Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Monday, December 14, 2015

WAZIRI WA KWANZA KUTIMULIWA NA RAIS MAGUFULI HUYU HAPA

Rais John Magufuli alionya Mawaziri aliowataja juzi kuwa tayari kufanya sherehe ya kufukuzwa, kama pia wataandaa sherehe za kuteuliwa kushika nyadhifa hizo katika Baraza la kwanza la serikali yake ya awamu ya tano.
Katika kauli yake hiyo mbele ya waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema anataraji Mawaziri aliowachagua wawe wachapa kazi, wenye lengo la kuleta maendeleo nchini kwa kasi.
Akitangaza Baraza lake hilo ikiwa ni siku ya 35 tangu aapishwe kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Rais Magufuli alisema:
“Na kwa hakika, wasihangaike kufanya sherehe. Wamepata kazi ngumu, wakafanye kazi, lakini kama wapo ambao wanaopenda kufanya sherehe, pia wajiandae kufanya sherehe siku wakifukuzwa.
“’Contract’ (mkataba) yetu ni miaka mitano, tukawafanyie Watanzania yale tuliyoyaahidi, bila kubagua rangi, dini, itikadi, ukanda, makabila, ndiyo maana siku zote nimekuwa nikisema Hapa ni Kazi Tu.”


Lakini si lazima Waziri adumu kwa miaka mitano ya mkataba baina ya serikali na wananchi huo, Rais Magufuli aliashiria.

Ni kipi hasa kinaweza kumfanya Waziri wa Serikali ya Magufuli awe wa kwanza kwenda na maji?

Kupoteza uadilifu, uzalendo, uzembe na kutokuwa tayari kupokea maagizo na kuyatekeleza kwa wakati, uchuguzi wa Nipashe umebaini.

Akizungumza na gazeti hili jana, Mwalimu wa Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Bashiru Ally, alisema Baraza la Mawaziri limekidhi kwa kiasi kiu ya Watanzania, japo hajakamilisha kwa kujaza wizara ambazo zipo wazi.

Alisema katika watu aliowateua anaamini alitumia muda mwingi kuangalia watu wanaoweza kufanya kazi kwa maelekezo ya katiba ya nchi, inayoweka wazi kuwa kiongozi lazima awe muadilifu, mchapakazi na elimu ya kutosha.

“Bahati mbaya Rais hana mshirika katika kumchagua mtu, habanwi na sheria wala katiba lakini naamini mawaziri aliowateua alizingatia mambo muhimu,” alisema Bashiru.

Alifafanunua kuwa mawaziri hao wakitaka kwenda na kasi ya kiongozi huyo wanatakiwa kuwa wazalendo na wawajibikaji kwa kuifanya kazi ya umma kwa juhudi na na maarifa ya ziada.

Kwa upande wake, Dk. Mohamed Bakari wa UDSM pia alisema anachoona katika safari ya mawaziri hao itakuwa ngumu kutimiza wajibu wao na linaweza kubadilishwa endapo hakutatokea mabadiliko ya haraka katika kasi ya kutumbua majipu kama anavyotaka Rais.

Aidha, Dk. Bakari alimsifu Rais kwa kuangalia ushirikishwaji wa kila eneo la nchi na usawa wa kijinsia.

Alifafanua kuwa katika vigezo hivyo aligusa kila eneo la nchi kwa kumteua Waziri au Naibu kwa ajili kufanya serikali iwe shirikishi.

Wakati huo huo, Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), umelitahadharisha Baraza la Mawaziri lililoteuliwa juzi lisiwe mizigo kwa Rais John Magufuli.
Pia umewataka mawaziri kuhakikisha mchakato wa kuundwa Baraza la Taifa la Vijana unakamilika ili kuwawezesha kushiriki katika shughuli za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Idara ya Uhamasishaji, Sera, Utafiti na Mawasiliano ya UVCCM, Egla Mwamoto, alisema ingawa baraza hilo ni dogo wanatarajia wafanye kazi kwa nguvu na bidii zaidi.
Alisema mawaziri wengi ni vijana na UVCCM inaamini kwamba iwapo watajituma kikamilifu wanaweza kuleta maendeleo na kubadilisha mfumo wa nchi.

Aidha, aliwataka mawaziri hao wasimamie kutenga maeneo ya uzalishaji mali, kuviwezesha vikundi vya kukopa na kuweka vya vijana (Saccos), kuweka vituo maalumu vya vijana kila wilaya, pamoja na kuhakikisha kuwa wananufaika na Shilingi milioni 50 zitakazotolewa na serikali kwa kila kijiji.

