UTANGULIZI
1. Mheshimiwa Spika, tarehe
12 Juni, 2012 tulianza Kikao cha Kwanza cha Mkutano wa Nane wa Bunge
lako Tukufu na leo tunafikia tamati. Ni jambo la kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kutuwezesha kuhitimisha shughuli zote zilizopangwa kwa amani
na salama. Mkutano huu ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kuwasilisha,
kujadili na hatimaye kupitisha Bajeti ya Serikali ikiwa ni Makadirio ya
Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Wizara, Mikoa na Taasisi mbalimbali.
2. Mheshimiwa Spika, napenda
niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kutumia muda wote wa Mkutano huu
kwa ufanisi mkubwa kuchangia hoja zinazolenga katika kujenga na kusaidia
Taifa letu. Napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge
wote kwa mwamko huo mzuri ambao bila kujali itikadi za Vyama umetoa
changamoto kwa Serikali katika kutekeleza malengo tuliyojiwekea ili
kuleta maendeleo ya Nchi yetu. Ninawashukuru sana kwa michango yenu.
3. Mheshimiwa Spika, wakati
wa Mkutano huu tukiwa hapa Bungeni, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge
walipata Misiba kwa kupotelewa na Wapendwa wao wakiwemo Wazazi, Ndugu,
Jamaa na Marafiki. Nitumie nafasi hii kuwapa pole wote waliofikwa na
Misiba hiyo. Lakini kipekee kabisa niruhusu nimtaje na kumpa pole
Mheshimiwa Joseph Selasini, Mbunge wa Rombo kwa kumpoteza Mama yake
kutokana na ajali ambayo yeye mwenyewe alihusika na hivyo kupata
majeraha makubwa. Aidha, nimpe Pole kwa kumpoteza Baba yake akiwa bado
ana Majonzi ya kumpoteza Mama yake katika kipindi kifupi. Tunampa Pole Sana.
Pamoja na ajali aliyoipata Mheshimiwa Selasini, katika siku chache
zilizopita tumeshuhudia Ajali za Barabarani zilizosababisha vifo,
majeruhi kwa Abiria wa Magari hayo. Watu wengi wamepoteza maisha na
wengine kujeruhiwa. Niungane na Watanzania wote kuwapa pole waliopoteza
Ndugu, Jamaa na Marafiki katika Ajali hizo.
4. Mheshimiwa Spika, vilevile,
kama ambavyo wote tunakumbuka kuwa mnamo tarehe 18 Julai 2012 tulipata
taarifa ya tukio la kusikitisha kuhusu ajali ya kuzama kwa Meli ya MV
SKAGIT karibu na Kisiwa cha Chumbe, Zanzibar. Kwa mujibu wa taarifa
zilizopatikana, Meli hiyo ambayo inamilikiwa na Kampuni ya SEAGUL
Transport ilikuwa imebeba Watu 290, wakiwemo Watalii na Raia wa Kigeni 16. Katika ajali hiyo Watu 146 waliokolewa kwa msaada wa Vyombo vya uokoaji na waliobaki 144 wanahofiwa kupoteza Maisha wakiwemo Raia Wawili wa Kigeni.
5. Nitumie
fursa hii ya mwanzo kabisa kuwapa pole Watanzania wote kwa msiba huo
mkubwa ambao ulikumba Taifa letu. Aidha, kwa uzito wa kipekee nawapa
pole Ndugu, Jamaa na Marafiki ambao wamepoteza Wapendwa wao katika ajali
hiyo. Kwa wale wote waliopoteza maisha, tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu
ili azilaze Roho zao mahala Pema Peponi. Amina! Vilevile,
tunawaombea wote walionusurika katika ajali hiyo kuweza kurejea katika
afya zao za kawaida na hivyo kuendelea na ujenzi wa Taifa.
6. Aidha,
napenda kuwashukuru wote walioshiriki katika uokoaji wa ndugu zetu na
hivyo kuokoa maisha yao. Nami niungane na Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumpongeza Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Ali
Mohamed Shein na Viongozi wenzake wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
(SMZ) kwa kazi kubwa walioifanya kuongoza juhudi za uokoaji, huduma zote
walizozitoa kwa Majeruhi na Wafiwa. Vilevile, ninamshukuru Mheshimiwa
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wetu kwa kukubali mapendekezo ya
Baraza la Usalama la Taifa la kuunda Kikosi Maalum cha Uokoaji na
Usalama Majini, yaani Coastal Guards. Ni dhahiri kuwa Kikosi hiki kitakuwa na faida kubwa katika Usafiri wa Majini na Usalama wake.
7. Mheshimiwa Spika, matarajio
yetu ni kwamba Tume iliyoundwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
kuchunguza ajali hiyo itatuwezesha kujua mazingira yaliyosababisha
ajali hiyo na kwamba tufanye nini ili kuhakikisha Vyombo hivi
vinasimamiwa vizuri katika kuzuia ajali hizo zisitokee tena. Tayari
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua hatua za kuzuia matumizi ya
Meli za Kampuni hii ambazo hazitakidhi viwango vya usafirishaji Abiria.
Aidha, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeanza taratibu za kununua Meli
Mpya ambayo itabeba Abiria 1,000 na kubeba Magari Mia Moja.
Inatarajiwa kuwa Ujenzi wa Meli hiyo utachukua takriban Mwaka Mmoja
kuanzia sasa.
MJADALA WA BAJETI YA SERIKALI 2012/2013
8. Mheshimiwa Spika, mjadala
wa Bajeti ya Serikali tunaohitimisha leo, ulikuwa na hoja nyingi ambazo
Waheshimiwa Wabunge walitaka kupata majibu na ufafanuzi. Yapo maeneo
ambayo Waheshimiwa Mawaziri walijibu na kutoa maelezo ya ufafanuzi kwa
ukamilifu. Napenda kuwashukuru Waheshimiwa Mawaziri wote kwa kazi nzuri
waliyoifanya hadi kupitishwa kwa Bajeti za Wizara zao. Ninaelewa kwamba
zipo Hoja kadhaa zilizotolewa na Waheshimiwa Wabunge ambazo Mawaziri
hawakupata muda wa kuzijibu na kutoa ufafanuzi wa kina kwa sababu
ya muda finyu. Aidha, najua kwamba kila Waziri aliahidi kujibu kwa
Maandishi hoja ambazo hazikupata nafasi ya kujibiwa wakati wa Majumuisho
yake. Napenda nami nitumie muda huu wa kujumuisha Hoja hii siku ya leo
kwa kutoa maelezo japo kwa kifupi kwa baadhi ya maeneo.
