Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Tuesday, November 25, 2014

JE, NI KWELI SHILINGI BILIONI 306 ZIMELIWA?

Spika wa Bunge , Anne Makinda.
Nimshukuru Mungu kwa kuniweka hai mimi na wewe msomji wa makala haya, hakika hatuna budi kumshukuru milele.
Wiki iliyopita gumzo la mjini au pengine nchini lilikuwa sakata la akaunti ya Tegeta Escrow ambapo kuna madai kuwa kuna mabilioni ya fedha ‘wakubwa’ wamezichota bila hata kulipia kodi ya nchi.
Zimetajwa kuwa ni shilingi bilioni 306! Ni fedha nyingi sana ambazo eti kuna watu wamegawana! Siamini mpaka niaminishwe kwa ‘data’ zisizo na mashaka yoyote.



Ajabu ni kwamba kuna wakati nilisikia baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali akiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), wakidai kwamba kiasi cha dola za Marekani milioni 250 zilizopaswa kuendelea kuwapo katika ‘Tegeta Escrow Account’ si za serikali, hivyo si mali ya umma.
Lakini nilichanganyikiwa zaidi baada ya kusikia ikisemwa kuwa akaunti hiyo ilifunguliwa na serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na Kampuni ya Independent Power Limited (IPTL)! Nilipigwa na bumbuwazi, vipi fedha ambazo siyo za umma zinafunguliwa akaunti na vyombo vya serikali?
Kwa bahati mbaya sana viongozi wa serikali wamekuwa wakiendelea kurudia kuueneza huo usemi kwamba fedha hizo si mali ya umma. Inasikitisha pia kwamba baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa navyo vikibeba na kusambaza maelezo hayo bila kuhoji na kuchunguza. Inashangaza sana kuona asasi za kiraia nazo zimekaa kimya juu ya jambo hilo zito.
Nilisikia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) ilielekeza kuwapo kwa ukaguzi maalumu kwenye akaunti hiyo ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuwa ndani yake kulikuwapo fedha za umma.
Mimi naamini kwamba kamati hiyo ya PAC ilifanya hivyo kwa kuwa kuna fedha za umma ndani yake vinginevyo ingekuwa haina sababu yoyote ya kufuatilia fedha za watu binafsi. Niwakumbushe tu wasomaji wa safu hi kwamba mwaka 2009 iliyokuwa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) ilitoa maelekezo kwa BoT kutothubutu kutoa fedha hizo. Agizo hilo la POAC lilitokana na sababu kwamba fedha hizo zilikuwa ndani ya hesabu za Tanesco.
Akaunti ya ‘Tegeta Escrow’ ilifunguliwa kutokana na kuwapo kutoelewana kuhusiana na gharama halisi na halali za umeme unaozalishwa na IPTL na kuuzwa kwa Tanesco. Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICSID) katika uamuzi wake wa Februari, 2014 ilitoa hukumu kuonyesha kwamba Tanesco walitozwa kiwango cha juu zaidi ya kilichopaswa kulipwa kwa IPTL.
Kwa uamuzi huo ni dhahiri kwamba fedha zilizokuwa zimehifadiwa kwenye akaunti hiyo maalumu ya Escrow zilipaswa kugawanywa kwa IPTL na Tanesco baada ya hesabu kufanyiwa marekebisho upya kwa viwango halali.
Kwa mujibu wa PAC , hesabu za mwaka wa fedha ulioishia Desemba 2012 za Tanesco zinaonyesha wazi kwamba fedha hizo ni mali ya shirika hilo la umma linalomilikiwa na serikali kwa asilimia 100.
Kwa maelezo hayo na hoja hizo, inakuaje serikali ianze kudai kwamba fedha hizo si mali ya umma? Hivi inawezekanaje kwa fedha za mtu binafsi zikaingizwa katika hesabu za shirika la umma linalomilikiwa na serikali kwa asilimia 100?
Umma una haki ya kukumbushwa kwamba madai hayo yalitolewa pia katika lile sakata la ufisadi maarufu wa EPA unafanana kwa kila hali na huu wa sasa wa ‘Tegeta Escrow’.
Hoja nyingine ni kwamba, Mbunge David Kafulila alisema kwamba Jaji Utamwa wa Mahakama Kuu ya Tanzania hakutoa uamuzi wa kuchukuliwa fedha kutoka akaunti ya ‘Tegeta Escrow’. Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa PAC anasema amepitia kwa makini hukumu ya Jaji Utamwa na kubaini kwamba hakuna popote alipotaja akaunti ya ‘Escrow’.
Hata hivyo, alipopitia muhtasari wa kikao kati ya Tanesco, IPTL na Wizara ya Nishati na Madini, ndipo kwa mara ya kwanza alikuta wametafsiri uamuzi wa mahakama wakidai kwamba fedha zote za ‘Tegeta Escrow’ zipewe Kampuni ya PAP.
Zitto anakwenda mbali zaidi na kudai kwamba wote waliohudhuria kikao hicho kilichojipa mamlaka ya kutafsiri hukumu ya Mahakama Kuu Tanzania, wanapaswa kuchunguzwa na kufikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Lakini nami najiuliza kama hivyo ni kweli, inawezekana vipi uamuzi wa mahakama ukatafsiriwa na kikao cha wizara? 
Tunatarajia kwamba Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), katika ripoti yake iliyofika bungeni imefichua ukweli wa sakata hili . Bunge chini ya Spika, Anne Makinda (pichani), lina kila sababu kupitia sheria yake kujadili hoja hii ili ukweli ubainike kama ulivyoapa na tuondoe hisia binafsi zenye kubebwa na itikadi, chuki na misimamo yetu ya kisiasa. Tuwe wazalendo ili tuweze kusimamia utaifa, jibu lipatikane, shilingi bilioni 306 zimeliwa? Au kodi ya nchi nayo imeliwa?
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.

No comments:

Post a Comment