Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, February 12, 2016

SERIKALI YAWASIMAMISHA KAZI WATENDAJI WAKALA WA VIPIMO TANZANIA



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitaka maelezo kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo na Mizani, Bibi Magdalena Chuwa (kulia) kuhusu sababu zilizomfanya azuie matumizi ya flow Meter katika kuhakiki kiwango cha mafuta yanayoingia nchini kupitia bandari ya Dar es salaam wakati alipofanya ziara kwenye badari hiyo Februari11, 2016.

SERIKALI imeamua kuwasimamisha kazi watendaji wawili kutoka Wakala wa Vipimo nchini (WMA) kuanzia leo ili kupisha uchunguzi wa upotevu wa mafuta bandarini kutokana na zuio la kufunga kwa mita kwa zaidi ya miaka mitano.

Waliosimamishwa kazi ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo nchini (WMA), Bi. Magdalena Chuwa na Meneja Vipimo Kitengo cha Bandari, Bi. Bernadina Mwijarubi. Bi. Mwijarubi ndiye anashughulikia kitengo cha mafuta bandarini.


Akitangaza uamuzi huo kwenye kikao cha Makatibu Wakuu kilichofanyika leo (Ijumaa, Februari 12, 2016) ofisini kwake Magogoni jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemwagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Adelhelm Meru awaandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi huo.

“Katibu Mkuu Viwanda, waandikie barua za kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi. Katika kipindi hiki hawatatakiwa kusafiri kwenda popote hadi uchunguzi utakapokamilika. Pia utafute mtu wa kukaimu nafasi hiyo ili kazi ziendelee,” alisema.

Waziri Mkuu pia amesema ofisi yake itawaandikia barua ofisi ya TAKUKURU na polisi ili wafuatilie suala hilo mara moja na ikithibitika kuwa walihusika hatua rasmi zitachukuliwa na itathibitika hawakuhusika basi watarudishwa.Waziri Mkuu pia aliagiza mfumo wa upimaji mafuta kwa kutumia flow meters uendelee kutumika na ule upimaji wa kukadiria uache kutumiwa mara moja.

Jana (Alhamisi, Februari 11, 2016) Waziri Mkuu alifanya ziara kukagua flow meters za zamani zilizopo Kurasini (Kurasini Oil Jetty) na kisha akatembelea na kukagua flow meters mpya ambazo zinajengwa Kigamboni. Mita hizo zimegharimu dola za marekani milioni 6 (sawa na sh. bilioni 12.96/- za sasa).

Pia Waziri Mkuu alitembelea sehemu ya kuchukulia mafuta yanayotoka bandarini (TPA Manfold) iliyoko Kigamboni na kukagua mitambo ya kusambazia mafuta kwenye matenki ya mafuta ya kampuni ya TIPER yaliyoko Kigamboni yanayomilikiwa kwa ubia baina ya Serikali na kampuni ya Oryx Energies.

Katika ziara hiyo ilibainika kuwa Kampuni ya TIPER imejiunganishia bomba la moja kwa moja kutoka kwenye bomba kubwa la mafuta linalotoka bandarini hali iliyomlazimu Waziri Mkuu kuagiza kwamba bomba hilo litolewe kwenye maungio hayo ndani ya mwezi mmoja.

“Jana niliagiza kuwa bomba hilo ling’olewe. Nimetoa mwezi mmoja ili kurekebisha mfumo huo. Simamieni vizuri na kuhakikisha kuwa na wao pia wanarudi kwenye manfold kama ilivyo kwa wengine,” alisema Waziri Mkuu.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S. L. P. 3021,
11410 DAR ES SALAAM.
IJUMAA, FEBRUARI 12, 2016.

No comments:

Post a Comment