WAZIRI
wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe amesema kuwa atamfukuza kazi Meneja
Mkuu wa Shirika la Reli la Tanzania na Zambia (TAZARA), Abdallah
Shekimweri iwapo atashindwa kusimamia majukumu yake ikiwa ni pamoja na
kuwapa vitendea kazi na posho wafanyakazi wa shirika hilo.
Licha
ya kusema hayo, ameahidi kutembelea Tazara kesho na pia kukutana na
upande wa Zambia ili kujadili matatizo yaliyopo katika reli hiyo na
kuyapatia ufumbuzi.
Hayo
aliyasema jana jijini Dar es Salaam, alipofanya ziara ya kushitukiza
kujionea utendaji kazi katika karakana za Tazara, Kampuni ya Reli
Tanzania (TRL) na Bandari.
Dk.
Mwakyembe, alisema, haridhishwi na ufanyaji kazi katika karakana ya
Tazara na kumtaka Shekimweri kuwapa vifaa wafanyakazi hao na iwapo
atashindwa kufanya hivyo, atalazimika kumfukuza kazi.
“Jamani
tutafukuzana hapa, vijana wapo tayari kufanya kazi, lakini
mnawakwamisha …naomba mmueleze Shekimweri kuwa nitamfukuza na
niwahakikishie kuwa ninalazimika kurudi hapa kesho Jumatatu,” alisema
Mwakyembe.
Alisema
kuwa, anashangazwa kuona menejimenti ya Tazara ikishindwa kutoa fedha
kwa watumishi wakati serikali imeshatoa ili kukarabati mabehewa ya treni
yanayotakiwa kuanza kutoa huduma ya usafiri kwa wakazi wa jijini
kuanzia Oktoba, mwaka huu.
“Hivi
naomba niulize hizo fedha mnaziweka makao makuu ni maua hayo…naomba
muwalipe watu fedha zao na mnunue vifaa, nawaambia kweli tutafukuzana
hapa, hakuna wa kunilaumu,” alisema Mwakyembe.
Hata
hivyo, aliitaka menejimenti hiyo kukamilisha mabehewa 14 aliyoyaagiza
ambapo hadi sasa ni mabehewa manne ndiyo yaliyoonekana kuanza
kukarabatiwa.
Baadhi
ya watumishi waliokuwa eneo hilo, walilalamikia hatua ya menejimenti ya
Tazara kushindwa kupeleka makato ya mishahara yao katika Mifuko ya
Hifadhi ya Jamii, ukiwemo, NSSF.
Pia, walidai kuwa huu ni mwezi wa pili hawajalipwa mishahara yao hatua inayowafanya waishi kwa tabu na familia zao.
Mwakyembe alimtaka meneja wa karakana hiyo kuhakikisha watumishi hao wanalipwa posho zao kwa wakati.
Kwa
upande wa TRL, waziri huyo, aliliridhishwa na utendaji kazi na kusema
kuwa, anaamini wanaenda na muda na ifikapo Oktoba, huduma ya treni
itaanza kama ilivyotangazwa.
Usafiri
wa njia ya treni kwa wakazi wa jijini, unatarajia kuanza kutolewa
Oktoba mwaka huu kwa lengo la kuondoa tatizo la msongamano.
TANZANIA DAIMA
No comments:
Post a Comment