|
KITENDO cha wabunge wengi kuhudhuri kikao cha Bunge na kusababisha Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kutopitishwa, kimewachukiza wananchui wa kada mbalimbali wakisema huo ni ufisadi.
Mwishoni
mwa wiki iliyopita Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alilazimika
kuahirisha upitishaji wa bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika
kwa mwaka 2012/13, baada ya idadi ya wabunge Bungeni kuwa ndogo.
Wakizungumza
na gazeti kwa nyakati tofauti jana kuhusiana na tukio hilo baadhi ya
wananchi walisema kuwa, wabunge wanalipwa posho nyingi ili watekeleze
majukumu yao, lakini wanazembea kwa kutoshiriki kikamilifu katika vikao
vya Bunge kama walivyofanya mwishoni mwa wiki.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea
Nkya alisema kitendo cha wabunge wengi kutokuwapo wakati wa majadiliano
ya bajeti ni changamoto katika suala zima la utawala bora na uwajibikaji
hapa nchini.
"Spika atueleze wabunge ambao hawakuwapo wakati
walikuwa wapi? Walikuwa wanafanya nini na kwa ruksa ya nani? Na wananchi
tuambiwe," alisisitiza Nkya.
Aliongeza kuwa, wawakilishi hao wa
wananchi wanalipwa fedha zinazotokana na kodi za wananchi, hivyo ni
vizuri wanaotoa fedha hizo wapate taarifa sahihi juu ya tukio hilo.
Nkya alisema utoro na mipangilio mibovu ya uratibu wa mahudhurio, unasababisha hoja za msingi kukosa michango ya maana.
"Hayo
ni matumizi mabaya ya fedha za umma, kwani wanalipwa mishahara na posho
zingine kutokana na fedha zetu na mbaya zaidi umeme na viyoyozi
vinatumika bila watu kuwepo Bungeni, hivyo Serikali inaingia gharama za
bure," alisema.
Nkya alitaka kila siku asubuhi uwekwe utaratibu wa kuwatangaza wabunge ambao hawapo na sababu zinazowafanya wasiwepo.
"Kama
wakipata wageni wanawatangaza; pia watumie utaratibu huo kuwatangazia
wananchi wabunge ambao hawapo bungeni," alisema Nkya.
Alisema
kufanya hivyo kutachochea uwajibikaji na ndio dhana ya utawala bora na
hali hiyo pia ndiyo ambayo ipo pia ofisi za Serikali.
Wanasiasa Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba aliitaka Ofisi ya Bunge kuliangalia kwa kina jambo hilo kwa sababu ni tatizo sugu ambalo siku za nyuma halikutazamwa kwa umakini na wabunge sasa wanaliona ni kawaida. Alisema wananchi wanapaswa kuhoji sababu za wawakilishi waliochaguliwa kutoonekana Bungeni. “Naiomba ofisi ya Bunge lilichukilie suala hili kwa umakini, kwani Serikali yetu imekuwa ikitumia fedha nyingi kuwalipa mishahara pamoja na posho lakini matokeo yake wabunge wetu hawahudhurii vikao,” alilalamika Proefsa Lipumba. Aliongeza: "Ndio hawa hawa katika vikaovilivyopita walikuwa wakipiga kelele ili Serikali iwaongezewe posho kwa maelezo wanazolipwa hazitoshelezi." Katibu Mkuu NCCR Naye Katibu Mkuu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Sam Ruhuza alilielezea tatizo la utoro Bungeni kuwa lilianza kuonekana dhahiri tangu Bunge lililopita la 2005 hadi 2010. "Kuna wabunge hata mwezi mzima hawaonekani na hata wapigakura wao hawajui aliko. Umefika wakati wa kuwekwa masharti ya kuwabana," alisema Ruhuza. Ndugai Kwa upande wake Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai amekiri wabunge wengi kushindwa kuhudhuria ipasavyo vikao vya Bunge kutokana na kushindwa kuendana na urefu wa ratiba na kuongeza kwamba, ratiba ya Bunge la Tanzania ni tofauti na ya nchi zingine za Jumuia ya Madola. “Ratiba yetu ni tofauti na ya nchi nyingine za Jumuia ya Madola kama ilivyo Kenya na Uganda. Wakati wenzetu wanahudhuria vikao vitatu kwa wiki Tanzania tunafanya vikao siku zote kuanzia asubuhi hadi usiku na siku ya Jumamosi,” alisema.
Ndugai alisema hali hiyo ambayo kwa wengine
inatafsiriwa kuwa ni utoro, inatokana na walio wengi kushindwa kuendana
na kasi ya ratiba hiyo ndefu.
Wakati akiahirisha Juzi, Ndugai
alisema wabunge wa mkoa wa Mtwara ambao waliambatana na Kamati ya
Nishati na Madini kwenda kushuhudia uzinduzi wa bomba la gesi kutoka
Mtwara hadi Dar es Salaam na wale wa Zanzibar walienda kwenye msiba wa
watu waliofariki katika ajali meli ya Skagit.
Naibu Spika huyo alongeza kuwa wabunge wengine ambao wanaunda Kamati ya Bunge katika msiba huo ambao walikuwa na kikao na Makamu wa Rais mjini Zanzibar na wale wa Kamati ya Ardhi, Masili na Mazingira walikwenda kwenye msiba wa mzazi wa Mbunge wa Londigo, Lekule Laizer. “Kwa mantiki hiyo, utaona kuwa walio wengi walitawanyika katika matukio tofauti hali ambayo imetafsiriwa kuwa ni utoro dhana ambayo sio sahihi,” aliwatetea. Alisema bajeti hiyo haikuweza kupitishwa kwa kuwa nusu ya idadi ya wabunge haikufikia kama kanuni inavyotaka. alisema asubuhi mahudhurio yalikuwa zaidi ya nusu lakini, mchana hali ikawa tofauti na Bungeni inataka wawe walau nusu ya wabunge wote. Alisema hiyo ndiyo sababu iliyolilazimisha bunge kuahirishwa hadi leo kukamilisha upitishaji wa bajeti hiyo ya kilimo na kuongeza, ipo haja ya kupitiwa upya kwa ratiba ya Bunge ili iwe kama za nchi nyingine za Jumuia ya Madola. Kukwama kwa Bajeti wiki iliyopita lilikuwa ni tukio la mara ya kwanza kutokana na uchache wa wabunge waliohudhuria kikao. Amri ya Makinda Kutokana na kukithiri kwa utoro bungeni, Spika wa Bunge Anne Makinda aliwahi kupiga marufuku wabunge na mawaziri kusafiri bila kibali maalumu.
Makinda
alitoa agizo hilo na kusema mbunge yeyote ambaye hatakuwepo bungeni
atapaswa kuomba ruhusa kwake na hata mawaziri kwake au kwa Waziri Mkuu,
Mizengo Pinda ama ofisi yake.
SOURCE http://www.mwananchi.co.tz/ |
No comments:
Post a Comment