Kuanzia leo taarifa ya habari ya Azam TV itakuwa ikisomwa na watangazaji wawili na kutakuwa na pea tatu tofauti za watangazaji.
Dar es Salaam. Kituo cha Televisheni cha Azam kimefanya mabadiliko katika utangazaji wa taarifa za habari, huku kikimuajiri Jane Shirima kuwa mkurugenzi wa televisheni.
Kuanzia leo taarifa ya habari ya Azam TV itakuwa ikisomwa na watangazaji wawili na kutakuwa na pea tatu tofauti za watangazaji.
Naibu Mtendaji Mkuu wa Azam Televisheni, Tido Mhando alisema jijini Dar es Salaam jana kuwa wamejiandaa vilivyo kuhakikisha kuwa mbali na studio bora wanakuwa pia na kikosi cha wanahabari wenye uwezo mkubwa.
“Hapana shaka tunao vijana wazuri sana, lakini pia tulihitaji waandishi wenye uwezo na ujuzi wa hali ya juu ili kuendana na mikakati, fikara na mipango yetu ya kufanya mageuzi makubwa ya hali ya utangazaji wa habari za televisheni nchini,” alisema Tido.
“Duniani pote vituo vingi vya televisheni na redio vilianzishwa kwa mtindo kama huu. Kituo cha lugha ya Kiingereza cha Al Jazeera kilipoanzishwa kiliajiri watangazaji waliobobea kutoka mashirika kadhaa makubwa ya utangazaji duniani ikiwa ni pamoja na CNN, BBC na NBC. Lakini pia lazima kuwepo na hadhi ya kuweza kuwavutia watu hao,” alisema mkurugenzi huyo wa zamani wa redio Idhaa ya Kiswahili ya BBC.
Tido aliwataja baadhi ya waandishi na watangazaji ambao wameungana na Azam TV kuwa ni Charles Hilary, Baruani Muhuza, Ivona Kamuntu na Fatuma Almasi Nyangasa.
“Watangazaji hao sasa wataungana na wasomaji wetu wazuri wa siku nyingi Rehema Salum na Nurdin Suleiman kukamilisha pea tatu za wasomaji wa mtindo wa wawili wawili,” alifafanua Tido.
Tido alisema leo na kesho habari itasomwa na Charles Hillary na Ivona Kamuntu wakati siku mbili nyingine itakuwa ni zamu ya Baruhani Muhuza na Fatuma Nyangasa huku Rehema Salum na Nurdin Suleiman nao wakiwa na zamu yao.
Alisema licha ya taarifa ya habari ya saa mbili usiku pia wanatarajia hivi karibuni kuanzisha taarifa ya habari ya saa saba mchana itakayokuwa ikiendeshwa na Zainab Chondo na Raymond Nyamwihula.
“Mpango wote huu wa mabadiliko haya ya utangazaji na upatikanaji wa habari wa Azam TV utakuwa unasimamiwa na kuratibiwa na Joseph Warungu aliyekuwa Mwafrika wa kwanza kuongoza kitengo cha BBC cha Focus on Africa,” alisema Tido.
Tido aliwataja wanahabari wengine mbao wamejiunga na Azam TV kuwa ni Taji Liundi, Phillip Cyprian, Mwanga Kirahi na Jane Shirima ambaye ataanza kazi leo kama mkurugenzi wa televisheni.
Wakati huohuo, Tido alisema kuanzia Jumamosi wiki hii watazindua kipindi maalumu cha mahojiano ya kina kwa wote waliotangaza na kuchukua fomu za kugombea nafasi ya urais. Kipindi hicho kinachojulikana kwa jina la Funguka kitakuwa kinatangazwa kila siku kuanzia saa moja kamili usiku.
Tido alisema katika muda wa mwezi mmoja ujao Radio ya Azam Media Group itakayojulikana kwa jina la UFM itakuwa hewani
No comments:
Post a Comment