Kikosi cha Yanga kilichoingia kilichoifunga Mafunzo ya zanzibar kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 5-3.
YANGA imefuzu kuingia Nusu Fainali ya Klabu Bingwa ya soka
Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, baada ya kuifunga Mafunzo ya
Zanzibar kwa penalti 5-4, kufuatia sare ya 1-1 ndani ya dakika 90 Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Wawakilishi wa Zanzibar Mafunzo walikuwa wa kwanza kupata bao
lililofungwa na Ali Othman Mmanga, dakika ya 34, akiunganisha kona ya Juma
Othman Mmanga na Yanga wakasawazisha dakika ya 46, mfungaji Said Bahanuzi ‘Spider
Man’.
Yanga sasa itamenyana na APR ya Rwanda, keshokutwa ambayo katika
Robo Fainali ya kwanza, imeitoa URA ya Uganda kwa kuifunga 2-1, mabao yake
yakifungwa na Jean Claude Iranzi dakika ya tisa na Suleiman Ndikumana dakika ya
34, wakati la Watoza Ushuru wa Kampala, lilifungwa na Robert Ssentongo dakika
ya 57.
Katika mchezo huo, Juma Othman Mmanga alipoteza fahamu na
kuwaweka roho juu wachezaji wenzake na mashabiki, akatolewa nje akipepewa na
hakuweza kuendelea na mchezo, lakini taarifa za baada ya mchezo zilisema anaendelea
vizuri.
Kipa wa Yanga Berko aliumia dakika ya 69 na akatibiwa kwa
dakika tatu, kabla ya kutolewa nje dakika ya 72, nafasi yake ikichukuliwa na
Ally Mustafa Barthez ambaye ukaaji wake mazuri langoni wakati wa penalti ulimfanya
Said Mussa Shaaban wa Mafunzo akapiga nje na kuipa Yanga ushindi.
Saidi Bahanuzi alipiga penalti ya kwanza, Nahodha Nadir
Haroub ‘Cannavaro’ ya pili, Hamisi Kiiza ya tatu, ya nne Haruna Niyonzima na
Athumani Iddi ‘Chuji’ alipiga ya mwisho na kuwainua maelfu ya mashabiki wa
Yanga Uwanja wa Taifa.
No comments:
Post a Comment