Shirikisho la soka la Afrika CAF limeichagua na kuipatia
nafasi Guinea ya Ikweta kuandaa fainali za kombe la Afrika 2015 kuchukua nafasi
ya Moroko iliyojitoa wiki iliyopita. Awali Rais wa CAF Issa Hayatou alikuwa na
majadiliano yenye manufaa na Rais wa nchi hiyo tajiri ya mafuta Teodoro Obiang
Nguema mjini Malabo kabla ya kufikia hatua ya kuikabidhi nchi yake dhamana
hiyo.
Taarifa ya CAF imethibitisha leo ijumaa kuwa Guinea ya
Ikweta mojawapo ya nchi ndogo barani Afrika imepewa jukumu hilo kubwa la kuokoa
jahazi la michuano hiyo na itashiriki fainali hizo kama ilivyo kawaida ya mwenyeji.
Nchi hiyo yenye kutumia kihispaniola kama lugha ya Taifa
iliandaa fainali za Afrika za mwaka 2012 kwa pamoja na jirani yake Gabon.
Mashindano hayo yatafanyika kuanzia Januari 17- Februari 8 mwakani kwenye miji
ya Bata, Ebebiyin, Mongomo na mji mkuu Malabo. Mwaka 2012 walitumia miji miwili
tu ya Bata na Malabo.
Ratiba kupangwa Malabo
Sherehe za kupanga ratiba ya mechi za fainali hizo
itafanyika mji mkuu wa Malabo mnamo Desemba 3 mwaka huu. Taarifa ya CAF imesema
kuwa Shirikisho hilo linawashukuru watu wa Guinea ya Ikweta, Serikali pamoja na
Rais Ngwema mwenyewe kwa utayari wao wa kuokoa mashindano hayo. Moroko ilijitoa
kaandaa fainali hizo baada ya kuomba CAF isogeze mbele mashindano kwa ajili ya
hofu ya ugonjwa wa Ebola ambao umeenea kwenye nchi kadhaa za Afrika Magharibi
ambazo kwa kawaida hupeleka timu nyingi Zaidi katika fainali za Afrika.
CAF ilikataa mpango huo kwa madai kuwa haijawahi kuahirisha
wala kufuta fainali hizo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1957. Moroko walipewa
hadi jumamosi iliyopita kuthibitisha utayari wao wa kuandaa mashindano hayo
lakini walishindwa kufanya hivyo na CAF ikaamua kufanya mchakato wa kutafuta
nchi ya kuokoa na hatimaye imepatikana hii leo.
Shirikisho hilo limeipa adhabu Moroko ya kutoshiriki fainali
zijazo za huko Guinea ya Ikweta.
No comments:
Post a Comment