CHAMA Cha
Madaktari nchini (MAT), kimesema maandamano yao yako pale pale na
tayafanyika Jumatatu ya Julai 16, saa nne, na si vinginevyo.
Aidha, MAT, kimelaani kutekwa na kupigwa kwa mwenzao Dk. Steven Ulimboka na kufutiwa leseni kwa wanafunzi wa vitendo (interns).
Uamuzi huo
wa MAT, ulitolewa jijini Dar es Salaam, katika kikao cha dharula cha
madaktari 500 walioketi katika ukumbi kituo cha Utamaduni wa Korea.
MAT, kupitia
Katibu wake, Rodrick Kabangila alisema “Kwa pamoja tulilaani vitendo
vya unyanyaswaji wa serikali dhidi yetu, kwanza uamuzi wa Baraza la
Madaktari (MCT), wa kuwafutia leseni wanafunzi wa vitendo bila kuwapa
nafasi ya kuwasikiliza kutoa maelezo yao.
“MCT
lilishindwa kuwaita na kupata maelezo yao badala yake walijichukulia
hatua za haraka za kuwafukuza, wakati suala hilo lipo mahakamani”alisema
Kwa mujibu
wa Kabangila, madaktari wanalaani hatua ya kunyimwa chakula na kufukuzwa
na FFU kwenye vyumba vya kulala (hosteli), madaktari kabla ya taarifa
ya maandishi kutoka Wizarani.
Pia, wanafunzi hao na wengine walinyimwa posho kabla ya barua ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Hivyo,
vitendo hivyo na vingine vinaonyesha udhalilishwaji mkubwa kwao,
ikizingatiwa kuwa ni wanataaluma wanaohitajika ndani ya nchi.
Katika
maelezo yake, taaluma hiyo ina umuhimu mkubwa, na ikiwa unyanyasaji huo
utaendelea, kutasababisha idadi kubwa ya madaktari kuondoka nje ya nchi.
Alionya kwamba endapo wataondoka taifa litakosa madaktari na kutafanya Wananchi zaidi ya milioni 12 kukosa huduma ya afya.
Mbali na
hilo, Katibu huyo alisema, bado milango iko wazi kukutana na serikali
ili kukaa mezani kwa lengo la kumaliza mgogoro wao ambao umedumu kwa
muda mrefu sasa.
Kimsingi, Kabangila alisema kutokana na hatua hizo, wameandaa maandamano pindi watakapopata kibali kutoka vyombo vya usalama.
Hata hivyo, alisema maandamano ni haki yao na kibali ni kwa ajili ya ulinzi wao.
Alifafanua kwamba, maandamano yana lengo la kupinga dhuluma na uonevu dhidi ya taaluma muhimu ya udaktari na madaktari wenyewe.
Alisema, MAT
inasikitishwa na dhuluma hiyo kwa kuzingatia uwiano duni wa madaktari
hapa nchini ambapo daktari mmoja hutibu wagonjwa 30,000 kwa mwaka chini
ya viwango vya kimataifa.
“Tutafanya
maandamano ya amani, madaktari wote na wadau wa sekta hii wenye mapenzi
mema tunawaomba washiriki… madaktari tutavaa makoti yetu meupe na
watakaoshiriki nasi wavae vitambaa vyeupe.
Maandamano
yataanzia nje ya Hospitali ya Taifa Muhimbili, tutaishia kwenye geti la
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, tukiwa na mabango ya kulaani kitendo
cha kutekwa, kupigwa na kutelekezwa kwenye msitu wa Pande alichofanyiwa
Dk. Steven Ulimboka,” alisema.
Dk.
Kabangila alisema kuwa wataishinikiza serikali iunde tume huru kwa ajili
ya kuchunguza suala la Dk. Ulimboka itakayofanya kazi haraka na
wahusika wote wafikishwe kwenye vyombo vya sheria.
No comments:
Post a Comment