
KOCHA wa Yanga, Mbelgiji Tom
Saintfiet amewaacha kwenye kikosi kitakachoshiriki michuano ya Klabu
Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame kuanzia Jumamosi
wachezaji watatu nyota na chipukizi, Omega Seme, Simon Msuva na Frank
Damayo kwa sababu watakuwa na majukumu ya kitaifa kwa muda mrefu.
Akizungumza na Waandishi wa
Habari mchana huu, makao makuu ya klabu makutano ya Mitaa ya Twiga na
Jangwani, Dar es Salaam, Saintfiet alisema kwamba wachezaji hao watakuwa
na timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, inayojiandaa
mechi ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika Julai 29
dhidi ya Nigeria.
“Kwa mujibu wa kanuni
natakiwa kuwaachia wachezaji siku tano kabla ya mechi, na Jumamosi
wanacheza na Rwanda, Jumatatu wanarudiana na Rwanda, baada ya hapo
watakuwa kwenye maandalizi ya mechi na Nigeria, kwa hivyo sitakuwa nao
hata kwenye Nusu Fainali, kwa sababu hiyo nimeamua kuwaacha,”alisema.
Saintfiet alisema amemtema pia
Nahodha wa klabu hiyo, Nsajigwa Shadrack katika kikosi cha wachezaji
20, lakini amesema mchezaji huyo ni muhimu na atakuwa naye kwenye Ligi
Kuu.
Amewataja wachezaji aliowateua baada ya kushauriana na wasaidizi wake, Freddy Felix Minziro na Mfaume Athumani kuwa ni;
Makipa; Yaw Berko na Ally Mustafa ‘Barthez’
Mabeki; Juma Abdul, David
Luhende, Kelvin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Godfrey Taita,
Ladislaus Mbogo, Oscar Joshua na Stefano Mwasyika
Viungo; Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzima, Shamte Ally, Nizar Khalfan na Idrisa Assenga.
Washambuliaji; Said Bahanuzi, Hamisi Kiiza na Jerry Tegete.
Yanga ndio mabingwa watetezi
wa Kagame, watafungua dimba na mabingwa wa Burundi, Atletico FC Jumamosi
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. na wenyeji blog

No comments:
Post a Comment