MFANYABIASHARA
wa baa na nyumba ya kulala wageni ya Bongo Star Lodge iliyopo Kawe
Ukwamani, James Isame, maarufu kama Mzee Chacha (50), anashikiliwa na
Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni kwa tuhuma ya kukutwa na kichwa cha
binadamu anayedhaniwa kuwa ni mlemavu wa ngozi (albino).
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela amethibitisha kushikiliwa
kwa mfanyabiashara huyo na kusema kuwa alikamatwa juzi saa 2:45 usiku
baada ya wasamaria wema kutoa taarifa kwa jeshi hilo juu ya kuwepo kwa
tukio lisilo la kawaida katika nyumba hiyo ya kulala wageni.
Alieleza
kuwa, baada ya taarifa hizo, polisi waliizingira nyumba hiyo kisha
wakamtafuta mjumbe wa eneo la Kawe kwa ajili ya kuthibitisha upekuzi
utakaofanyika na kwamba baada ya taratibu zote, walimtaarifu muhusika
ambaye alianza kuonesha upinzani juu ya kufanyiwa upekuzi.
Alisema
jitihada za mtuhumiwa kuzuia upekuzi huo zilishindikana, ndipo katika
kufanya kazi hiyo maeneo yote ya ndani na nje ya nyumba hiyo pamoja na
baa, walifanikiwa kukuta kichwa cha binadamu kikiwa kimewekwa juu ya
ukuta wa choo.
“Kilikuwa
kimevingirishwa katika mfuko wa rambo na tuliweza kubaini kuwa ni
kichwa cha binadamu baada ya kuona nywele na meno, ila bado hatujajua ni
wa jinsia gani au kama ni mlemavu wa ngozi,” alisema Kenyela.
Akielezea
tukio zima, Kamanda Kenyela alisema baada ya Jeshi la Polisi kupata
taarifa za kuwepo kitu kisichoeleweka katika eneo la mfanyabiashara
huyo, waliweka ulinzi maeneo yote.
Aliongeza
kuwa, kichwa hicho kilikuwa na mchanga hali inayoonesha kuwa huenda
kilikuwa kimefukiwa kabla ya kufikishwa hapo au wakati wa kukatwa
kilikuwa kimewekwa katika mchanga.
Kamanda
Kenyela alisema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea na baada ya
upelelezi kukamilika, watapeleka maoni ya Jeshi la Polisi kwa Mkurugenzi
wa Mashitaka (DPP) kwa ajili ya hatua zaidi.
Baada
ya taarifa hizo kuenea, Tanzania Daima ilifika hadi katika nyumba ya
kulala wageni ya Bongo Star Lodge iliyoko Kawe na kuangalia mazingira ya
eneo zima na kisha kuzungumza na baadhi ya wafanyakazi na majirani.
Eneo
la nyumba hiyo limezungukwa na nyumba nyingine za makazi ya watu, huku
eneo la kuuzia vinywaji likiwa limepakana na vyoo vitatu ambavyo ukuta
wake ndiyo unaosadikiwa kuwekwa kichwa hicho.
Kuanzia
mlango wa kuingilia katika baa hiyo hadi vyumbani, kumesakafiwa na
kuwekwa vigae ambavyo si rahisi kwa mtu kuchimba pasipo kujulikana, huku
vyooni kukiwa na hali hiyo pia.
Mmoja
wa wafanyakazi wa nyumba hiyo aliyeomba jina lake lihifadhiwe alisema
kuwa, walishuhudia askari wakifika katika eneo hilo na kwenda moja kwa
moja katika upande wa choo, na baada ya muda wakaondoka na mmliliki wa
nyumba hiyo.
“Hatukujua
ni kitu gani kinaendelea mpaka meneja alipotuambia kuwa mzee ameshikwa
na kichwa cha binadamu,” alisema mmoja wa wafanyakazi hao.
Majirani
waeneo hilo walipoulizwa kama wanafahamu juu ya jirani yao kukamatwa
kwa tuhuma za kukutwa na kichwa cha binadamu, walishangaa na kusema
ndiyo kwanza wanapata habari hizo kutoka kwa mwandishi.
Kwa
upande wake, mjumbe wa nyumba kumi wa eneo hilo aliyefahamika kwa jina
moja la Mzee Kilambo, alisema aliitwa na polisi kwa ajili ya kushuhudia
upekuzi katika eneo hilo, na kwamba maelezo zaidi ya nini kimetokea
yanapaswa kuulizwa polisi.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment