Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, December 14, 2015

Profesa Muhongo aiagiza Tanesco kuandaa mpango madhubuti wa utiririshaji maji

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akimsikiliza Mhandisi John Skauk (kulia)wakati wa ziara yake kwenye kituo cha kuzalisha umeme cha Hale. Kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), Felchesmi Mramba. Lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kujionea shughuli za uzalishaji umeme zinazoendelea kwenye mabwawa ya Hale, New Pangani Falls na Nyumba ya Mungu.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (katikati) akizungumza wakati wa ziara yake kwenye kituo cha kuzalisha umeme cha Nyumba ya Mungu kilichopo Mkoani Kilimanjaro. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga na kushoto ni Mtaalamu kutoka Bodi ya Maji- Bonde la Pangani.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akielezea jambo wakati wa ziara yake ya kukagua vituo vya kuzalisha umeme kwa kutumia maji. Kulia ni Meneja wa Vituo vya kuzalisha umeme vya Hale, New Pangani na Nyumba ya Mungu ambavyo kwa pamoja vinajulikana kama Pangani Hydro systems, Mhandisi John Skauk.

 
Bwawa la kuzalishia umeme lijulikanalo kama New Pangani Falls.

Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) limetakiwa kuandaa mpango madhubuti wa utitirishaji maji kutoka kwenye bwawa la Nyumba ya Mungu ili kuwepo na maji ya kutosha kuzalisha umeme kwenye vituo vya Hale na New Pangani.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alitoa agizo hilo wakati  wa ziara yake katika mabwawa ya kuzalishia umeme ya Hale na Pangani yaliyoko mkoani  Tanga na bwawa la Nyumba ya Mungu la mkoani Kilimanjaro.

Agizo hilo alilitoa baada ya kujionea namna ambavyo kina cha maji kwenye mabwawa ya Hale na Pangani kimepungua kutokana na mipango hafifu ya utiririshaji maji kutoka bwawa la Nyumba ya Mungu ambalo ni chanzo  kikuu cha upelekaji maji katika mabwawa hayo yaliyoko mkoani Tanga.

Profesa Muhongo alisema wananchi wanatarajia umeme usiokatikakatika, umeme wa kutosha na wa bei nafuu.

“Nimeamua kufanya ziara katika vyanzo vyote vya uzalishaji umeme nchini ili baada ya hapa tuangalie jinsi tutakavyoboresha hali ya uzalishaji umeme na wananchi wetu wapate umeme wa uhakika na wa bei nafuu,” alisema Profesa Muhongo.

Meneja wa Kituo cha kuzalisha umeme wa maji wa Pangani, Mhandisi John Skauk alisema kuwa mitambo ya Hale ilifungwa mwaka 1964 ikiwa na uwezo wa kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 21 ambapo kila mtambo (kati ya mitambo miwili) katika kituo hicho una uwezo kuzalisha umeme wa kiasi cha megawati 10.5.

Aliongeza kuwa  ukarabati wa kwanza wa mitambo hiyo ulifanyika mwaka 1986 na kuwa ilipofika mwaka 2008 mtambo mmoja uliharibika na hivyo kusababisha mtambo mmoja tu kufanya kazi hadi sasa.

Akionekana kukasirishwa na taarifa hiyo,  Profesa Muhongo alihoji ni kwanini ukarabati wa mtambo huo umechukua muda mrefu  na na kuagiza mtambo huo kufungwa haraka ili uweze kuzalisha nishati ya umeme.

Profesa Muhongo pia alisisitiza kufanyika kwa ukarabati wa mara kwa mara wa mitambo ya uzalishaji umeme huku akielezea kuwa kuchelewa kwa ukarabati wa mitambo hiyo ni sababu mojawapo ya matatizo ya umeme nchini.

Kwa upande wa kituo cha uzalishaji umeme cha New Pangani ilielezwa kuwa mitambo iliyopo ina uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati 68 hata hivyo kutokana na upungufu wa maji kwenye bwawa la Pangani mitambo hiyo inazalisha megawati 17 hadi 50 kwa siku.

"Mitambo hii ya Pangani iko vizuri haina hitilafu yoyote isipokuwa tu ni suala la kutopata maji ya kutosha kutoka kwenye chanzo kikuu ambacho ni Nyumba ya Mungu," alisema Mhandisi Skauk.

Aidha, akizungumzia Kituo cha Nyumba ya Mungu, Mhandisi Skauk alieleza kuwa kituo kinao uwezo wa kuzalisha jumla ya Megawati nane hata hivyo kiasi hicho hakijafikiwa kutokana na utiririshaji mdogo wa maji hivyo kwa sasa kinazalisha Megawati 3.7.

“Tunashindwa kutiririsha maji ya kutosha kwa sababu tukifanya hivyo tutasababisha mafuriko kwenye baadhi ya maeneo ambapo maji hayo yanapita,” alisema.

Akizungumzia kwa ujumla suala la uzalishaji umeme kwa kutumia maji, Profesa Muhongo alisema kuwa changamoto ya uzalishaji umeme wa maji nchini inatokana pia na mabwawa mengi kujengwa kwa kutumia teknolojia ya zamani hivyo Serikali imedhamimiria kuwa na vyanzo vingi zaidi vya kuzalisha nishati hiyo ya umeme mbali na maji.

"Lazima tuwe na vyanzo vingi, umeme upatikane, usikatikekatike. Tunafanya tathmini ya vyanzo vyote tuone uzalishaji wake, ziara hii ni muhimu kwani bila kufanya hivi nisingejionea kwamba kuna mtambo haufanyi kazi tangu mwaka 2008,” alisema Muhongo.

Alisema alichokiona Kanda ya Kaskazini ni kuwa maji yapo ya kutosha isipokuwa hakuna mipango madhubuti ya kutiririsha maji kutoka kwenye chanzo kikuu hadi kufika kwenye mabwawa ya uzalishaji umeme ya Hale na Pangani.

"Habari ya kuwa mnawaambia wananchi kwamba huku hakuna maji sio sahihi. Maji yapo isipokuwa hakuna mipango mizuri ya mtiririko wa maji kutoka Nyumba ya Mungu kwenda Hale na Pangani," alisema.

Alisema vyanzo vya umeme wa maji nchini vinapaswa kuzalisha Megawati 561 lakini umeme unaozalishwa kwa njia hiyo kwa sasa si zaidi ya Megawati 110 ambayo ni sawa na asilimia 20.

"Hili suala la maji linatia aibu; tunataka tutathmini ndani ya siku kumi tubaini wapi tuongeze nguvu zaidi, Tanesco inapaswa iingie gharama ya kutengeneza miundombinu ya maji," alisema Profesa Muhongo.

Aliliagiza Shirika hilo la Umeme kufanya kikao na Bodi ya Bonde la Pangani ili kuandaa mpangilio mzuri wa kuruhusu maji kutoka bwawa la Nyumba ya Mungu hadi Hale na Pangani bila kuleta uharibifu kwa kuwa wananchi pia wanahitaji maji hayo kwa matumizi mbalimbali.

Aliagiza kikao hicho kifanyike tarehe 15 mwezi huu (Jumanne) asubuhi na makubaliano ya kikao yapelekwe Wizara ya Nishati na Madini na wakuu wa wilaya wa maeneo husika ili hatua zichukuliwe haraka.

No comments:

Post a Comment