CHAMA cha Wamiliki wa Daladala Mkoa wa Dar es Salaam (DARCOBOA),
kimetangaza kuanza mgomo kwa ajili ya kupinga manyanyaso wanayofanyiwa
na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) wa
kuzikamata bila utaratibu.
Akitangaza mgomo huo kwa waandishi wa habari Dar es Salaam jana,
Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Sabri Mabrouk, alisema wamechukua uamuzi
huo baada ya SUMATRA kufanya operesheni ya kukamata wagari yao
wakiwatumia walinzi shirikishi.
Alisema kuanzia Jumatatu wiki ijayo, watasitisha kutoa huduma ya
kubeba abiria kutokana na Mamlaka hiyo kushindwa kutekeleza jukumu
walilonalo kwa utaratibu unaokubalika.
“Kimsingi tumekelwa sana na tabia hii ya kutumia watu wa pembeni
kukamata daladala wakati si watumishi wa SUMATRA ambao sisi tunawatambua
na kusababisha kero kwa madereva,” alisema.
Amewataka SUMATRA kuacha kutumia utaratibu huo badala yake kama
wanataka kuendesha oparesheni hiyo, waingie wenyewe barabarani kwa
kufuata utaratibu na sheria walizojiwekea.
Bw. Mabrouk alisema hadi sasa, zaidi ya daladala 100 zimekamatwa
katika msako huo ambao unaoendelea ambapo daladala nyingine zaidi ya
6,000 zimejiandaa kusitisha huduma.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Madereva na Makondakta wa
Daladala (UWAMADAR), Bw. Shukuru Mlawa, alisema kitendo cha SUMATRA
kutumia wakala katika operesheni hiyo ni wazi kuwa jukumu hilo
wamelishindwa.
“Awali mamlaka hii ilitaja sehemu korofi kwa madereva wa daladala
ambazo ni Uhuru, Gongolamboto, Mbagala na Kawawa lakini bado wameshindwa
kutekeleza kazi ya kukamata badala yake imewaagiza watu wa pemebeni
kama vishoka,” alisema.
Chanzo: http://majira-hall.blogspot.com
No comments:
Post a Comment