Ni mwanasheria aliyesimamia ubomoaji wa mahekalu Kunduchi
na Betty Kangonga
KASI
ya vitendo vya utekaji nyara inayotokana na visasi na chuki miongoni
mwa jamii, inazidi kushamiri nchini, hususan jijini Dar es Salaam,
Tanzania Daima Jumatano limebaini.
Wakati wananchi wengi bado wana kumbukumbu ya tukio la kutekwa,
kuteswa na kupigwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk.
Steven Ulimboka, takriban wiki mbili zilizopita, tukio lingine la aina
hiyo limemkumba Mwanasheria wa Baraza la Taifa la Mazingira Nchini
(NEMC), Manchere Heche.
Heche ni mmoja kati ya watendaji wa NEMC waliosimamia mpango mzima
wa ubomoaji wa mahekalu ya baadhi ya vigogo waliojenga kandokando ya
mito ya Mbezi Beach, Mndubwe na eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mikoko
ufukweni mwa Bahari ya Hindi, jijini Dar es Salaam.
Habari ambazo gazeti hili imezipata kutoka chanzo cha karibu na
mwanasheria huyo, zilidai kuwa mwanasheria huyo alitekwa nyara hivi
karibuni katika eneo lilelile alilotekwa nyara Dk. Ulimboka la Leaders
Club majira ya saa 4:00 usiku wakati walipoenda kupata vinywaji na
chakula. Siku ya tukio, mwanasheria huyo aliongozana na wadogo zake.
Akiwa katika eneo hilo, ghafla liliibuka kundi la watu zaidi ya kumi
na kumkamata mwanasheria huyo mithili ya kibaka na kumpeleka eneo la
giza na kisha kuanza kumpiga.
“Yaani tulishangazwa na jinsi watu hao walivyokuwa mahiri kwa
kuzingira gari na kusema kuwa sisi tunauza tiketi bandia jambo ambalo
liliwastaajabisha wale waliokuwa karibu,” kilisema chanzo hicho.
Mtoa habari wetu alisema kuwa Heche alipelekwa eneo ambalo lilikuwa
na giza totoro na kupigwa huku wakijaribu kumsukumia ndani ya roli
lililopaki jirani na eneo la Uwanja wa Leaders Clab.
Hata hivyo chanzo hicho kilisema mwanasheria huyo alipambana vilivyo
na watu hao kabla ya kuokolewa na mzee mmoja aliyekuwa akipita eneo
hilo.
“Yaani hiyo ndiyo ilikuwa pona yake maana bila yule mzee sijui
walitaka kumpeleka wapi hata hatuelewi…hata hivyo tunashanga kwa nini
suala hilo linaibuka sasa maana lilitokea kitambo,” alisema mtoa habari
wetu.
Habari zaidi juu ya tukio hilo zilisema kuwa watekaji hao
walidhamiria kufanya uovu mkubwa kwani walikuwa wamebeba tindikali
ambayo pengine ilikuwa itumike kummwagia mwanasheria huyo.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, tukio hilo liliripotiwa katika kituo cha
polisi cha Oysterbay ambapo mwanasheria huyo alipewa PF3 na kwenda
kutibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ambako alilazwa kwa
zaidi ya wiki mbili kutokana na majeraha aliyoyapata.
Inaelezwa kuwa kabla ya tukio hilo, mwanasheria huyo alikuwa
akipokea simu na ujumbe wa vitisho kupitia ujumbe mfupi wa mkononi
tangu NEMC ilipoanza taratibu za kutaka kubomoa mahekalu ya vigogo wa
eneo la Mbezi Beach.
SOURCE Soma zaidi:http://freemedia.co.tz/daima/habari.php?id=38274
No comments:
Post a Comment