MPANGO WA MAENDELEO NA BAJETI YA SERIKALI 2012/2013
9. Mheshimiwa Spika, Bajeti ya Serikali tuliyoipitisha kwa mwaka 2012/2013 ni jumla ya Shilingi Trilioni 15.12. Kati ya fedha hizo, Fedha za Matumizi ya Kawaida ni Shilingi Trilioni 10.59 na Fedha za Matumizi ya Maendeleo ni Shilingi Trilioni4.5. Aidha, kati ya Shilingi Trilioni 10.59 za Matumizi ya Kawaida, Shilingi Trilioni 2.75 ni za kulipa Deni la Taifa, Shilingi Trilioni 3.78 ni za malipo ya Mishahara na Shilingi Trilioni 4.06, sawa na Asilimia 26.8 tu ya Bajeti yote ni kwa Matumizi Mengineyo (Other Charges-OC).
Bajeti hii imeelekeza Rasilimali Fedha kidogo tulizo nazo katika maeneo
machache ya kipaumbele ambayo yatatuwezesha kufungulia fursa za Kukuza
Uchumi na Kupunguza Umaskini kwa kasi zaidi kwa kushirikiana na Sekta
Binafsi.
10. Kama mtakavyokumbuka, mwaka jana tarehe 8 Juni 2011 tukiwa hapa Dodoma, Mheshimiwa Rais alizindua Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016) wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo hadi 2025. Mwaka wa Kwanza wa utekelezaji wa Mpango huo, (yaani 2011/2012) ulikuwa wa Mpito (Transition)
kabla ya kuanza utekelezaji halisi wa Mipango inayofuata ya Miaka
Mitano Mitano ya kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa hadi 2025. Aidha,
Mheshimiwa Rais wakati wa uzinduzi alisisitiza kuwa, katika Mfumo wa
Upangaji Mipango, ni lazima Serikali ianze kuwekeza katika Vipaumbele vichache vitakavyoleta matokeo (impact) makubwa katika Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini.
11. Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa
Wabunge wengi walipata fursa ya kushiriki kwenye Uzinduzi wa Mpango huo
wa Miaka Mitano uliofanyika hapa Dodoma, St. Gaspar. Aidha, Serikali
ilipata fursa ya kuwasilisha Mpango huo Bungeni mwezi Juni 2011 katika
Mkutano wa Bunge la Bajeti ya mwaka 2011/2012. Wakati wa mjadala
Waheshimiwa Wabunge wengi pia walichangia mawazo na kutoa maoni yao
kwenye Mpango na Bajeti ya Serikali ya mwaka 2011/2012 ambayo Serikali imeanza kuyazingatia mwaka huu wa Bajeti ya 2012/2013.
12. Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kurejea Vipaumbele Vitano vilivyobainishwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kama ifuatavyo:
· Kipaumbele cha Kwanza ni kuwekeza kwenye Sekta za Miundombinu hasa uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya Nishati, Usafirishaji, Maji Safi na Maji Taka, Umwagiliaji na TEHAMA;
· Kipaumbele cha Pili ni kuwekeza katika Sekta ya Kilimo kwa
tafsiri pana ambayo inajumuisha Sekta ya Kilimo cha mazao ya chakula na
biashara pamoja na Sekta ya Mifugo, Uvuvi, Ufugaji wa Nyuki na
Rasilimali za Misitu. Shabaha Kuu ya kuendeleza Kilimo ni kuleta
Mapinduzi ya haraka ya Kilimo yatakayotuwezesha kuongeza uzalishaji na
tija ili kujitosheleza kwa chakula na kuuza ziada nje;
· Kipaumbele cha Tatu ni kukuza Maendeleo ya Viwanda,
hasa vile vinavyotumia malighafi zinazopatikana hapa Nchini ili
kuwezesha kusindika mazao ya Kilimo, Mifugo, Samaki, Misitu na Mazao ya
Ufugaji Nyuki, pamoja na kuongeza thamani ya Madini. Aidha, kuvutia
uwekezaji kwenye viwanda vikubwa vya mbolea, saruji na viwanda vya
kieletroniki kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya soko la ndani na kikanda
hasa Afrika Mashariki;
· Kipaumbele cha Nne ni Maendeleo ya Rasilimali Watu na ujuzi, hasa kukuza Sayansi, Teknolojia, Ubunifu na kuimarisha huduma za Jamii; na
· Kipaumbele cha Tano ni
kuendeleza huduma za Utalii, Biashara na Huduma za Fedha ambazo ni
muhimu katika kuchochea kasi ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya jamii.
13. Mheshimiwa Spika, Serikali inakubaliana na maoni na ushauri uliotolewa na Waheshimiwa Wabunge wengi na hasa Kamati ya Uchumi na Fedha kwambausimamizi
madhubuti wa utekelezaji wa Vipaumbele hivi na nidhamu ya matumizi ya
fedha zilizoelekezwa kwenye Vipaumbele vilivyowekwa, itakuwa ndiyo nguzo
kuu ya mafanikio ya Ukuaji wa Uchumi wetu, ikiwa ni pamoja na kushirikisha Sekta Binafsi na Wananchi wote kwa ujumla.
14. Mheshimiwa Spika, vilevile,
wakati wa mjadala wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2012/2013 baadhi ya
Waheshimiwa Wabunge walitoa maoni na ushauri wao kuhusu uwiano wa Bajeti
ya Serikali iliyowasilishwa ambayo imezingatia kutenga Asilimia 70 ya fedha za Bajeti kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Asilimia30 kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo, badala ya mgawanyo wenye uwiano wa Asilimia 65 kwa Asilimia 35 katika
matumizi hayo. Pamoja na maoni hayo, tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge
ambao walielewa vizuri maelezo ya ufafanuzi yaliyotolewa tarehe 22 Juni
2012 na Waziri wa Fedha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mahusiano na
Uratibu kuhusu Mgawanyo huo wa Bajeti. Kwa ujumla, mgawanyo huo
umezingatia hali halisi ya Mapato ya Serikali ikilinganishwa na mahitaji
makubwa ya fedha kwa ajili ya Mishahara ya Watumishi wa Serikali,
Mfuko Mkuu wa Serikali na Matumizi Mengineyo ambayo yanajumuisha
matumizi kwa ajili ya shughuli zisizoweza kuepukika.
