
WANACHUO
wa Chuo Kikuu cha St John mjini Dodoma, jana wamegoma kuingia madarasani
hadi wawasilishe malalamiko yao kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Zelothe
Stephen kutokana na kukithiri kwa vitendo vya kupigwa nondo, kuibiwa
kadi za benki, kompyuta za mkononi, kulawitiwa na kubakwa.
Hali
hiyo ilisababisha wanafunzi kukusanyika huku wakiwa wamebeba mabango
mbalimbali ambayo yalikuwa yakisomeka, ‘Tunaomba ulinzi ili kubaka na
kulawitiwa kukomeshwe’, ‘Ulinzi ni haki yetu ya msingi polisi Mko wapi?
Tumechoka kuwa wajinga katika jamii yetu na Ulinzi Shirikishi stop
crime.’
Baadhi
ya wanafunzi hao walilaani vitendo vya wenzao kubakwa na kulawitiwa na
kudai kuwa katika siku za hivi karibuni, mwanafunzi wa kiume ambaye
anasoma mwaka mwaka wa pili aliibiwa na kisha kulawitiwa hali
iliyolazimu alazwe hospitali.
“Kesi kadhaa zimepelekwa polisi lakini hakuna chochote kinachofanyika,” alisikika mwanachuo moja akizungumza kwa jazba.
Walisema
kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na wakati mgumu kutokana na
kuibiwa vifaa muhimu zikiwemo kompyuta za mkononi hali ambayo hulazimika
kuishi kwa hofu.
“Juzi
wenzetu wamevamiwa usiku na kuporwa simu tano na laptop tatu sasa
tunaona maisha yanakuwa magumu sana kwetu kwani usalama wetu sasa ni
mdogo,” alisema mmoja wa wanafunzi hao.
Walisema
hali ni mbaya zaidi kwa wanafunzi ambao wanaishi nje ya chuo kwani hata
kujisomea nyakati za jioni kumekuwa kwa mashaka kutokana na kuogopa
kuvamiwa na vibaka.
Walisema
baadhi ya wenzao wanaanza mitihani Juni, hali ambayo inawatia hofu kama
wimbi hilo la kuvamiwa na vibaka linaweza hata kupunguza ufaulu
mioungoni mwao.
Pia
walitaja sababu kadhaa ambazo zinadhaniwa kuwa zinasababisha matukio
hayo ni chuo hicho kukosa uzio na hivyo kufanya mwingiliano wa watu na
wanachuo kuingia chuoni bila kuwa na utaratibu.
Walisema
kundi lisilojulikana limekuwa na kawaida ya kuvamia sehemu ambazo
wanachuo wanakaa na baada ya kuiba vitu mbalimbali humalizia kwa kubaka
wasichana au kwa kulawiti kama ni mvulana.
Hata
hivyo, juhudi za wanafunzi wao kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma
hazikufanikiwa baada ya kuelezwa kuwa alikuwa na majukumu mengine ya
kikazi, na kutuma mwakilishi wake ambaye ni Mkuu wa Polisi Wilaya,
Dominic Mlei na Mkuu Mpya wa Polisi wa Wilaya atakayeanza kazi hivi
karibuni, Thadeus Malingumu.
Kwa
upande wake, OCD Mlei alisema ulinzi unaanza rasmi leo, kufanya doria
maeneo yanayozunguka chuo hicho na maeneo jirani, pia chuo kijenge
hosteli za kutosha na kwa kila hosteli za nje na nyumba walizopanga
wanafunzi zitakaguliwa kesho na mapungufu ya kiusalama kwenye makazi
hayo yataainishwa na wamiliki wataitwa na hosteli zote zitatakiwa kuwa
na mageti na ulinzi wa makazi hayo kuboreshwa.
Pia alitaka kuundwa kwa mara moja kwa vikundi vya ulinzi shirikishi.
Hata hivyo, mtumishi wa Chuo hicho, Mzee Muganda alishauri Kituo Kidogo cha Polisi kijengwe Kikuyu na bidii ya doria iongezwe
Habari na - Sifa Lubasi, Dodoma
Chanzo - http://www.habarileo.co.tz
No comments:
Post a Comment