|
KAMPUNI ya Usambazaji wa MajiSafi katika Mkoa wa Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani, (Dawasco) limesema Jiji la Dar es Salaam litakabiliwa na uhaba wa maji kwa siku kadhaa. Kufuatia hali hiyo, kampuni imewataka wakazi wa mkoa huo, kutumia maji kwa umakini katika kipindi hiki ya kuifanyia matengenezo ya mifumo ya umeme katika mtambo wa Ruvu Chini. Mtambo huo ulizimwa jana , ili kuruhusu makandarasi kuhamisha mfumo wa umeme. Akizungumza na gazeti hili jijini jana, Ofisa Mawasiliano wa Dawasco, Thed Mlengu. alisema matengenezo hayo yatadumu kwa siku kadhaa na kwamba wananchi watakaoathiriwa ni wa maeneo ya mji wa Bagamoyo, Mapinga, Bunju, Boko, Tegeta, Kunduchi, Salasala, Jangwani, Mbezi Beach na Kawe. “Kuna mradi wa wa upanuzi wa mitambo ya kuhamisha mifumo ya umeme wa bomba la Ruvu Chini, lengo ni kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na maeneo jirani yanayopata maji kutoka kwenye mtambo huo,”alisema Mlengu. Alisema maeneo mengine yatakayoathiriwa na tatizo hilo ni Mlalakua, Mikocheni, Mwenge, Msasani, Sinza, Kijitonyama, Kinondoni, Oysterbay,Magomeni, Upanga, Kariakoo, Ilala, Ubungo Maziwa, Kigogo, Mburahati, Muhimbili, Ubungo na katikati ya jiji. Alisema kutokana na hali hiyo wananchi wanatakiwa kuhifadhi maji ili kuhakikisha kuwa wanapata huduma hiyo bila matatizo hasa katika kipindi hiki cha matengenezo ya mtambo. |
No comments:
Post a Comment