Social Icons

IMETOSHA

IMETOSHA

Friday, March 18, 2016

KIWANDA CHA RHINO CEMENT CHA TANGA CHAFUNGIWA KWA UHARIBIFU WA MAZINGIRA


Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Raisi Muungano na Mazingira Mh. Luhaga Mpina (MB) amekifungia kiwanda cha kuzalisha cement na chokaa kilichopo jijini Tanga cha Rhino Cement, leo jioni kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni uharibifu na uchafuzi wa mazingira na kuvunja sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake.
Mh. Mpina amechukua uamuzi huo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wa kata ya maweni kupitia diwani wa kata hiyo Bw. Joseph Colvas na kujionea mwenyewe namna ambavyo kiwanda hicho kinavyo achilia moshi mzito kwenda angani, pamoja na vumbi lisilovumilika kusambaa katika maeneo ya makazi ya wanachi wa kata hiyo ikiwa ni pamoja na kusambaa katika maeneo ya shule ya sekondari ya Don Bosco ambapo, Mh. Mpina ameelezwa kuwa athari zitokanazo na uachiachi wa hewa hiyo chafu angani si tu kwa watoto wa shule zinazozunguka kata hiyo bali pia ni kwa viumbe hai na mazingira.

“Hawa jamaa wamekuwa wakiachilia vumbi jingi na moshi mzito kutoka katika kiwanda hiki mara kwa mara, hivi tangu jana wamezima mitambo yao wakijua kabisa kuwa kuna ugeni wa Naibu Waziri kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Alisisitiza Bw. Joseph.”
Kwa upande wake Afisa Afya wa jiji la tanga aliyejulikana kwa jina moja la bwana Kizito alimuelezea Naibu Waziri Mpina kuwa ni kweli kiwanda hicho kimekuwa kikifanya uchafuzi huo wa mazingira, na Afisa uendeshaji kutoka Baraza la Taifa na HIfadhi ya Mazingira NEMC Bw. Novatus Mushi ameeleza kuwa kiwanda hicho kimeshawahi kutozwa faini ya shilingi milioni kumi na saba (17) kwa kosa la kuchelewa kulipa ada ya mwaka ya mazingira pamoja na uharibifu wa mazingira uliokuwa ukifanywa na kiwanda hicho kwa upande wa kuzalisha chokaa.

 
Mh. Mpina ameelekeza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ( NEMC) kukifunga kiwanda hicho kisiendelee na uzalishaji kwa muda usiopungua miezi mitatu, na kulitaka baraza hilo lijiridhishe na kufuatilia namna kiwanda hicho kinavyotakiwa kutekeleza sheria ya mazingira kwa kujenga mfumo wa kisasa wa kutoa taka zitokanazo na uzalishaji kiwandani hapo pamoja, na kupima vumbi na moshi utokao kiwandani hapo kama hautakuwa na madhara na athari kwa mazingira na viumbe hai. Kinyume na hapo kiwanda hicho kitafungiwa moja kwa moja.
Aidha, akitolea mfano wa kiwanda cha bonite bottles cha mjini moshi kwa kuwa kinara katika upandaji miti na utunzaji wa mazingira, mh Mpina alivitaka viwanda vingine viige mfano wa kiwanda hicho cha coke cola.
Ziara ya Mh. Mpina Jijini Tanga ilihusisha pia kuangalia namna ukuta wa fukwe ya Pangani uliojengwa enzi za mkoloni, ulivyo athirika na madhara yatokanayo na athari za mabadiliko ya tabia nchi na kusema kuwa, ukuta huo huko kwenye mchakato wa kujengwa na kuboreshwa upya, ifikapo mwezi wa  nne mwaka huu mradi wa ujenzi wa ukuta huo utaanza kutekelezeka kwa kuwa tenda imeshatangazwa na jumla ya kiasi cha fedha za kimarekani dola milioni 1,400 zimepatikana kupitia mfuko wa nchi maskini zaidi duniani (LDCf).
Mh. Mpina aliwaasa wakazi wa mji wa Tanga na viunga vyake kutunza mazingira kwa kupanda miti na kufanya usafi kama ilivyoagizwa na serikali, ili kuhepukana na nchi kuwa janga na magonjwa yatokanayo na uchafu.

Waziri Mpina Pia alitembelea kiwanda cha maziwa cha Tanga Fresh na kiwanda cha Tanga Cement na kuridhirishwa na namna ambayo wanatekeleza sheria ya mazingira ya mwaka 2004 na kanuni zake.
Chanzo Issa Michuzi Blog

No comments:

Post a Comment