Wapiganaji wa Kikurdi wanakabiliana vikali na wanamgambo wa
Islamic State katika mji wa mpakani mwa Syria Kobane,huku mashambulizi dhidi ya
wanamgambo hao yanayoongozwa na Marekani yakiendelea.
Mwandishi wa BBC anayeshuhudia vita hivyo amesema kuwa
mashambulizi kadhaa yamefanyika pamoja na milipuko ya gurunedi.
Katika ripoti ya hivi karibuni,makao makuu ya majeshi ya
Marekani yamesema kuwa mashambulizi sita ya angani yameharibu vifaa vya kijeshi
vya kundi la Islamic State katika eneo la Kobane.
Mjumbe wa Umoja wa mataifa nchini Syria ametoa wito kwa
jamii ya kimataifa kuchukua hatua ili kuwazuia wapiganaji wa Islamic state
kuuteka mji huo muhimu.
Steffan de Mistura ameiambia BBC kwamba kutekwa kwa mji wa
Kobane kutasababisha mauaji na janga la kibinaadamu.
Utekaji wa mji wa Kobane utawapa wapiganaji wa Islamic State
udhibiti wa eneo kubwa la mpaka wa Syria na Uturuki,ambao umekuwa ukitumika
kama njia ya wapiganaji wa kigeni wanaoingia nchini Syria pamoja na kuwasaidia
wapiganaji hao kusafirisha mafuta kutoka maeneo inayodhibiti.
Vita vya wiki tatu kuwania udhibiti wa mji wa Kobane
vimesababisha mauaji ya watu 400,huku zaidi ya raia 160,000 wa Syria
wakilazimika kukimbilia nchini Uturuki.
No comments:
Post a Comment