15. Mheshimiwa Spika, matumizi
yasiyoweza kuepukika ni kama vile ununuzi wa Dawa na Vifaa vya Tiba;
gharama za uendeshaji wa Shule na Mitihani; uendeshaji wa Shughuli za
Bunge; Mahakama na Vyombo vya Ulinzi na Usalama pamoja na kutoa Ruzuku
ya Pembejeo za Kilimo. Matumizi hayo yametengewa jumla ya ShilingiBilioni 2,032.2, sawa na Asilimia 19.3 ya Matumizi Mengineyo (yaani Other Charges-OC) ya jumla ya Shilingi Trilioni 10.59. Kiasi kinachobakia cha fedha za Matumizi Mengineyo cha Shilingi Bilioni 1,959.5, sawa na Asilimia 18.6 ndicho
pekee kitatumika kwa ajili ya kugharamia shughuli zote za uendeshaji wa
Serikali nzima pamoja na kutekeleza kazi muhimu zinazoendelea kama
vile, kuendesha Zoezi la Sensa ya Watu na Makazi, Vitambulisho vya Taifa
na kukidhi mahitaji ya Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba Mpya na
shughuli nyingine kama hizo.
16. Aidha,
ni muhimu Waheshimiwa Wabunge kutambua kuwa sehemu ya fedha za
Maendeleo ya Rasilimali Watu na huduma za Jamii ambacho ni Kipaumbele
cha Nne cha Mpango wa Maendeleo ya Taifa zimewekwa pia katika Matumizi
ya Kawaida. Kiasi kilichotengwa katika Bajeti kwa ajili ya
matumizi hayo ni ShilingiBilioni 841.4. Fedha hizo zikijumuishwa na Shilingi Trilioni 4.5 zilizotengwa kwa ajili ya Mpango wa Maendeleo, zinafikia jumla ya Shilingi Trilioni 5.3, sawa na Asilimia35.5 ya Bajeti yote. Hivyo, uwiano halisi wa Bajeti iliyotengwa kwa Miradi ya Maendeleo ni Asilimia 35.5. Serikali
itajitahidi kuzingatia ushauri wa kutenga Bajeti kubwa kwa ajili ya
Miradi ya Maendeleo kwa kadri Mapato ya Serikali yanavyoongezeka na
kubana matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima.
17. Mheshimiwa Spika, Serikali
imejipanga vizuri kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa
Mwaka 2012/2013. Serikali itafanya ukaguzi na ufuatiliaji wa karibu wa
Miradi ya Maendeleo na tathmini ya mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa
kazi zinazofanyika zinawiana na thamani ya fedha zinazotolewa (Value for Money)
kwa Miradi ya Maendeleo. Aidha, Tume ya Mipango imepewa jukumu la
kuchambua Mipango Kazi ya Miradi ya Maendeleo na kushauri ipasavyo.
18. Mheshimiwa Spika, Serikali
imedhamiria kuhakikisha kwamba malengo ya ukusanyaji Mapato na Matumizi
ya Fedha za Serikali yanazingatia Bajeti iliyoidhishwa na Bunge. Ili
kutekeleza azma hiyo, Serikali imekubali kuwa kila baada ya robo ya
mwaka, Baraza la Mawaziri la Kazi litakutana na kujadili mwenendo
wa ukusanyaji wa Mapato ya Serikali (ya Kodi na yasiyo ya Kodi) pamoja
na matumizi ya Serikali katika kipindi hicho. Baraza hilo litajadili
Mapato na Matumizi ya kila Wizara, kila Mkoa pamoja na Wakala na Idara
za Serikali zinazojitegemea na Taasisi zote za Serikali.
19. Mheshimiwa Spika, natoa
wito kwa Watendaji wote wa Serikali katika ngazi zote kuwa na nidhamu
katika matumizi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Matumizi ya
Serikali pamoja na kuwajibika ipasavyo katika matumizi ya Bajeti
tuliyoipitisha.
KUIMARISHA UTENDAJI SERIKALINI NA KUDHIBITI MATUMIZI
20. Mheshimiwa Spika, Serikali
imedhamiria kuimarisha Utendaji kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na
Taratibu zinazoongoza Utendaji wa Watumishi wa Serikalini. Ili
kutekeleza azma hii kikamilifu, Serikali itatumia uzoefu wa Nchi ya
Malaysia ambayo imefanikiwa kuweka mfumo madhubuti wa kupima ufanisi wa
Utendaji Kazi wa Viongozi na Watendaji wake kwa kutumia Chombo maalum
kinachojulikana kwa jina la PEMANDU. Hatua hiyo, itawezesha Serikali
kuimarisha utoaji wa huduma nzuri kwa Wananchi pamoja na kuimarisha
usimamizi wa matumizi ya fedha za Serikali ikijumuisha Mipango ya
Maendeleo.
21. Mheshimiwa Spika, napenda
kusisitiza kwamba, Utendaji Kazi mzuri ni pamoja na matumizi bora ya
rasilimali chache tulizonazo, kutoa huduma inayotarajiwa na Watanzania.
Sote tunaelewa kwamba, mahitaji ya fedha ni makubwa sana kulinganisha
na uwezo wetu wa sasa. Hata hivyo, kila mmoja wetu akiwajibika
ipasavyo na kutumia kwa uangalifu rasilimali hizo bado tunaweza
kufanya mambo makubwa sana. Ni kwa sababu hiyo Serikali imeendelea
kusisitiza kwamba Bajeti tuliyoipitisha hapa inalenga matumizi
yatakayotupatia matokeo makubwa na ya haraka. Tutaendelea kubana
matumizi yasiyo na tija kama vile Warsha, Semina na Makongamano, Safari
zisizo na lazima Ndani na Nje ya Nchi, ununuzi na matumizi ya magari ya
kifahari pamoja na matumizi mengine yasiyo ya lazima.
