Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Sunday, October 18, 2015

TAZAMA PICHA:::SIMBA WALIPOITANDIKA MBEYA CITY GOLI 1 BILA


Wachezaji wa Simba wakishangilia kwa staili ya ‘Selfika’ baada ya Juuko Murshiid kufunga bao dhidi ya Mbeya City katika dimba la Sokoine jijini Mbeya. (Picha na David Nyembe)
Kipindi cha kwanza kilianza kwa kasi huku Simba ikifanikiwa kupata kona katika dakika ya kwanza ya mchezo.

Mlinzi wa kushoto wa Simba Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ alipiga mkwaju huo ambao ulimkuta Abdi Banda ambaye aliusukumiza kwa kichwa na kupanguliwa bila mafanikio na mlinda mlango wa Mbeya City, Juma Kaseja ambapo Juuko Murshiid  aliukwamisha nyavu bao lililodumu hadi mapumziko.

Simba walionyesha uhai zaidi katika kipindi cha kwanza baada ya kuongoza wakitaka kuongeza bao lingine ambapo dakika 24 baada ya Mbeya City kushindwa kuitumia vizuri kona waliyopata, Banda alishindwa kabisa kumalizia kazi nzuri iliyofanywa na safu ya kiungo na shuti lake kudakwa vilivyo na Kaseja.

Katika dakika ya 18 ya mchezo Mwinyi Kazimoto baada ya kuwapita viungo wa Mbeya City alijikuta katika wakati mgumu alipochezewa rafu mbaya iliyomfanya atoe machozi licha ya kadi yoyote kutotolewa.

Dakika ya 38 ya mchezo huo uliokuwa wa kuvutia hususani kwa Simba SC walionekana kupiga pasi, Abdi Banda alionyeshwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu mchezaji wa Mbeya City.

Dakika moja baadaye Kaseja aliokoa mkwaju uliolekezwa langoni mwake na viungo wa Simba.

Kipindi cha Pili kilianza kwa kasi ambapo Mbeya City walionekana kuimarika zaidi na kuichezea nusu uwanja Simba huku ukuta shupavu wa Watoto wa Msimbazi chini ya Hassan Isihaka ukionyesha umahiri mkubwa kwa kuzuia hatari zote za Mbeya City.

Kwa upande wao mashabiki wa Simba dimbani hapo walionekana kuwa na furaha muda wote pale camera ya Wadhamini wakuu wa kurusha matangazo kwa njia ya runinga Azam TV iliyokuwa ikiendeshwa kwa ‘remote’ ikielea angani huku mashabiki wa Mbeya City wakibaki kimya.

Aidha mashabiki wa Simba walionekana kufanya ishara ya ‘mabadiliko’ walipokuwa dimbani hapo hali iliyowanyong’onyeza mashabiki huku wakiimba ‘Simba! Simba! Simba! Pompo! Eee! Kidedea! Pompo! Eee! Kidedea! Pompo! Eee! Kidedea!

Aidha mashabiki walivamia uwanja na kwenda katika basi la Simba kutaka kuwapongeza wachezaji wao kwa nzuri waliyoionyesha dhidi ya Mbeya City.

Simba walifanya mabadiliko wakimtoa kipindi cha pili wakiwatoa Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Abdi Banda  na kuwaingiza Awadh Juma, Joseph Kimwaga, Peter Mwalyanzi.

Kwa upande wake Kocha Kerr, alisifia Mbeya City kwa uimara iliyouoneysha licha ya kuwafunga lakini alisisitiza kuwa alama tatu kwake ni muhimu na timu yake imelilinda bao lake.

Kocha Mingange alisema makosa ameyaona, na kwamba walipata nafasi nyingi lakini walishindwa kuzitumia hivyo wataangalia katika dirisha dogo la usajili ni kwa namna gani wanaweza kukiunda kikosi vizuri kwa ajili ya ngwe ya lala salama.

Boban awa kivutio
Licha ya mbembwe nyingi za mashabiki wa Simba na Mbeya City kabla ya mtanange huo lakini habari kubwa ilikuwa kumwona kiungo mahiri wa zamani wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ akiwa katika uzi wa zambarau na nyeupe kwa udhamini wa RB Battery unaovaliwa na Mbeya City ambaye alitolewa katika dakika ya 48 akiingizwa Hamad Kibopile.

Hata hivyo alionyesha uanamichezo pale alifanyiwa ‘sub’ alikwenda kumshika mkono na kumkumbatia Mwinyi Kazimoto hali iliyoibua shangwe dimbani hapo.

Waikumbuka 17 Oktoba 1993
Simba iliendelea kuwapa raha mashabiki wake na wapenzi wa kandanda nchini baada ya kuwafumua Atlético Sportive Aviáco (ASA) ya Angola mabao 3-1 katika dimba la taifa jijini Dar es Salaam. Mabao ya Simba yalifungwa na Edward Chumila,  Abdul Ramadhani ‘Mashine’ na Malota Soma katika mchezo huo wa awali wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Unakumbukwa kwasababu ya ufundi ulioonyeshwa siku hiyo ukifanana na dhidi ya Mbeya City jana katika mtanange wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Vikosi
Mbeya City

Kikosi cha Mbeya City kilichowavaa Simba SC Okotba 17 , 2015 katika dimba la Sokoine jijini Mbeya. Simba ilishinda 1-0 Picha na Kenneth Ngelesi)

Juma Kaseja, Hassan Mwasapili, John Kabanda, Yohana Moris, Haruna Shamte, Stephen Mazanda, Christian Sembuli, Temi Felix, Haruna Moshi ‘Boban’,Joseph Mahundi.

Akiba
Hannington Kasyebula, Hamad Kibopile, Rajabu Seif, Geofry Mlawa, Seleman Magoma, Richard Peter, Abdala Seif


Coach: Meja Abdul Mstaafu Mingange.

Simba SC
Kikosi cha Simba SC kilichowavaa Mbeya City Oktoba 17 2015 katika dimba la Sokoine jijini Mbeya. Simba ilishinda 1-0 Picha na Kenneth Ngelesi)
Vincent Angban, Mussa Hassan Mgosi, Mohamed Hussein, Hassan Isihaka, Murusid Juuko, Justice Majabvi, Said Hamis Juma, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto, Abdi Banda.
Akiba
Peter Manyika Jr., Peter Mwalyanzi, Awadh Juma, Simon Sserunkuma,, Ibrahim Migomba, Pape Ndaw, Joseph Kimwaga.
Coach: Dylan Kerr 

No comments:

Post a Comment