KWA mara nyingine tena, Jeshi la Polisi mkoani Mwanza, limelazimika
kutumia nguvu kubwa kwa kufyatua mabomu ya machozi na risasi za moto
hewani, kutokana na vurugu kubwa zilizotokea dhidi ya waumini wa dini ya
Kiislamu, waliokuwa wamevamia kwenye Mahakama ya Mwanzo jijini hapa
kisha kusababbisha taharuki kubwa.
Mwandishi wa mtandao huu wa
www.francisgodwin.blogspot.com kutoka mkoani mwanza Sitta Tumma
anaripoti kuwa Vurugu hizo kubwa zilitokea leo majira ya saa 2:20 hivi
asubuhi, baada ya waumini wa dini hiyo ya Kiislamu kuvamia katika
Mahakama hiyo kwa lengo la kusikiliza kesi inayowakabili waumini wanne
wa dini ya Kikiristu, ambao wanatuhumiwa kuchoma Korani, na baada ya
mahakama kuwaachia kwa dhamana watuhumiwa hao, ndipo kasheshe
ilipoanzia na kusababisha ghasia kubwa.
Kufuatia hali hiyo,
waumini wengi wa Kiislamu walionekana dhahiri kupinga kitendo cha
mahakama hiyo kuwapa dhamana watuhumiwa hao, licha ya sheria za nchi
kuruhusu dhamana kwa kila raia kutegemea na kosa la mshakiwa.
Wakiwa
wametanda nje ya mahakama hiyo, baadhi ya waumini hao wa dini hiyo ya
Kiislamu, walisikika wakilalamikia kwa kusema kwamba, iwapo washakiwa
hao watapewa dhamana na mahakama, wao wapo tayari kuwahukumu papo hapo,
jambo lililoonekana kuwashtua watu wengi waliokuwa wakifuatilia
mwenendo wa kesi hiyo.
"Tutatoa hukumu yetu hapa kama mahakama
itawaachia watu hawa. Hatutaki pia kesi hii iendelee kuahirishwa mara
kwa mara, tunataka haki itendeke vinginevyo tutawahukumu hapahapa,
maana walichana Korani tukufu", alisikika muumini mmoja wa Kiislamu
akisema nje ya mahakama hiyo.
Kufuatia hali hiyo, polisi walipata taarifa ya kuwepo viashiria vya uvunjifu wa amani katika eneo
hilo la mahakama, na walifika haraka katika eneo
hilo na kuwataka waumini hao kuondoka haraka kwenye eneo hilo, lakini walikataa kutii
amri hiyo ya polisi.
Baada
ya waumini hao kugoma kuondoka, polisi walilazimika kujipanga kisha
kuanza kupiga mabomu ya machozi hewani, hali ambayo ilizua mtafaruku
mkubwa, ambapo waumini hao wa Kiislamu walionekana kujibu mapigo kwa
kuwashambulia polisi kwa mawe.
Polisi walipoona wanashambuliwa,
walilazimika kujihami kwa kuzidisha mashambulizi kwa kufyatua mabomu ya
machozi ovyo hewani, huku milio ya risasi za moto ikisikika, na kwamba
baadhi ya barabara zilifungwa na kuzuiwa magari, pikipiki kuingia
katikati ya jiji.
Katika vurugu hizo baadhi ya wananchi walijeruhiwa na mabomu hayo, ambapo
Tanzania
Daima ilishuhudia muuza magazeti mwanamke anayeuza magazeti katika
eneo la Bantu akiwa amejeruhiwa shingoni na mkononi baada ya bomu la
machozi kulipuka mbele yake.
Watu waliokuwa wakiingia katikati
ya jiji, wakiwemo wafanyakazi walilazimika kushuka kwenye magari umbali
wa zaidi ya kilometa tano, kisha kutembea kwa miguu hadi mjini, na
kwamba askari polisi kitengo cha Usalama barabarani ndiyo waliokuwa
wakiwajibika kuzuia magari yote yasiingie mjini kwa takriban saa mbili
hivi.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoa
wa Mwanza, Liberatus Barlow (RPC), alisema polisi walilazimika kutumia
nguvu hiyo kubwa kwa lengo la kuimarisha usalama wa raia na
mali zao, ikiwa ni pamoja na kuwatawanya waumini hao wa Kiislamu wasiendelee kufanya fujo mahakamani hapo.
Alisema, tayari
kuna
watu 19 wakiwemo baadhi ya viongozi wa Kiislamu wamekamatwa, na
wanafanyiwa mahojiano maallumu na jeshi hilo la polisi, na kwamba jeshi
hilo linawasaka watu wengine wanaodaiwa kusababisha vurugu hizo kubwa.
"Polisi
hatuwezi hata siku moja kuruhusu uvunjifu wa amani utokee mahala
popote. Na ndiyo maana tumelazimika kutumia nguvu kwa ajili ya
kurejesha usalama!. Lakini tayari kuna watu 19 tumewakamata, na wamo
baadhi ya viongozi wao...sheria lazima ifuate mkondo wake katika hili",
alisema Kamanda Barlow.
Hivi karibuni waumini wa dini ya
Kikiristu walifikishwa katika mahakama ya Mwanzo jijini Mwanza,
wakituhumiwa kuchoma Korani tukufu, baada ya mwanamke mmoja muumini wa
dini ya Kiislamu kuombewa na kubahatika kupata mtoto katika Kanisa moja
jijini hapa na waumini hao kuamua kuchoma moto Korani hiyo kinyume cha
sheria za nchi.
Miezi mitano iliyopita, Jeshi la polisi mkoani
Mwanza, liliingia kwenye majaribu baada ya kulazimika kutumia mabomu na
risasi za moto kupambana na ghasia kubwa zilizofanywa na
wafanyabiashara wadogo jijini hapa , maarufu kwa jina la 'Machinga',
ambapo waligoma kuondoka eneo la Makoroboi ambalo haliruhusiwi
kuendesha biashara za machinga, kwani lipo karibu sana na msikiti na
shule moja ya awali.
Mapigano hayo makali yaliyosababisha mtu
mmoja kufariki dunia kutokana na kile kilichoelezwa kupigwa risasi ya
aina ya Shortgun, ilikuwa ni mwendelezo wa vurugu kama hizo zilizowahi
kufanyika tena kabla ya mwezi Juni mwaka huu, kisha kuleta kizaazaa
kikubwa na kusababisha hasara kubwa.
No comments:
Post a Comment