Kigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Muheza mkoani
Tanga, Ally Mkufya (60), anadaiwa kujiua kwa kujipiga risasi shingoni.
Mkufya ambaye alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya
Halmashauri Kuu ya Wilaya hiyo, alijipiga risasi jana alfajiri akiwa chumba
alichokuwa akiishi kwenye baa yake ya Tete Pub Extra ambayo pia ina sehemu ya
nyumba ya kulala wageni, iliyopo pembeni ya barabara ya kwenda Tanga mjini.
Kigogo huyo wa CCM ambaye pia ni mfanyabiashara anayemiliki
baa kadhaa, anadaiwa kukatisha maisha yake kwa kujipiga risasi shingoni wakati
huo akiwa amejifungia chumbani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Costantine Massawe,
akizungumzia kifo hicho alisema uchunguzi unafanyika ili kujua chanzo cha
kujiua kwa kujipiga risasi ingawa baadhi ya watu wanasema kifo hicho kimetokana
na sababu za kifamilia zilizomfanya ahame nyumbani kwake na kuishi baa kwa muda
mrefu.
Viongozi wa chama wilayani humo akiwamo Mwenyekiti Peter
Jambele, Katibu Mwenezi , Makame Seif na Katibu wa CCM wa Wilaya ya Muheza,
Josephin Mbezi, walielezea kusikitishwa na kifo hicho walichosema ni kibaya.
Awali akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mlinzi wa baa
hiyo, Idd Abdallah, alisema alipoingia kazini juzi jioni hakukutana na mwajiri
wake licha ya kwamba alikuwa na kawaida ya kukaa nje hadi usiku baa
inapofungwa.
Alieleza kuwa aliingiwa na hofu na kuwauliza wahudumu,
lakini alijibiwa kuwa bosi wao amejipumzisha chumbani kwake kwa kuwa anajisikia
homa na kwamba hali iliendelea hivyo hadi muda wa kufunga baa ulipofika na
wahudumu kuondoka.
Mlinzi huyo alisema kuwa ilipofika asubuhi wahudumu
walifungua baa na kufanya usafi, lakini cha kushangaza Mkufya alikuwa hajaamka
jambo ambalo halikuwa kawaida yake kulala hadi wakati huo.
Hofu hiyo iliwafanya kugonga mlango, lakini haukufunguliwa
hivyo kulazimika kuwapigia simu ndugu zake ili waje kwenye baa hiyo.
Abdallah alisema walipofika chumbani kwake walivunja mlango
na kumkuta amekufa kwa kupigwa risasi shingoni na bunduki aina ya Short ikiwa
pembeni yake huku damu zikiwa zimetapakaa chumba kizima.
Alisema walipiga simu polisi na askari walifika kuuchukua
mwili wa marehemu hadi hospitali Teule wilayani Muheza ambako umehifadhiwa.
KAULI YA MKEWE
NIPASHE ilifika nyumbani kwa marehemu jana na kumkuta mkewe,
Anna Mkufya, akiwa katika majonzi makubwa. Hata hivyo, hakuwa tayari kuzungumza
lolote juu ya tukio hilo.
Marehemu ameacha watoto watano na anatarajiwa kuzikwa kesho
katika kijiji cha Semgao wilayani Muheza.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment