DAWA mpya inayokinga na kuua kwa kasi virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi, tayari imeshaanza kutumika, hii ni kwa mujibu wa ripoti za mitandaoni.
Dawa hiyo ambayo toleo lake la kwanza ipo kwenye muundo wa vidonge, inaitwa Truvada na tayari imekwishaanza kufanya kazi nchini Marekani.
Kitendo cha Truvada kukubalika na Mamlaka ya Usimamizi wa Chakula na Dawa nchini Marekani (FDA), kinatoa picha kuwa sasa vidonge hivyo vinaweza kuuzwa sehemu yoyote duniani.
Kamishna wa FDA, Margaret Hamburg, amesifu Truvada na kueleza kwamba itapunguza wastani wa maambukizi mapya pamoja na vifo vinavyotokana na ugonjwa wa Ukimwi.
Hamburg alisema kuwa hivi sasa nchini Marekani kumekuwa na kasi ya maambukizi mapya, kwani kila mwaka kumekuwa na wastani wa watu 50,000 wanaobainika kupata Virusi Vya Ukimwi (VVU).
Watafiti waliogundua Truvada wanaeleza kuwa dawa hiyo kwa sehemu kubwa inakinga VVU na upande mwingine inasaidia kuua virusi vya Ukimwi kwa mtu ambaye tayari amekwishaathirika.
Hata hivyo, FDA na watafiti hao, hawajaeleza kama Truvada inatibu moja kwa moja, isipokuwa wanasisitiza: “Inamkinga mtu kupata maambukizi mapya, inamsaidia mwathirika kwa kuua VVU pamoja na kumkinga dhidi ya magonjwa nyemelezi.”
INAFIKAJE TANZANIA
Nchini Marekani, imeelezwa kuwa inabidi serikali ya nchi hiyo ifanye juu chini kugharamia usambazaji wa dawa hiyo ili iwafikie wananchi wa kawaida kwa urahisi.
Imebainishwa kuwa usambazaji wa Truvada kwa mwaka unaweza kugharimu Dola za Marekani 10,000 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 15 za Kitanzania.
Umetolewa wito kuwa serikali zinatakiwa zishughulikie upatikanaji wa dawa hizo na kuzisambaza ili wananchi wake wazipate madukani au kwenye vituo vya afya kwa urahisi.
Limetolewa angalizo kwamba endapo wafanyabiashara wataingilia kati na kununua haki za kusambaza dawa hizo, itasababisha wananchi wa kawaida wanunue Truvada kwa bei kubwa mno ambayo pengine wasio na uwezo wanaweza kushindwa kumudu.
SERIKALI YA TANZANIA INASEMAJE
Mwandishi wetu alijitahidi kwa njia mbalimbali kumpata Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi ili aweze kuzungumzia jinsi Serikali ya Tanzania ilivyojipanga kuhakikisha dawa hiyo inafika nchini lakini hakupatikana.
Hata hivyo, Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamwaja alisema wikiendi iliyopita kwamba hawezi kuzungumza chochote kwa sababu alikuwa ‘bize’ na watendaji wengine kuandaa kuwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni.
Kwa mujibu wa Mwamwaja, Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ilitarajiwa kusomwa jana, hivyo akabainisha kwamba si yeye tu, bali watendaji wakuu wote wa wizara hiyo walikuwa bize.
TRUVADA ILIFANYIWA UTAFITI TANZANIA
Mtafiti wa VVU, Connie Celum wa Chuo Kikuu cha Washington, mjini Seattle, Marekani, kwanza alieleza ugumu wa usambazaji wa dawa hiyo endapo serikali hazitaamua kusimamia kisha akaeleza kwamba Truvada imefanyiwa utafiti karibu mabara yote.
Celum alisema kuwa baada ya Truvada kuendelezwa na Taasisi ya Gilead Sciences kwenye Jiji la Foster, California, ilifanyiwa utafiti Afrika Mashariki (Tanzania ikiwemo) na kusaidia kupunguza maambukizi mapya kwa asilimia 75.
ONYO LATOLEWA
Hata hivyo, baadhi ya watafiti wamesema kuwa pamoja na Truvada kuonekana ni mkombozi dhidi ya Ukimwi kwa sasa lakini haitakiwi kutumika kiholela.
Wamesema kuwa dawa hiyo imeunganishwa kutoka kwenye mkusanyiko wa dozi za kupunguza makali ya virusi, hivyo inaweza kumuathiri mtumiaji.
Imeshauriwa kwamba kabla ya kutumia Truvada ni vizuri kupimwa na kuthibitishwa na daktari kwamba mwili wako una sifa za kutumia dawa hiyo.
TUNDU LISSU ASHINDA UWENYEKITI CHADEMA, MBOWE ABARIKI MATOKEO
-
NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
TUNDU Lissu ameibuka mshindi katika nafasi ya Mwenyekiti Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) dhidi ya mpinzani wake...
45 minutes ago
No comments:
Post a Comment