MAANDALIZI YA MSIMU WA KILIMO 2012/2013 NA UPATIKANAJI WA PEMBEJEO NA ZANA ZA KILIMO
Mbolea
Mheshimiwa Spika, moja
ya maeneo ambayo yalikuwa na hoja nyingi katika Mjadala wa Bunge hili
la Bajeti ni suala la Kilimo, hususan maandalizi ya Msimu wa Kilimo,
upatikanaji wa Pembejeo na Zana za Kilimo. Programu
ya kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP) inalenga kuleta mageuzi ya Sekta
ya Kilimo, mkazo wake mkuu ni pamoja na kuongeza upatikanaji wa
pembejeo na Zana za Kilimo. Napenda kuwahakikishia Watanzania kwamba,
katika msimu wa Kilimo 2012/2013, Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya
mbolea na mbegu kwa mazao mbalimbali kwa utaratibu wa Vocha. Lengo ni
kuongeza upatikanaji wa pembejeo na uelewa wa Wakulima kuhusu matumizi
ya mbolea na mbegu bora. Kwenye maeneo ya Nchi yenye ukame, ambayo
imethibitishwa na Wataalam kwamba matumizi ya Mbolea ya Minjingu Mazao (NPS)
inafaa kwa uzalishaji wa Mazao ya Alizeti na Mtama, Vocha za Ruzuku
zitatolewa kwa ajili ya mazao hayo. Lengo ni kubadilisha mtazamo hasi
kuwa mazao haya hayahitaji mbolea pamoja na kuwapunguzia Wakulima
gharama kwa sababu bei ya mbolea ya Minjingu Mazao (NPS) ni nafuu
ikilinganishwa na mbolea ya DAP. Vilevile, lengo lingine la Serikali ni
kuongeza uzalishaji wa mazao hayo ili kupunguza uagizaji wa Mafuta ya
Kula kutoka nje pamoja na kukabiliana na upungufu wa chakula katika
maeneo hayo. Kwa hiyo, nawasihi Wakulima kutumia Mbolea ya Minjingu
Mazao (NPS) kwa sababu bei yake ni nafuu, inatengenezwa hapa Nchini na pia ni rafiki wa mazingira.
Mbegu
22. Mheshimiwa Spika, mahitaji ya mbegu kwa mwaka ni Tani 60,000, lakini mwaka 2011/2012 Tani 28,770 tu
zilizalishwa kutoka katika mashamba ya Wakala wa Mbegu wa Taifa,
Mashamba ya Magereza na JKT na Sekta Binafsi. Ili kupunguza tatizo
hili, Sekta Binafsi imeruhusiwa kupata Mbegu Mama (Breeder Seeds) kutoka Vituo vya Utafiti ili wazalishe Mbegu za Msingi (Foundation Seeds) zitakazotumika kuzalisha Mbegu zilizothibitishwa (Certified Seeds).
Serikali itahakikisha kwamba Mbegu bora zinapatikana kwa wakati ili
ziweze kuwafikia Wakulima kabla ya kuanza kwa Msimu wa Kilimo.
Zana za Kilimo
23. Mheshimiwa Spika, Hotuba
ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ilielezea kwa kina
jitihada za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya Zana Bora za Kilimo
ili kuongeza tija na kupunguza Sulubu ya kazi za kutumia Jembe la Mkono.
Matumizi ya Matrekta Makubwa na Madogo yaliyoingizwa Nchini na SUMA JKT
yameongezeka na hivyo kuongeza eneo linalolimwa kutoka Asilimia 12
mwaka 2010 hadi Asilimia 14 mwaka 2011. Nitumie nafasi hii kuwahimiza
Wananchi kwamba Matrekta ya SUMA JKT aina ya Farmtrac 2; Wheel Driveyapatayo 547 bado yapo. Ninazo taarifa kwamba Matrekta ya New Holland naFarmtrac 4 Wheel Drive yameisha,
lakini bado mahitaji ni makubwa. Serikali inafanya Mpango wa kuagiza
Matrekta hayo na tayari kuna Mpango wa kupata Mkopo wa Matrekta 3,000
kupitia Makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Serikali ya India.
Aidha, bei za Matrekta ya SUMA JKT zimepunguzwa na muda wa marejesho ya
Mkopo wa Matrekta hayo kwa Wananchi umeongezwa. Nawasihi Wananchi
kujiunga katika Vikundi vya kuwawezesha kukopa Matrekta hayo.
24. Mheshimiwa Spika, ni
hivi karibuni tu nilifanya Uzinduzi wa Matrekta 50 ili yakopeshwe kwa
Wakulima wa Mkoa wa Ruvuma. Alichokifanya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ni
kuchukua jukumu la kuratibu zoezi zima la ukopeshaji wa Matrekta hayo
kwa Wakulima katika Mkoa wake. Yeye akawa kama Focal Person wa
kukusanya fedha zinazohitajika na kuhakikisha upatikanaji wa Matrekta
hayo kwa Wakulima wake. Nitumie mfano huu mzuri kuwaomba Viongozi wote
katika ngazi za Mikoa na Wilaya kuweka nguvu za ziada wasaidie katika
kufanikisha upatikanaji wa Matrekta hayo katika maeneo yao. Halmashauri
zijipange kuhakikisha kwamba fursa iliyotolewa ya kupunguza bei ya
Matrekta ya SUMA JKT na fursa ya Asilimia 10 ya malipo ya awali
inatumika vizuri. Kipaumbele kiwe kwenye SACCOS, hasa za Vijana.
Hali ya Chakula Nchini
25. Mheshimiwa Spika, hali
ya chakula Nchini ni ya kuridhisha. Takwimu za tathmini ya awali za
mwezi Juni 2012 kuhusu hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula na utabiri
wa hali ya chakula kwa 2012/2013 zinaonesha kuwa uzalishaji wa mazao ya
chakula utafikia Tani 13,572,804 ikilinganishwa na mahitaji ya chakula yanayokadiriwa kuwa Tani Milioni 11.99. Taifa linatarajia kujitosheleza kwa chakula kwa Asilimia 113 na hivyo kuwa na ziada ya Tani Milioni 1.58. Matarajio
ni kwamba kwa maeneo yenye kuonesha upungufu wa chakula utaratibu
utafanywa wa kupata mahindi toka katika Hifadhi ya Taifa ya Chakula
(NFRA).
26. Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyo ya kuridhisha, tathmini ya mwezi Juni 2012 inaonesha kuwa bado kutakuwepo na uhaba wa chakula katika MikoaSita (6) ya
Arusha, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Manyara, Shinyanga na Tabora.
Kutokana na hali hiyo, katika mwaka 2012/2013 Serikali itawezesha
Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kununua Tani 200,000 za nafaka kutoka kwa Wakulima wa Mikoa iliyozalisha ziada ya Iringa, Mbeya, Rukwa na Ruvuma. Aidha, Serikali itahamisha Tani 100,000 za
akiba ya Nafaka iliyopo katika Maghala yenye ziada ya chakula kwenda
kwenye Maghala ya Mikoa yenye upungufu wa chakula. Zoezi la kuhamisha
Mahindi hayo kwenda Dar es Salaam limeanza. Hatua hii pia itatoa nafasi
ya kuhifadhi nafaka zitakazonunuliwa Msimu wa Ununuzi wa 2012/2013.
