Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania Prof Yunus
Mgaya akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) Kuhusu uamuzi wa Tume
kufuta usajili wa vyuo vikuu vishiriki vya Mtakatifu Joseph tawi la
Songea. Picha na Raymond Mushumbusi
MAELEZO
Na Nyakongo Manyama MAELEZO
TUME ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefuta kibali
kilichoanzisha vyuo vikuu viwili vishiriki vya Mtakatifu Joseph ambavyo ni Chuo
Kikuu kishiriki cha Sayansi ya Kilimo na Teknolojia (SJUCAST) na Chuo Kikuu
kishiriki cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (SJUIT) vilivyopo Songea.
Akizungumza na waandishi wa habari leo katika ofisi za Tume
hiyo, Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania, Prof. Yunus Mgaya amesema kutokana na
mapungufu yaliyobainishwa na Tume ambayo ni matatizo ya ubora wa elimu na
ukiukwaji wa Sheria za uendeshaji wa Chuo Kikuu kama ulivyobainishwa na Sheria
ya Vyuo Vikuu hii imepelekea Tume
kuchukua hatua ya kufuta usajili wa vyuo hivyo.
“ kutokana na yaliyobainishwa hapo awali tunapenda kutaarifu
umma kwamba ,Tume imejiridhisha kuwa hivi vyuo vikuu vishiriki viwili havitoi
elimu ya Chuo kikuu ya viwango stahiki na ukizingatia wanafunzi katika Vyuo
hivi ndio waathirika wakubwa wa matatizo yaliyopo”Alisema Prof Mgaya.
“Napenda kufafanua kwamba Vyuo vikuu vishiriki tuliyovifutia
usajili ni tawi la Songea na Vyuo vingine vishiriki vya Mtakatifu Joseph
vilivyopo Dar es Salaam na Arusha vitaendelea kufanya kazi kama kawaida”Alisema
Prof Mgaya.
Prof Yunus Mgaya amesema wanafunzi wote wanaosoma katika
vyuo vishiriki vilivyofutwa usajili wanaarifiwa kuwa watahamishiwa kwenye vyuo
vikuu vingine vinavyofundisha programu za masomo zinazofanana na masomo
wanayosoma hivi sasa chini ya utaratibu uliopangwa.
Amevitaja vyuo ambavyo watapelekwa wanafunzi walipo katika
vyuo vishiriki vilivyofutwa usajili kuwa ni Chuo Kikuu cha kilimo Sokoine
(SUA), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM),Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mwenge(MWECAU) na Chuo Kikuu
cha Kikatoliki cha Ruaha(RUCU).
Amesisitiza kuwa orodha ya majina ya wanafunzi na vyuo
watavyohamishiwa yatawekwa kwenye tovuti ya Tume hivi karibuni na wale wote
wanaonufaika na Mikopo toka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, mikopo
yao itahamishiwa katika vyuo watakavyokuwa wamehamishiwa.
Vyuo vikuu vyote chini vinakumbushwa kufata Sheria na
kuzingatia utoaji wa elimu inayokidhi viwango vya ubora vinavyokubalika kitaifa
na kimataifa, hivyo Tume haitasita kuchukua hatua stahiki kwa chuo kikuu
chochote kitakachobainika kutoa elimu isiyokidhi viwango vya ubora kwa
kisingizio cha aina yoyote.
No comments:
Post a Comment