HATIMAYE mkazi wa kijiji cha Nhelegani manispaa ya
Shinyanga Lugenzi Maguta (45), aliyeshambuliwa kwa kipigo na askari magereza wa
gereza la wilaya ya Shinyanga baada ya kuwanyima soda na biskuti amefikishwa
mahakamani na kusomewa shitaka la kufanya fujo gerezani.
Maguta amefikishwa katika mahakama ya mwanzo Shinyanga mjini
ambapo upande wa mashitaka ulimsomea shitaka la kuingia gerezani na kufanya
fujo akidaiwa kulazimisha kumpatia soda na biskuti ndugu yake aliyekuwa
mahabusu shitaka ambalo mshitakiwa amelikana.
Mshitakiwa huyo anashitakiwa kwa kosa la kufanya fujo
katika Gereza la wilaya ya Shinyanga mnamo Desemba 7, mwaka jana mnamo saa 5.00
asubuhi alipokuwa amekwenda kumsalimia ndugu yake aliyetajwa kwa jina la
Mahushi Nangale aliyekuwa akishitakiwa kwa kosa la kuchukua ng'ombe kutoka kwa
baba yake.
Hata hivyo kwa mujibu wa mashitaka aliyosomewa katika
mahakama hiyo ya mwanzo ya mjini Shinyanga mbele ya Hakimu Ruth Meshack
mshitakiwa huyo alifanya fujo ambazo zingehatarisha usalama wa gereza baada ya
kulazimisha kumpatia ndugu yake vyakula (soda na biskuti) ambavyo haviruhusiwa
gerezani.
Mara baada ya kusomewa shitaka hilo mshitakiwa alikana
kufanya fujo gerezani kama alivyoshitakiwa ambapo hakimu aliuhoji upande wa
mashitaka ni njia zipi alizotumia kuingia gerezani mshitakiwa siku hiyo ya
tukio iwapo ni za kawaida au alivunja mlango na kujibiwa kuwa aliingia kwa
kufuata taratibu zote za magereza.
Mahakama hiyo imeiahirisha kesi hiyo mpaka Desemba 28,
mwaka huu itakapoendelea kutajwa mahakamani hapo na mshitakiwa yupo nje kwa
dhamana mpaka siku hiyo ya kesi.
Akizungumza nje ya mahakama Maguta aliwaeleza
waandishi wa habari kushangazwa kwake na jinsi ambavyo askari magereza
waliomshambulia kwa kipigo bila kosa lolote wanavyoshinikiza kutaka kumbambikia
kesi japokuwa siku hiyo ya tukio hawakuwa zamu.
Alisema shitaka alilofunguliwa halina ukweli bali
chanzo cha kushambuliwa kwake ni baada ya kuwanyima askari magereza
waliokuwa zamu siku hiyo soda na biskuti vyenye thamani ya shilingi 2,000
ambapo wakati akitoka nje ndipo alipodakwa na askari wanaomshitaki hivi sasa
waliokuwa wamevaa kiraia waliomrudisha ndani na kuanza kumshambulia kwa kipigo.
“Ninashangazwa na kitendo cha kufunguliwa mashitaka
kwamba eti nilifanya fujo gerezani, ajabu watu wanaofungua kesi hii siyo
waliokuwa zamu siku hiyo, wao walinihoji eti kwa nini ninawasimulia watu
wengine kwamba niliombwa niwachie soda na biskuti askari wenzao waliokuwa zamu
siku hiyo baada ya kuelezwa vitu hivyo haviruhusiwi kupewa mahabusu,”
“Sasa kitendo hicho ndicho kilikuwa chanzo cha
kushambuliwa kwangu, mmoja wa askari magereza aliyekuwa katika eneo la magereza
siku hiyo baada ya kuona nimejeruhiwa miguuni na damu zinanitoka kwa wingi
alishauri suala hili tulifikishe kituo cha polisi ili tukalimalizie huko, ajabu
kufika wenzangu wakanibambikia kesi ya kufanya fujo,” alieleza.
Hata hivyo kwa upande wake mmoja wa wasemaji wa Jeshi
la Magereza mkoani Shinyanga Grace Massawe aliyewahi kuhojiwa na waandishi wa
habari juu ya kuwepo kwa tukio hilo alikana kutokea kwa vuguru gerezani ambapo
hata hivyo alishangazwa na kitendo cha mwananchi kupigwa akiwa ndani ya gereza
kitendo kinachokatazwa hata kama ni kwa mfungwa au mahabusu.CHANZO MT
No comments:
Post a Comment