Bajeti ya Kilimo kuwa Asilimia 10
27. Mheshimiwa Spika, katika
Mkutano wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU) uliofanyika Maputo, Msumbiji
mwezi Julai 2003, moja ya makubaliano ya Kikao hicho ni agizo la Nchi
zote za Umoja huo kuhakikisha kuwa Bajeti zao za Kilimo zinafikia
Asilimia 10 ya Bajeti ya Taifa baada ya kipindi cha miaka Mitano.
Napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, makubaliano hayo
tunayatekeleza kwa kadri ya uwezo wetu na fedha zinazotengwa kwa ajili
ya Kilimo zimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 233.3 mwaka 2005/2006, sawa na Asilimia 5.6 hadi kufikia Shilingi Bilioni 926.2 mwaka 2011/2012, sawa na Asilimia 8. Katika mwaka huu wa fedha 2012/2013, fedha zilizotengwa ni Shilingi Bilioni 1,103.6, sawa na Asilimia 9.0. Ni matumaini yangu kwamba kwa mwelekeo huu tutaweza kufikia Asilimia 10 kama tulivyokubaliana katika Nchi za Umoja wa Afrika muda wowote kuanzia mwaka ujao wa fedha.
MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI
Kuboresha Ufugaji wa Kuku ili Kuondoa Umaskini
28. Mheshimiwa Spika, ufugaji
wa Kuku wa Asili unayo nafasi kubwa ya kukuza uchumi wa Wananchi
waishio Vijijini, kuboresha lishe na kipato chao. Takwimu zinaonesha
kuwa Ufugaji wa Kuku wa Asili huchangia Asilimia 94 ya Kuku wote Nchini. Aidha, unachangia Asilimia 80 ya nyama na mayai yanayoliwa Vijijini na Asilimia 20 ya
Mijini. Hata hivyo, Sekta hii bado inakabiliwa na changamoto nyingi
hususan, vifo vya Kuku vinavyosababishwa na magonjwa hasa ya mdondo (Newcastle Disease).
Changamoto nyingine ni uhaba wa Maafisa Ugani, ukosefu wa taarifa za
masoko na ukosefu wa mitaji ya kuanzisha Miradi endelevu ya Ufugaji
Kuku.
29. Serikali
imekuwa na mikakati mbalimbali ya kuboresha ufugaji wa Kuku wa Asili
ikiwa ni pamoja na kutengenezwa kwa Chanjo ya Kupunguza Vifo vya Kuku
kutokana na Ugonjwa wa Mdondo. Chanjo ya kuzuia Mdondo wa Kuku (Newcastle Disease Vaccine)
iligunduliwa Nchini Australia na kufanyiwa majaribio hapa Nchini.
Serikali inaagiza mbegu kutoka Australia na kutumia teknolojia hiyo
kutengeneza Chanjo hiyo hapa Nchini kupitia Maabara Kuu ya Temeke.
Chanjo hii imefanya vizuri sana na katika baadhi ya Vijiji katika Mkoa
wa Singida na imepunguza vifo dhidi ya Mdondo wa Kuku kwa Asilimia 96
hadi Asilimia 100.
30. Mheshimiwa Spika, Shirika la Research Into Use (RIU)
linaloongozwa na Timu ya Wataalam ambao ni Vijana wetu waliosoma Chuo
Kikuu cha Sokoine, Morogoro wameanzisha Mradi wa Kuendeleza Kuku wa
Asili. Mradi huu ulizinduliwa Mwezi Machi mwaka huu 2012. Mradi wa RIU,
umeonesha kuwa Kuku wa Asili wanaweza kufugwa kibiashara. Mradi huo
ambao unatekelezwa katika Mikoa ya Singida, Dodoma, Morogoro na Pwani
umewezesha Wafugaji wa Kuku wa Asili wapatao 3,500 kuongeza idadi ya Kuku wanaofugwa katika Kaya kutoka 5hadi 10 na kufikia kati ya 100 hadi 300.
Mafanikio haya yametokana na Wafugaji kuwezeshwa kupata mafunzo,
mitaji, masoko na kuwaunganisha na Wadau wengine hususan wauzaji wa Dawa
za Tiba ya Kuku.
31. Kutokana
na mafanikio yaliyoonekana katika Mradi huo, Serikali itaendelea
kuwasaidia Wananchi na Wafugaji wa Kuku hapa Nchini kuendeleza Ufugaji
wa Kuku wa Asili ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo na kuajiri Maafisa
Ugani wa kutosha wa Kuku Asili. Vilevile, Serikali itahimiza Mpango wa
kuanzisha Mashamba Darasa ya Ufugaji Bora wa Kuku ambao utawezesha
kutoa elimu kwa Wafugaji wengi zaidi. Natoa wito kwa Halmashauri
za Wilaya kutoa kipaumbele katika kuhamasisha Wananchi kuanza Ufugaji wa
Kuku wa Asili ambao umeonesha kuwa na mafanikio na manufaa makubwa ya
kuondoa umaskini.
Maendeleo ya Ufugaji Nyuki
32. Mheshimiwa Spika, kama
ambavyo mtakumbuka katika Mikutano kadhaa ndani ya Bunge lako Tukufu
nimekuwa nikisisitiza fursa ya kipekee tuliyonayo ya kufanya Ufugaji
Nyuki ambao una faida kubwa kiuchumi na katika kuondoa umaskini.
Gharama za Ufugaji Nyuki ni nafuu sana ikilinganishwa na aina
nyingine yoyote ya Ufugaji. Kutokana na ukweli huo Wananchi wameanza
kuhamasika katika maeneo mengi Nchini kuhusu Ufugaji Nyuki. Aidha,
Wawekezaji wameanza kuwekeza baada ya kujiridhisha kwamba Ufugaji wa
Nyuki katika Nchi yetu una faida na manufaa makubwa.
33. Mheshimiwa Spika, mwanzoni
mwa mwezi Juni 2012 niliweza kufungua Kiwanda kipya cha kisasa cha
kuchakata Asali pale Visiga, Kibaha. Kiwanda hicho kina uwezo wa
kuchakata Tani 10,000 za Asali kwa mwaka. Aidha, vipo pia
Viwanda vingine Saba (7) Nchini. Takwimu za mwaka 2011/2012 zinaonesha
Uzalishaji wa Asali ulifikia Tani 9,000 zenye thamani ya Shilingi Bilioni 27 na Nta Tani 600 zenye thamani ya Shilingi Bilioni tatu (3).
