Baada ya utata mzito kutawala kwenye vyombo vya habari juu
ya uhalali wa mtoto wa Mbongo Fleva, Emmanuel Elibariki ‘Nay wa Mitego’ kwa
mzazi mwenzake Siwema Edson, hatimaye kipimo cha vinasaba (DNA) kimetoka na
kumaliza ubishi kwamba
mtoto huyo aitwaye Curtis ni damu halisi ya msanii huyo.
Hivi karibuni, Nay na Siwema ambao walikuwa wapenzi kisha
kumwagana, waligombana na kila mmoja kuzungumza lake juu ya mtoto wao huyo
ambapo Siwema alidai si damu ya Nay wakati msanii huyo alisema ni damu yake.
Licha ya kupokea majibu hayo mazuri kwake, Nay aliyachukua
majibu hayo kwa kuangua kilio cha furaha huku akieleza ya moyoni kuhusiana na
sakata hilo.
“Hili ni swala ambalo lilikuwa linaniumiza kichwa kila
kukicha. Unajua kama mwanaume, mtu akwambie mtoto si wako unadhani ni maumivu
kiasi gani utayapata? Inauma sana, mtu umelea kuanzia mimba hadi mtoto
amezaliwa, si kitu kidogo.
“Namshukuru Mungu kwa majibu kwamba ni damu yangu. Mashabiki
wangu watambue tu kwamba, Curtis ni mwanangu asilimia mia hivyo hakuna ubishi
tena.
“Ujue nampenda sana mwanangu na kwa bahati nzuri huyo ndiye
mwanangu wa kiume pekee, hivyo sikutaka kuruhusu wazo lolote kutoka kwa mtu
mwingine maana hata kama majibu yasingesema kama ni wangu nilikuwa radhi kuishi
naye na kumlea bila kujali hilo kwa sababu tu niliamini siku zote ni mali
yangu,” alisema Nay.
Nay aliingia kwenye utata huo takriban mwezi mmoja uliopita
baada ya kupishana kauli na Siwema ambaye alimfumania akiwa na mwanaume
mwingine nyumbani kwake, jijini Mwanza na kuamua kumchukua mtoto kisha kuishi
naye jijini Dar kwa msaada wa mama yake mzazi.
No comments:
Post a Comment