Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Saturday, February 20, 2016

BENKI YA POSTA TANZANIA YAJENGA VYOO VYENYE THAMANI YA SH. MILIONI 4.7 KATIKA SHULE YA MSINGI MAKAMBI ILIYOPO MANISPAA YA SONGEA MKOANI RUVUMA


 Wanafunzi wa shule ya msingi ya Makambi iliyopo Kata ya Ndilima Litembo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma wakifurahia vyoo vya kisasa vilivyojengwa na Benki ya Posta Tanzania.
 Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na Mawasiliano wa Benki ya Posta, Noves Moses akiongea kwenye mkutano katika shule hiyo muda mfupi kabla ya kuzindua vyoo hivyo. 
 Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na Mawasiliano wa Benki ya Posta, Noves Moses akikata utepe ikiwa ni ishara ya 

 
kuzindua vyoo vyenye matundu 14, vitakavyohudumia wanafunzi 850 katika shule ya Msingi ya Makambi, Songea Mkoa wa Ruvuma, ujenzi huo umegharimu shilingi milioni 4.7 kulia ni Meneja wa Oparesheni wa tawi la Songea, Simon Mlelwa.
Meneja Mwandamizi wa Mahusiano na Mawasiliano wa Benki ya Posta, Noves Moses akiwa kwenye picha ya pamoja na walimu wa shule hiyo pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali ya mtaa.

Na Mwandishi Wetu

MENEJA mahusiano na mawasiliano wa Benki Posta Tanzania, Noves Moses amelitaka suala la elimu bure liendane na mazingira mazuri ya kimiundo mbinu kwa wanafunzi pamoja na walimu wao ili kuifanya elimu hiyo kuwa bora zaidi.

Rai hiyo aliitoa jana wakati akizindua vyoo vya kisasa vya Shule ya Msingi ya Makambi iliyopo Kata ya Ndilima Litembo Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, ambavyo vimejengwa na Benki hiyo kwa thamani ya shilingi Milioni 4.7 ikiwa ni sehemu ya mchango kwa jamii katika kuboresha mazingira ya elimu.

Akizindua matumizi ya vyoo hivyo vyenye matundu 14, Noves alisema kuwa jamii na taasisi mbalimbali zinatakiwa zitambue kuwa suala la elimu bure linatakiwa liendane na uboreshwaji wa mazingira ya wanafunzi na walimu wawapo shuleni hapo.

Alisema kuwa kumekuwepo na baadhi ya wadau wa elimu kulichukulia suala la elimu bure kama kigezo cha kutokuchangia sekta hiyo na baadala yake wanadai ni kazi ya serikali pekee jambo ambalo siyo sahihi katika uboreshaji elimu.

“Suala la elimu bure lisiwe kigezo cha wadau kushindwa kuichangia sekta hiyo kwani kufanya hivyo kunapelekea baadhi ya shule kushindwa kuwa na mazingira mazuri ya watoto kujisomea pamoja na walimu wao kutokuwa na morali ya kufundisha” alisema Meneja mahusiano .

Noves alisema kuwa Benki ya Posta Tanzania inafanya kazi kwa kiwango kikubwa na serikali hivyo imetoa misaada mbalimbali ya kijamii hasa kwa upande wa afya na elimu huku katika upande wa elimu wamechangia madawati na ujenzi wa vyoo bora vya kisasa kwenye shule mbalimbali hapa nchini .

Kwa upande wake Mwalimu Mkuu msaidizi wa shule hiyo, Kanisius Ngongi awali akitoa taarifa ya shule hiyo kabla ya kukabidhiwa vyoo hivyo alisema kuwa shule hiyo ina wanafunzi 850 na matundu ya vyoo yapo 14 na kuwa vyoo vyote vina maji ya kutosha.

Ngongi aliipongeza benki hiyo alisema kuwa shule hiyo kwa sasa imeshabadilika, mazingira yamekuwa bora kwa upande wa vyoo vya wanafunzi ambavyo kwa sasa hakuna shule ndani ya Manispaa hiyo yenye vyoo kama hivyo.


Mwalimu Ngongi alisema kuwa licha ya vyoo vya wanafunzi kuwa bora lakini bado kuna changamoto ya vyoo vya walimu maana vyoo walivyokuwa wakivitumia vimeshapoteza ubora wake na kuwafanya walimu hao kupata shida mahala pa kujisitili hivyo amewaomba wadau mbalimbali waweze kuchangia kama Benki ya Posta inavyojitolea.

(Imeandaliwa na mtandao wa www. habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)

No comments:

Post a Comment