Hii ni ishara nzuri ya kwamba Soko la Asali lipo na Asali ni zao muhimu
la kuongeza Kipato cha Wananchi. Napenda kutumia nafasi hii tena
kuwahimiza Wananchi kutumia fursa hii kwa kuzalisha mazao ya Nyuki kwa
wingi, kwani Soko la Asali na Nta lipo tayari.
UPATIKANAJI WA MAJI NCHINI
34. Mheshimiwa Spika, wakati
wa mjadala wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji, Waheshimiwa Wabunge
wengi walionesha kutoridhishwa na hali ya upatikanaji wa Maji katika
maeneo mbalimbali Nchini. Maeneo mengi ya Nchini yameendelea kuwa na
uhaba wa maji kutokana na uharibifu wa vyanzo vya maji, ongezeko la
watu, ukame unaotokana na athari za mabadiliko ya Tabianchi na
matumizi ya maji yasiyozingatia tija na ufanisi. Aidha, tatizo la
Maji limechangiwa na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi na kijamii
zisizowiana na uwekezaji katika miundombinu ya maji.
35. Mheshimiwa Spika, katika
kukabiliana na Tatizo la Maji Nchini, Serikali inatekeleza Miradi
mbalimbali kwa kutumia fedha za ndani na fedha za nje kupitia kwa
Wafadhili na Wadau wa Maendeleo. Iko Miradi ya Maji inayoendelea
kutekelezwa katika Halmalshauri mbalimbali Nchini kwenye Mikoa ya
Arusha, Dar es Salaam, Lindi, Kagera, Katavi, Kigoma na Kilimanjaro.
Miradi hiyo iko pia katika Mikoa ya Manyara, Mtwara, Mwanza, Shinyanga
na Tabora.
36. Mheshimiwa Spika, niruhusu
nitumie muda mfupi kuelezea Miradi michache inayotekelezwa na Serikali
kama njia ya kukabiliana na tatizo hili. Kwa mfano, tarehe 21 Julai 2012
Serikali ya Tanzania imesaini Mkataba na Umoja wa Nchi za Ulaya wenye
thamani ya Euro Milioni 51.51 kwa ajili ya Miradi ya Majisafi na
Mazingira katika Mikoa ya Lindi, Kigoma, Babati, Mtwara na Rukwa. Aidha,
Serikali ya Ujerumani imetenga Euro Milioni 20 kwa ajili ya
Mikoa ya Lindi, Kigoma na Rukwa. Majadiliano ya kusaini Mkataba huu na
Wafadhili yanaendelea. Halmashauri zimeendelea kutekeleza Miradi ya Maji
katika Vijiji 10 ambapo hadi Julai 2012, Halmashauri 67 zimepata
vibali vya kuanza Ujenzi wa Miundombinu ya Maji. Miradi hii
inafadhiliwa chini ya Programu ya Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini
inayotekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na Benki ya Dunia, Benki ya
Maendeleo ya Afrika, Benki ya Kiarabu, Serikali za Uholanzi, Ufaransa,
Korea Kusini na Ubelgiji. Tayari fedha zimekwishatolewa kwa ajili ya
Vijiji ambapo utekelezaji utafanyika kufikia Wastani wa Vijiji Vitano (5) kwa kila Halmashauri.
37. Mheshimiwa Spika, katika
Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria, Serikali
ililenga kufikisha maji katika Miji ya Kahama na Shinyanga pamoja na
Vijiji vyote vilivyopo kandokando ya Bomba Kuu la kusafirishia Maji
umbali usiozidi Km 5. Jumla ya Vijiji 54 vilihusika na kati ya hivyo 39 vilianza
kupata huduma ya maji tangu uendeshaji wa Mradi ulipoanza mwezi
Februari 2009. Vijiji hivyo vyote vipo katika Mikoa ya Shinyanga na
Mwanza. Katika Awamu ya Pili ya Mradi, Vijiji vyote vilivyopo umbali wa Km 12 kutoka
kwenye Bomba Kuu katika Wilaya za Misungwi, Kwimba, Shinyanga na Kahama
vitaunganishwa, Vijiji hivyo tayari vimetambuliwa. Tayari Serikali
imepeleka kiasi cha Shilingi Milioni 304.5katika Mradi huu.
38. Mheshimiwa Spika, Mradi
wa ujenzi wa Bwawa la Kawa, katika Wilaya ya Nkasi unaendelea
kukamilishwa. Mradi huu unahusu Usanifu wa miundombinu ya usambazaji
maji kutoka kwenye Bwawa la Kawa kwenda kwenye Vijiji vya Nkundi,
Fyengerezya na Kalundi. Uandaaji wa Makabrasha ya Zabuni kwa ajili ya
kupata Mkandarasi wa kujenga miundombinu ya maji umeanza na ujenzi
utaanza mara baada ya kupata Mkandarasi. Kiasi cha Shilingi Milioni 300 kimetengwa katika mwaka 2012/2013 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kusambaza maji.
39. Mheshimiwa Spika, kuanzia mwaka 2007/2008 hadi 2011/2012, Serikali ilifanya maamuzi ya kutumia Shilingi Milioni 95.9 kwa
ajili ya ukarabati wa Bwawa la Mfili na Bomba Kuu la kutoka Mfili hadi
kwenye matanki pamoja na upanuzi wa Mtandao wa Maji Safi kwa Mji wa
Namanyere. Mwaka 2012/2013 Serikali imetenga Shilingi Bilioni 2.1 ili kutekeleza hatua za dharura kuupatia Mji huo maji kwa kuboresha huduma ya maji. Aidha, tarehe
23 Septemba 2011 Serikali ilisaini Mkataba na BADEA kwa ajili ya
utekelezaji wa Mradi wa Majisafi kwa Mji wa Orkesumet katika Wilaya ya
Simanjiro. Hadi sasa, majina ya Wahandisi Washauri watakaofanya mapitio
ya usanifu na kusimamia ujenzi yamepitishwa na Wizara; na BADEA
imekwisha idhinisha majina hayo kwa hatua zaidi. Mtaalamu Mshauri
anatarajiwa kuanza kazi mwaka 2012/2013.
