhusika na uasi huo dhidi ya timu ya taifa.

Malinzi aliyeingia madarakani mwishoni mwa mwaka jana, amekutana na wakati mgumu ndani ya Shirikisho hilo, licha ya kufanya maandalizi makubwa kwa timu hiyo, kuiwezesha kushiriki michuano ya AFCON.

Katika maandalizi ya mwaka huu, stars ilipewa maandalizi makubwa chini ya udhamini mnono wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia kinywaji chake cha Kilimanjaro.

Licha ya udhamini huo, pia Serikali imekuwa karibu na TFF kuhakikisha timu ya soka inafanya vyema na kuondokana na aibu ya kugeuzwa kuwa kichwa cha Mwendawazimu.

Stars mwaka huu ilifanya maandalizi makubwa chini ya kocha wake Mart Nooij kwa kuweka kambi takribani mwezi mzima nchini Botoswana, na pia Tukuyu mkoani Mbeya kwa lengo la kuhakikisha inashiriki AFCON mwakani nchini Morocco.

 “Hii hali inasikitisha sana. Kama mtu ana bifu na Malinzi, hamfanyie yeye lakini sio kuihujumu timu ya taifa. Kwa taarifa yako hao watu wataanikwa muda si mrefu maana wanajulikana,” alisema mtoa habari wetu.

Alipoulizwa juu ya kuwapo kwa hujuma hizo, Rais wa TFF Malinzi, hakukubali wala kukataa na badala yake alisema kama kweli kuna watu wa aina hiyo, taifa litakuwa limefika mahali pabaya.


 “Mimi katika hilo, sina cha kusema, lakini kama kuna ukweli ndani yake, nitasikitika sana, maana hii timu siyo yangu mimi ni timu ya Taifa,”alisema Malinzi.
chanzo Moblog

No comments:

Post a Comment