Nashukuru kwa heshima aliyonipa mtumishi wa Mungu, T.B Joshua kwa kuja
nyumbani kujadili mambo ya taifa, na baadaye kushiriki kwenye sala na
ndugu na familia. Mungu atuongoze. Mungu ibariki Tanzania!"-Edward
Ngoyai Lowassa
Maelezo kwa mujibu wa tovuti ya John Kitime (johnkitime.co.tz)Temitope
Balogun Joshua (T.B. Joshua) alizaliwa tarehe 12 Juni 1963, katika
kijiji kidogo cha Arigidi kilichoko Akoko, Jimbo la Ondo, Nigeria.
Inasemekana mama yake alikaa na mimba kwa miezi 15, kabla Temitope
hajazaliwa.
Katika kabila lake kulikuweko na hadithi ya zaidi ya miaka 100 ambayo
ilitabiri kuwa kuna mtoto atazaliwa katika familia masikini, ambaye
Mungu atamtumia sana, na wengi kule kwao huamini kuwa Temitope ndie
aliyetajwa katika utabiri huo. Siku tatu baada ya kuzaliwa kwake, jiwe
kubwa lilirushwa kutoka kwenye sehemu kulikokuwa kunapasuliwa mawe, jiwe
hilo lilitoboa bati na kumkosa kosa Temitope kwa sentimita chache. Na
ndipo mama yake alimpa jina la Temitope, likiwa na maana ‘Ulichonipa
Mungu lazima kishukuriwe’.
Jina analojulikana sana sasa ni T. B. Joshua.
TB Joshua ni muhubiri mwanzilishi na kiongozi wa The Synagogue, Church
of All Nations (SCOAN), hii ni taasisi ya kidini inayoendesha Emmanuel
TV, Tv ambayo huonekana kote duniani ikiwa inarushwa kutoka Lagos
Nigeria. TB Joshua anasemeka ni moja ya watu 50 wenye ushawishi zaidi
Afrika, anajulikana sana kwenye mitandao ya Facebook ambako anawafuasi
zaidi ya milioni moja laki tano, na video zake nyingi zilizomo kwenye
Youtube. Kwa mujibu wa Forbes, mwaka 2011 TB Joshua alikuwa mtu wa tatu
kwa utajiri nchini Nigeria.
Wakati akiwa shule alijulikana kwa jina la Balogun Francis, alisoma
shule ya St. Stephen’s Anglican Primary School ya Arigidi-Akoko, kati ya
mwaka 1971 na 1977, lakini hakumaliza sekondari. Wakati yuko shule
alijulikana kama “small pastor” kutokana na kupenda sana biblia, baada
ya kuacha shule alifanya kazi mbalimbali ndogo ndogo, hatimae akaanzisha
darasa la biblia kwa watoto, wakati huohuo akaanza kujiendeleza kwa
masomo ya jioni. Hatimae akaamua kwenda kujiunga na jeshi la Nigeria,
lakini kwa bahati mbaya akaachelewa treni kwenda kwenye usaili na hivyo
ndoto hiyo ikaishia hapo.
Kwa maelezo yake mwenyewe anaeleza jinsi alivyokabithiwa upako wake, “
Nilikuwa katika hali ya kuzimia kwa siku tatu mfululizo, nikaona mkono
ukielekeza Biblia kwenye moyo wangu, na Biblia ikaingia kwenye moyo
wangu na moyo wangu wa zamani ukachanganyika na Biblia. Ufahamu
uliponijia nikawaona Mitume na Manabii wa zamani wako na mtu ambaye
sikuweza kuona kichwa chake kwa sababu alikuwa mrefu sana amefika mpaka
mbinguni. Nikaamini kuwa alikuwa ndie Bwana wetu Yesu Kristo, nami
nikajiona nimo katika hawa Manabii na Mitume wa zamani.
Nikauona mkono wa yule mtu mrefu sikuweza kuona uso wake maana ulikuwa
na mwanga mkali sana sikuweza kabisa kuangalia uso wake. Lakini Mitume
wengine niliweza kuwaona. Mitume Peter na Paul, Manabii Moses, Eliya na
wengine, kwani majina yao yalikuwa yameandikwa kwa herufi kubwa vifuani
mwao. Nikasikia sauti inasema, “Mimi ni Mungu wako, nakupa upako nenda
kafanye kazi ya baba yako wa mbinguni.”
Wakati huohuo yule mtu mrefu akanipa Msalaba na Biblia iliyokuwa kubwa
kuliko ile iliyoingia moyoni mwangu. Akaniahidi kuwa kila nitakapo tumia
muda wake na jina lake nitapata Msalaba mkubwa zaidi, nikienda kinyume
na mambo yatakuwa kinyume. Nikasikia sauti ya yule mtu mrefu ambaye
sikuwa naweza kuona kichwa chake ikasema,’ Mimi ndie Bwana wako,
niliyekuwa na ambaye ndie, mimi ni Yesu Kristo ninaetoa amri kwa mitume
na manabii wote. Sauti ile ikasema tena ‘Nitakuonyesha mambo mazuri ya
ajabu na nitajionyesha kupitia mafunzo, mahubiri, miujiza, ishara, kwa
ajili ya kuokoa roho za watu. Kutoka wakati huo nimekuwa napata maono
kila mwaka na Msalaba mkubwa zaidi ukiwa na maana majukumu makubwa
zaidi”
SCOAN ina tawi moja tu nalo liko Ghana, kwa sasa kila Jumapili kuna
ibada Nigeria ambayo huhudhuriwa na kiasi cha watu 15,000 kila Jumapili.
Uponyaji ni kati ya mambo mengi yanayofanywa katika kanisa la TB Joshua
watu wengi wamekuwa wakisema wamepona maradhi mbalimbali kutokana na
kufika kanisani hapo na kwa kutumia maji, ‘annointed water’ ambayo
hutolewa na TB Joshua.
Wakati wa tatizo la Ebola TB Joshua alisema maji hayo yanaweza kutibu
ugonjwa huo na alituma chupa 4,000 za maji hayo zikiambatana na dola
50,000 kwenye serikali ya Sierra Leon. Hili lilikuja hasa baada ya
maafisa afya wa Lagos walipomtembelea TB Joshua kumtaka asiwaruhusu
wagonjwa Ebola kuja katika kanisa hilo kwa kuondoa uwezekanao wa kupata
mlipuko wa ugonjwa huo katika jiji hilo. Wasanii wa Nollywood kama Jimmy
Iyke na Camilla Mberekpe pia ni kati ya watu wengi waliowahi kupata
huduma za kuondoa mapepo katika miili yao katika kanisa hilo.
Pia TB Joshua anasemekana ameweza kutabiri mambo mengi ikiwemo kifo cha
Michael Jackson, milipuko ya Boston na hata matokeo ya mechi mbili za
fainali za AFCON, ambapo moja mshindi alikuwa Zambia na nyingine Nigeria
ilichukua ushindi. Amesha wahi kutabiri kuhusu kifo cha Rais mmoja wa
Afrika na inasemekana Bingu Mutharika wa Malawi ndie aliyetabiriwa
wakati huo. Pia anasemekana kutabiri kuhusu ndege ya Malaysian Airline
iliyopotea baharini, miezi kadhaa kabla ya tukio hilo.
No comments:
Post a Comment