40. Mheshimiwa Spika, ni
hivi karibuni tu tarehe 22 Julai 2012 Mheshimiwa Rais, Dkt. Jakaya
Mrisho Kikwete alizindua Mradi Mkubwa wa Maji Safi katika Jiji la Mbeya
uliotekelezwa chini ya Programu ya Regional Centres uliofadhiliwa
na Mfuko wa pamoja wa Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, Jumuiya
ya Ulaya, na Serikali ya Ujerumani. Kukamilika kwa Mradi huu ambao
uligharimu takriban Shilingi Bilioni 80 umeongeza huduma za Maji kutoka Mita za Ujazo 32,000 kwa siku hadi Mita za Ujazo 49,000 kwa siku kwa Wakazi wa Jiji la Mbeya. Lengo ni kufikia Mahitaji ya Jiji hili kwa Asilimia 100 ifikapo mwaka 2017.
41. Mheshimiwa Spika, napenda
nitumie fursa hii kuwaahidi Waheshimiwa Wabunge na Wananchi kwa ujumla
kwamba Miradi yote ambayo ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji
Nchini itaendelea kupewa Kipaumbele na Serikali inayoongozwa na Chama
Cha Mapinduzi hadi yote ikamilike.
Mradi wa Maji wa Ntomoko Wilayani Kondoa
42. Mheshimiwa Spika, mnamo
tarehe 12 Agosti, 2012 nilipata fursa ya kutembelea mradi wa maji wa
Ntomoko uliopo Wilayani Kondoa. Mradi huu ulibuniwa na Serikali
chini ya Uongozi wa Hayati Baba wa Taifa, Mwl. Julius K. Nyerere ili
kutoa huduma kwa watu wapatao 23,400 katika Vijiji 17 vilivyoko katika Uwanda kame wa Goima (The Goima Difficult Zone)
ambao una tatizo kubwa la kupata maji. Vijiji hivyo haviwezi kupata
maji kupitia visima virefu kutokana na asili ya Tabaka la miamba
iliyopo katika Ukanda huo.
43. Mheshimiwa Spika, Changamoto
kubwa zilizopo katika mradi huo, ni pamoja na uchakavu wa Miundombinu
na huduma ya maji na ongezeko la mahitaji ya maji linatokana na ongezeko
kubwa la Watu ambalo sasa linafikia watu wapatao55,397. Chanzo cha Maji katika Mradi huu ni Chemchem ya Ntomoko ambayo ina uwezo wa kuzalisha maji wastani wa lita 689,000 kwa siku. Hata hivyo, kwa sasa mahitaji halisi ya Maji katika Vijiji 17 ni Lita za Ujazo zipatazo 1,464,000 siku. Uchakavu wa Miundombinu ya Mradi umesababisha Vijiji vinavyopata maji kupungua kutoka 17 mwaka 1973 hadi Vijiji Vitano (5) kwa sasa.
44. Mheshimiwa Spika, ili kuondoa changamoto mbalimbali za Mradi huu, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Serikali itaongeza kiasi cha Shilingi Bilioni 2.3katika Fedha iliyotengwa kwa Mradi huo na Halmashauri za Wilaya ya Kondoa na Chemba ambazo zimetenga Shilingi Milioni 90. Lengo
ni kuhakikisha kuwa Mradi huo unafufuliwa na kurudisha huduma ya maji
kwa Wananchi. Aidha, Serikali itaendelea na Juhudi za kufufua Miradi ya
namna hii ya maji ili kuhakikisha kuwa Wananchi wanapata huduma ya
maji. Aidha, katika kuhakikisha kuwa chanzo hiki kinalindwa,
niliwaelekeza Viongozi wa Wilaya ya Kondoa na Mkoa wa Dodoma kuhakikisha
kuwa Wanakijiji cha Mafai ambako ndiko iliko Chemchem ya Ntomoko,
wanapata maji kutoka kwenye Chanzo hicho.
USAFIRI WA BARABARA NA KUKABILIANA NA MSONGAMANO WA MAGARI MIJINI
45. Mheshimiwa Spika, wakati
wa kujadili Bajeti za Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Ujenzi na Wizara
ya Uchukuzi, masuala mengi yaliyojitokeza katika mijadala hiyo yalihusu
namna ya kukabiliana na changamoto zinazoikabili Sekta Ndogo ya Usafiri
wa Barabara. Changamoto hizo ni pamoja na kutounganika kwa Mtandao wa
Barabara na maeneo ya uzalishaji Vijijini pamoja na masoko, msongamano
wa magari Mijini na mpangilio usio mzuri wa Miji yetu, uhaba wa fedha za
ujenzi, ukarabati na matengenezo ya barabara, uchakavu na uchache wa
mitaro ya kuondoa maji ya mvua katika barabara zetu, uhaba wa Watalam na
uwezo mdogo wa Makandarasi wa barabara na mfumo dhaifu wa kitaasisi wa
kuhudumia barabara za Wilaya na Vijiji.
46. Mheshimiwa Spika, vilevile,
wakati wa kuhitimisha Hoja za Bajeti kuhusu Sekta Ndogo ya Usafiri wa
Barabara, Mawaziri wa Sekta hizo walieleza mikakati ya kupunguza
changamoto hizo kwa Awamu kwa kuanzia na Bajeti ya mwaka 2012/2013.
Barabara zilizopewa kipaumbele katika Bajeti hizo ni zile zenye kufungua
fursa za kiuchumi katika maeneo ya uzalishaji, kupunguza msongamano
katika Miji hasa Jiji la Dar es Salaam, kuunganisha Nchi yetu na
Nchi jirani na kuendelea kutekeleza Programu kuhusu Uwekezaji katika
Miundombinu ya Uchukuzi kwa mwaka 2007 hadi 2017. Katika Programu hii, Miradi 16 ya
ujenzi wa barabara kuu za lami iliyoanza kutekelezwa na Serikali ya
Awamu ya Tatu na kuendelea kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Nne,
ilikamilika kwa nyakati tofauti kati ya mwaka 2005 na 2010. Barabara
zilizokamilika katika kipindi hicho zina urefu wa jumla ya Kilometa 1,236.
47. Mheshimiwa Spika, kati ya mwaka 2005 hadi 2012, Serikali ya Awamu ya Nne ilianzisha Miradi Mipya 78 ya Ujenzi na Ukarabati wa Barabara zenye urefu wa jumla ya Kilometa 4,176. Kati ya Miradi hiyo, Miradi 17 yenye urefu wa jumla ya Kilometa 662.2 imekamilika kwa Asilimia 100 kufikia mwezi Juni 2012 na mingine 61 ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Sambamba na ujenzi unaoendelea katika Miradi hiyo, kuna Miradi mingine 43 iliyobuniwa katika Awamu ya Nne yenye urefu wa jumla ya Kilometa 5,739 ambayo inaandaliwa kwa ajili ya kuanza ujenzi. Kati ya Miradi hiyo, Miradi 16 yenye urefu wa jumla ya Kilometa 3,817,
ipo katika hatua mbalimbali za kukamilishwa Usanifu, na Miradi 27 yenye
urefu wa jumla ya Kilometa 1,921 usanifu wake umekamilika na
inatafutiwa Makandarasi. Lengo ni kuunganisha kwa awamu Miji Mikuu ya
Mikoa yote Nchini kwa barabara za lami ifikapo mwaka 2017/2018.