“Sisi wadau wa vijana tunawataka mawaziri walioteuliwa wamsaidie Rais Magufuli kutatua changamoto zinazozikabili sekta mbalimbali ikiwamo ya vijana hasa katika suala la ajira na tunawakumbusha watekeleze ilani ya CCM, kwa kasi ambayo ameanza nayo Rais katika maeneo mbalimbali,” alisema Mwamoto.

Alisema mawaziri lazima wamuunge mkono Rais katika kuzuia matumizi yasiyo ya lazima ili fedha hizo zielekezwe kwenye maboresho ya huduma za kijamii zinazosuasua.

“Tatizo kubwa ni rushwa na ubadhirifu wa mali za umma, tunaamini kazi ya kudhibiti kundi hilo italeta mafanikio kutokana na jitihada zilizoelekezwa huko. Wananchi tushirikiane na viongozi wetu kuleta maendeleo ya taifa,” alisema.

WALIOTEULIWA

Mawaziri Ofisi ya Nchi Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora, George Simbachawene na Angela Kairuki, Naibu ni Jafo Suleiman; Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Waziri ni Januari Makamba, Naibu ni Luhaga Mpina.
Waziri wa Ofisi ya Nchi, Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, ni Jennista Mhagama, Naibu Mawaziri ni Profesa Possi Abdallah na Anthony Mavunde; Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Mwigulu Nchemba, Naibu ni William Tate Ole Nashe.

Wizara ya Katiba na Sheria, Waziri ni Dk. Harrison Mwakyembe; Dk. Augustine Mahiga, Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Naibu ni Dk. Susan Kolimba; Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Waziri ni Dk. Hussein Mwinyi; Wizara ya Nishati na Madini, Waziri ni Profesa Sospeter Muhongo na Naibu ni Medard Kalemani.

Wizara ya Mambo ya Ndani, Waziri ni Charles Kitwanga; Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Naibu Angelina Mabula; Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Waziri ni Charles Mwijage; Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri ni Ummy Mwalimu, Naibu Dk. Hamis Kigwangala.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Waziri ni Nape Nnauye, Naibu ni Anastazia Wambura; Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Waziri ni Profesa Makame Mbarawa, Naibu Mhandisi Isaack Kamwela. 

WIZARA ZILIZOKOSA MAWAZIRI
Katika uteuzi huo Wizara nne zimekosa mawaziri ambao alisema atawateua siku zijazo na kuteua manaibu pekee.

Wizara hizo ni Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi, Mawasiliano (haina Waziri), Naibu ni Injinia Edwin Ngonyani; Fedha na Mipango (haina Waziri), Naibu ni Dk. Ashaji Kijachi.

Nyingine ni Wizara ya Maliasili na Utalii (Haina Waziri), Naibu ni Mhandisi Lamo Makani; Wizara ya Elimu, Teknolojia na Ufundi (haina Waziri), Naibu ni Mhandisi Stellah Manyanya.

KUVUJA JASHO
Tofauti na miaka ya hivi karibuni ambapo nafasi za juu za uongozi zikiwamo za uwaziri zilikuwa zikichukuliwa kuwa ni ‘ulaji’ kiasi kwamba watu walikuwa wakipongezana, inaonekana wazi kuwa mawaziri wa Rais Magufuli watakuwa tofauti. 

Mianya mingi iliyokuwa ikitajwa kuwapatia mawaziri mamilioni ya fedha inaelekea kuzibwa kutokana na amri kadhaa alizotangaza tangu aapishwe kuwa Rais, lengo likiwa ni kubana matumizi na kuwezesha fedha zinazopatikana zitumike kumaliza kero mbalimbali zinazowakabili Watanzania.

Baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakitajwa kuwaingizia fedha nyingi mawaziri, lakini sasa yameondoshwa na hivyo kubana matumizi holela ya serikali ni pamoja na hafla za kupongezana, safari za nje; posho za semina elekezi, kuchapisha kadi za Krismasi, Mwaka Mpya, Iddi na sikukuu nyingine, manunuzi ya bidhaa mbalimbali yenye fedha za ziada maarufu kama ‘cha juu’, posho za vikao vya kikazi mikoani, manunuzi ya kila mara ya samani za ofisi zilizokuwa zikitoka ughaibuni na pia posho za vikao vya kamati za Bunge.

Rais alisema serikali yake imechelewa kuteua Baraza la Mawaziri kwa muda wa mwezi mmoja kwa ajili ya kuokoa fedha za mishahara na marupurupu ya Mawaziri na Manaibu ambazo zingetumika kwenye shughuli nyingine za maendeleo ya taifa.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment