Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete.
-Apokea Ripoti, nyaraka na maazimio ya Bunge
-Aagiza Ripoti ya CAG iwekwe wazi hadharani
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete amepokea Ripoti, nyaraka na ushauri wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow na atavifanyia maamuzi
katika wiki moja ijayo.
Rais Kikwete ambaye alianza kazi rasmi jana, Jumatatu,
Desemba 8, 2014 baada ya mapumziko ya kufuatia upasuaji aliofanyiwa mwezi
uliopita, amepokea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG), Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Umma (PAC) na Maazimio ya Bunge
kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow.
Kufuatia kupokea nyaraka hizo, Rais Kikwete ameelekeza kuwa
Ripoti ya CAG iwekwe hadharani kwa ajili ya umma kuweza kuisoma na kujua nini
hasa kimesemwa na kupendekezwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali.
Rais Kikwete ameelekeza kuwa Ripoti hiyo itangazwe kwenye
magazeti yanayosomwa na watu wengi na kwenye mitandao ya kijamii, ili Ripoti
hiyo iweze kupatikana kwa Watanzania wengi.
Rais Kikwete ameanza kupitia na kusoma nyaraka hizo na
katika wiki moja ijayo atazitolea maamuzi kwa maana ya kwamba yale mambo
yanayomhusu yeye moja kwa moja atayatolea maamuzi yeye, yale yanayohusu
Serikali atayatolea maagizo na maelekezo ya namna ya kuyashughulikia.
Wakati huo huo, Rais Kikwete jana, Jumatatu, Desemba 8,
2014, alianza kazi rasmi baada ya afya yake kuimarika kufuatia upasuaji
aliofanyiwa mwezi uliopita.
Mhe. Rais alianza kazi rasmi kwa kumwapisha Mkuu mpya wa
Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa Daudi Felix Ntibenda katika shughuli fupi
iliyofanyika Ikulu, Dar Es Salaam.
Kwa kuanzia Mhe. Rais atakuwa anafanya kazi za ofisini na
kwa muda mchache. Muda na kasi ya kufanya kazi ya Mhe. Rais vitaongezeka kwa
kadri afya yake inavyozidi kuimarika.
Na kwa sababu sasa ameanza kazi, Mhe. Rais ataanza
kushughulikia mambo yale ambayo yamekuwa yanasubiri maamuzi yake.
Rais Kikwete alifanyiwa upasuaji wa tezi dume katika
Hospitali ya Johns Hopkins ya Baltimore, Maryland, Marekani Novemba 8, mwaka
huu na alirejea nyumbani Novemba 29, mwaka huu.
Tokea awasili nyumbani, Mhe. Rais amekuwa anafanya mazoezi
asubuhi na jioni kuimarisha afya yake kama alivyoshauriwa na madaktari.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
9 Desemba,2014
No comments:
Post a Comment