Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, January 15, 2016

UZINDUZI WA STIKA MAALUM YENYE UJUMBE WA KUTOKOMEZA MAUAJI YA ALBINO

????????????????????????????????????
Na Nyakongo Manyama-MAELEZO
TAASISI ya  watu wenye ulemavu wa ngozi mkoa wa Dar es salaam inatarajia kufanya uzinduzi wa  ‘stika’ maalum yenye ujumbe wa kutokomeza mauaji ya watu wenye albinism utakaofanyika januari 26 mwaka huu.Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa taasisi hiyo Bw. Michael Lugendo amesema kuwa uzinduzi huo utafanyika katika kituo cha polisi kati jijini Dar es Salaam kuanzia saa tano asubuhi.
Bw. Michael Lugendo amesema kuwa stika hiyo ina lengo la kuhamasisha jamii kuungana na Rais Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli na Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam ili kuyafanya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yatokomezwe na yabaki kuwa historia.
Kwa upande mwingine Bw. Lugendo ameongeza kuwa kulingana na kasi ya mabadiliko tabia nchi, jamii isipochukua hatua za makusudi kuna uwezekano wa watu wenye ulemavu wa ngozi kuangamizwa na saratani ya ngozi.


Alisema watu wenye ulemavu wa ngozi wanaishi katika mazingira ya umaskini kiasi kwamba waliowengi hawana uwezo wa kupata fedha ya kununua mafuta ya kuzuia mionzi ya jua  ambayo husababisha saratani ya ngozi.“Sisi watu wenye ulemavu wa ngozi ni wahanga wakubwa sana na jamii isipochukua hatua za makusudi upo uwezekano wa kuangamizwa na saratani ya ngozi ukizingatia kwamba tunaishi katika mazingira ya umaskini na walio wengi hatuna uwezo wa kupata fedha ya kununua mafuta” alisema Bw. Lugendo.
Aidha Bw. Lugendo amesema kuwa  taasisi hiyo imemteua Bw. Mbwana Ally Samata kuwa balozi wa kudumu wa kusemea watu wenye ulemavu wa ngozi.
Alibainisha kuwa majukumu ya Nahodha huyo wa Timu ya Taifa ya Tanzania kwa ujumla ni kuhamasisha dunia kwa njia ya soka kuhakikisha  kwamba hakuna mlemavu wa ngozi anayefariki kwa kifo cha saratani ya ngozi au mauaji ya kukatwa viungo yanayotokana na Imani za kishirikina.

Bw. Lugendo aliwataka wadau mbalimbali, kampuni, balozi mbalimbali, Mashirika yasiyokuwa ya Serikali kujitokeza ili kuwezesha kutimiza lengo hilo kwa kutoa taarifa za uhalifu dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi kupitia vyombo vya habari pamoja na jeshi la polisi.

No comments:

Post a Comment