
Pichani: Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya wa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL), Kapteni Milton Lusajo Lazaro.
IKIWA
ni siku mmoja tu baada ya kuteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji mpya
wa Shirika la Ndege la Air Tanzania (ATCL), Kapteni Milton Lusajo
Lazaro amesema shirika hilo linanafasi kubwa ya kupata mafanikio iwapo
litaendelea kutekeleza mpango wake wa maendeleo wa miaka mitano.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa jana ( leo mtandaoni), Lusajo alisema
atatumia uzoefu wake alioupata katika sekta ya usafiri wa anga kuleta
mabadiliko katika shirika hilo na kuliwezesha kushindana sambamba na
kampuni nyingine za ndani na nje ya nchi.
Kpt.
Lusajo, rubani anaeheshimika katika sekta ya usafiri wa anga si kwa
Afrika Mashariki pekee ila Afrika kwa ujumla ana rekodi ya kuendesha
ndege kwa saa zaidi ya elfu kumi na mbili, pia amewahi kushika nyadhifa
mbali mbali katika Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) pamoja na
ATCL kabla ya kuteuliwa kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL.
“Napenda
kutoa shukrani zangu kwa Waziri Mwakyembe na viongozi wengine wa Wizara
kwa kuwa na imani nami. Nimekubali uteuzi wake na nitafanya kazi
aliyonipa kwa moyo mmoja.
Ninaahidi
kuwa nitautumia uzoefu wangu wa zaidi ya miaka 35 katika sekta ya
usafiri wa anga na kuipa ATCL uwezo kushindana kibiashara. Natoa wito
kwa wafanyakazi wenzangu kutoa ushirikiano ili tuweze kusonga mbele. ”
Alisema.
Lazaro
alisema Shirika lake litaendelea kutoa huduma kama kawaida na kuongeza
kuwa safari zote za Shirika zitaendelea kama ilivyopangwa na ratiba
licha ya mabadiliko ya uongozi.
“Hakuna
sababu ya wananchi kuwa na wasi wasi. Kilichotokea ni mabadiliko ya
uongozi tu lakini mipango na shughuli zote za Shirika zinaendelea kama
ilivyopangwa,” alisema.
Lazaro
aliongeza kusema, kuwa jukumu kubwa alionalo mbele yake ni kuongeza
idadi ya ndege za shirika hilo aidha kwa kukodi au kuingia ubia na
mashirika mengine katika jitihada za kuimarisha nafasi ya kampuni yake
ili iweze kushindana Kitaifa na Kimataifa katika miaka michache ijayo.
“ATCL
haiwezi kupata mafanikio bila kuwa na ushirikiano mzuri na Serikali
pamoja na wananchi kwa ujumla. Nawaomba wananchi waendelee kuonyesha
ushirikiano na uzalendo waliouonyesha katika wiki chache zilizopita
baada ya kuanza kwa huduma za kampuni yetu.
“Nawahakikishia
wateja wetu na wananchi kwa ujumla kuwa kampuni yangu itaendelea kutoa
huduma na bidhaa bora zilizo katika bei za kiushindani ukilinganisha na
makampuni mengine yanayotoa huduma hii katika soko,” alisema.
No comments:
Post a Comment