Dar
es Salaam. Baadhi ya wanafunzi walioshika nafasi 10 za juu katika
matokeo ya kidato cha nne yaliyotangazwa jana na Baraza la Mitihani
Tanzania (Necta), wameelezea ndoto zao, huku wazazi na walimu
wakibainisha siri za mafanikio yao, huku shule za binafsi zikishika kumi
bora.
Wakizungumza na waandishi wetu jana, wanafunzi
hao walisema kumtanguliza Mungu, kusoma kwa bidii na nidhamu ndivyo
vilivyowawezesha kupiga hatua hiyo.
Aliyeshika nafasi ya kwanza
Mwanafunzi
wa Shule ya Sekondari Canossa, Butogwa Shija (17) aliyeshika namba moja
kitaifa amesema kilichomsaidia kufaulu vizuri ni kufanya marudio,
kumwomba Mungu na kujiwekea lengo la kwenda kusoma Chuo Kikuu cha
Harvard nchini Marekani.
Alisema alianza kujiandaa kwa
safari hiyo ya kwenda Harvard tangu akiwa kidato cha kwanza ambako
amekuwa akiongoza hadi alipomaliza.
“Nilipopigiwa simu nilikuwa nasuka hivyo nilipoambiwa nimeongoza, nikaona safari yangu ya Harvard imeanza,” alisema Butogwa.
Alisema
alipokuwa kidato cha tatu, alimuomba baba yake amuandalie hati ya
kusafiria kwa sababu anajua atafanya vizuri katika mitihani yake.
“Wazazi wangu hawawezi kunipeleka Harvard lakini kwa juhudi zangu nitakwenda. Mimi ubongo wangu ni kama memory card,” alisema.Chanzo Mwanainchi
Mama
mzazi wa Butogwa, Angela Shija alielezea furaha ya kufaulu kwa binti
yake na kusema mara baada ya matokeo hayo yaliyotangazwa akiwa ofisini,
alianza kupigiwa simu nyingi jambo lililomlazimu kuacha shughuli zake na
kurudi nyumbani.
“Tangu akiwa kidato cha kwanza alishaniambia kuwa atafanya vizuri na sisi tumekuwa tukimsisitiza asome,” alisema.
Angela
alisema binti yake huyo amekuwa na tabia ya kujisomea kila wakati
akisema kila alipokuwa nyumbani wakati wa likizo, alikuwa akijisomea
hata pale alipokuwa kwenye gari katika safari yoyote.
Aliyeshika nafasi ya pili
Aliyeshika
nafasi ya pili kitaifa Congcong Wang (16) kutoka Shule ya Sekondari ya
Wasichana ya Feza alisema alijiunga na shule hiyo mwaka 2006 akitokea
China na kulazimika kujifunza lugha tatu; Kiswahili, Kiingereza na
Kituruki ambazo hutumika katika shule hiyo ili aweze kuwasiliana na
wenzake vizuri.
Alisema baada ya kujua lugha hizo, ilikuwa rahisi kwake kuelewana na wenzake na walimu walimsaidia.
“Walinisaidia
wakijua baadhi ya vitu sitaelewa. Cha muhimu ni kwamba hakuna njia ya
mkato zaidi ya kusoma,” alisema Congconge, ambaye ni raia wa China
aliyepata alama B somo la Kiswahili.
Aliyeshika nafasi ya tatu
Mwanafunzi
aliyeshika nafasi ya tatu, Innocent Lawrence (20) wa Shule ya Sekondari
ya Wavulana ya Feza alisema kusoma, nidhamu na kumtegemea Mungu ndiko
kulikomfikisha hapo.
“Nilikuwa nafuatilia ratiba ya
kusoma niliyokuwa napanga. Wanafunzi wengi huwa wanapanga ratiba lakini
hawazifuati,” alisema Innocent.
Baba mzazi wa Innocent,
Lawrence Nyakabunda alisema walitarajia matokeo hayo kwa kuwa ndiye
aliyeongoza pia katika matokeo ya kitaifa ya darasa la saba.
“Matokeo
hayo yametufurahisha, nidhamu, kumtegemea Mungu na kuheshimu malengo
aliyojiwekea ndiko kumemsaidia,” alisema Nyakabunda.
Aliyeshika nafasi ya tano
Mwanafunzi
wa Shule ya Sekondari Ilboru, Sang’udi Emmanuel aliyeshika nafasi ya
tano kitaifa alisema hakutarajia mafanikio hayo na kusema siri ya
ushindi ni kusoma kwa bidii, nidhamu na kumwamini Mungu.
Sang’udi
ambaye alishika nafasi ya kwanza kitaifa katika mtihani wa majaribio wa
kidato cha nne mwaka jana, alisema anawashukuru walimu, wanafunzi na
wazazi wake kwa malezi mazuri.
“Nimefurahi sana,
kushika nafasi ya tatu kitaifa na siri ya ushindi ni Mungu, nidhamu na
kushirikiana na wenzangu darasani,” alisema.
Alisema malengo yake ni kuwa mhandisi wa ndege baada ya kumaliza masomo yake.
Mwalimu
Mkuu wa Sekondari ya Ilboru, Julius Shulla alisema alitegemea kuwa
Sang’udi angeshika nafasi za juu, kwani tangu kidato cha kwanza hadi cha
nne amekuwa akifanya vizuri na mwenye nidhamu darasani.
“Ni
kijana mzuri, ana nidhamu na amekuwa akiongoza katika soko la hesabu,
mwaka jana aliongoza kitaifa na darasani amekuwa akishika nafasi za juu
sambamba na mwenzake David Joseph aliyeshika nafasi ya nane kitaifa,”
alisema.
Mlezi wa mwanafunzi huyo, Veronica Sang’udi
alisema amekuwa na nidhamu na amefuata nyendo za dada yake, Getrude
Mande ambaye mwaka 2014 alikuwa mmoja wa wasichana waliofanya vizuri.
Aliyeshika nafasi ya tisa
Mwanafunzi
aliyeshika nafasi ya tisa kitaifa, Bright Mwang’onda (17) alisema
ufaulu huo utamuwezesha kuifikia ndoto yake ya kuwa mhandisi wa ndege.
Bright
aliyehitimu katika Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Marian alisema
tabia njema, bidii katika masomo na kumuomba Mungu vimekuwa ngao ya
ufaulu wake.
“Nakumbuka niliwahi kuwa wa mwisho wakati
nikiwa chekechea, cha ajabu wazazi wangu na walimu hawakunichukia badala
yake walinitia moyo wakiniambia nikikazane kusoma nitafaulu. Namshukuru
Mungu, tangu darasa la tatu hadi leo, maendeleo yangu ya shule yamekuwa
mazuri,” alisema.
Mama yake mzazi, Hamida Kejo alisema haikuwa rahisi kupokea matokeo ya mwanaye na kwamba, ufaulu wake umeifurahisha familia yao.
“Nilikuwa
kwenye kazi za bustani nilipopigiwa simu na kaka yangu (Rashid Kejo,
Mhariri Msanifu Mkuu wa Mwananchi), akinipa hongera ya mtoto kufaulu,
baadaye nikaambiwa ameingia 10 bora hakika imekuwa furaha na
tunamshukuru Mungu,” alisema.
Aliwashauri wanafunzi wengine kusoma kwa bidii, kuwapenda walimu wao na kuepuka makundi mabaya yanayoweza kuwapotezea ndoto zao.
Imeandikwa na Kalunde Jamal, Tumaini Msowoya na Mussa Juma.
No comments:
Post a Comment