Kuondoa Msongamano wa Magari katika Jiji la Dar es Salaam
48. Mheshimiwa Spika, tatizo
la msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam linaathiri
Wananchi wengi. Waheshimiwa Wabunge wengi, hasa wale wa Mkoa wa Dar es
Salaam walielezea kwa uchungu tatizo hili. Serikali kupitia Wizara
husika imeeleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa ili kukabiliana na
Msongamano kuwa ni pamoja na kuanzisha Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka,
ujenzi wa Barabara za Mzunguko (ring roads), Barabara za Mlisho (feeder roads), Barabara za Juu (flyovers) na kuanzisha huduma za Usafiri wa Reli na vivuko Jijini Dar es Salaam.
Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART)
49. Mheshimiwa Spika, Serikali
inatekeleza Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART). Lengo
ni kuliwezesha Jiji la Dar es Salaam kuwa na Mtandao wa Usafiri wa
Mabasi makubwa yatakayopita katika njia Maalum na hivyo kuwahakikishia
Wananchi huduma bora za usafiri Jijini. Mradi huo pia utasaidia
kupunguza msongamano unaotokana na wingi wa mabasi madogo ya Daladala
katika barabara za Jiji.
50. Mheshimiwa Spika,
Bajeti ya Mwaka 2012/2013 itatumika zaidi katika utekelezaji wa Miradi
ya Awamu ya Kwanza na kuanza maandalizi ya Miradi itakayotekelezwa
katika Awamu ya Pili na ya Tatu. Awamu ya Kwanza ina Miradi Saba (7)
ambayo Mikataba ya Ujenzi ilisainiwa katika vipindi tofauti kuanzia
mwezi Mei 2010 hadi mwezi Machi 2012. Miradi yote hii itakamilika katika
vipindi tofauti, kuanzia mwaka 2012 hadi 2015.
Ujenzi wa Barabara Mbalimbali, Madaraja na Barabara za Juu (flyovers)
51. Mheshimiwa Spika, pamoja
na Mradi wa Mabasi yaendayo Kasi, katika Bajeti Wizara ya ujenzi ya
mwaka 2012/2013, Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS) unatekeleza
Miradi 14 itakayogharimu Shilingi Bilioni 580 kwa ajili ya
ujenzi wa barabara zitakazopunguza msongamano wa magari katika Jiji la
Dar es Salaam. Miradi hiyo inahusu ujenzi wa Barabara Kuu za njia nne,
Barabara za Mzunguko (ring roads), Barabara za Mlisho (feeder roads) barabara ya kupita juu (flyover)
kwenye Makutano ya TAZARA, Daraja la Kigamboni na Gati za Vivuko.
Miradi hii itakapokamilika itatoa mchango mkubwa katika kupunguza
msongamano uliopo hivi sasa.
Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania
52. Mheshimiwa Spika, tarehe 29 Julai 2012 nilikagua utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu na Utoaji wa Huduma za Jamii (Tanzania Strategic Cities Project)
unaotekelezwa na Mamlaka ya Uendelezaji Makao Makuu (CDA) na
Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma. Mradi huu unatekelezwa pia katika
Halmashauri nyingine saba Nchini kwa ufadhili wa Benki ya Dunia na Serikali ya Denmark.
53. Mheshimiwa Spika, katika
ziara hiyo nilibaini kwamba ili Miradi hii itekelezwe kwa kasi
iliyokusudiwa, kuna umuhimu mkubwa kwa Wadau wanaoguswa na utekelezaji
wakiwemo TANESCO na Mamlaka za Maji, kukutana mara kwa mara ili kuondoa
vikwazo mbalimbali vinavyoathiri utekelezaji wa Mradi. Halmashauri
nyingine ambako Mradi huu unatekelezwa ni Majiji ya Mwanza, Tanga na
Mbeya na Arusha na Manispaa za Kigoma Ujiji na Mtwara Mikindani.
Kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa
Kilometa 141, ujenzi wa Madampo ya Taka Ngumu, Vituo vya Mabasi
na Mitaro ya Maji Machafu. Mradi huu pia unajumuisha kipengele cha
kujenga uwezo wa Halmashauri hizo katika usimamizi na uendelezaji Miji,
usimamizi na utunzaji mali za Miji, usimamizi wa taka ngumu Mijini na
uboreshaji wa Mfumo wa kukusanya mapato ya ndani na upangaji Miji
kimkakati. Nitumie fursa hii kuagiza Vikao vya Kamati za Mashauriano za
Mikoa husika kujadili taarifa za utekelezaji wa Miradi hii kila
vinapokaa ili matatizo yatakayobainika ya kiutekelezaji yaweze kupatiwa
ufumbuzi wa pamoja haraka.
54. Mheshimiwa Spika, Serikali pia inaendelea na maandalizi ya Mradi mwingine utakaogharimu Dola za Marekani Milioni 255, utakaoanza kutekelezwa mwaka 2013/2014. Mradi huu utahusu uimarishaji wa Serikali za Mitaa zikiwemo Manispaa tatu za Jiji la Dar es Salaam pamoja na Manispaa 11 za
Morogoro, Tabora, Moshi, Sumbawanga, Shinyanga, Songea, Singida,
Musoma, Iringa, Bukoba na Lindi na Miji ya Mpanda, Njombe, Babati,
Geita, Korogwe, Bariadi na Kibaha. Kutekelezwa kwa Miradi hii
kutaboresha hali ya Miji yetu pamoja na huduma zitolewazo na hivyo
kuondokana na vikwazo vya usafiri na usafirishaji vilivyopo katika Miji
hiyo likiwemo suala la kuondoa misongamano ya magari kwa baadhi ya Miji.
UKUSANYAJI WA MAONI KUHUSU KATIBA MPYA
55. Mheshimiwa Spika,
wakati nikiwasilisha Bajeti yangu nilielezea hatua iliyofikiwa katika
Mchakato wa Mabadiliko ya Katiba na kwamba Mheshimiwa Rais alikwishateua
Tume na tayari Tume hiyo ilianza kazi tarehe 1 Mei, 2012. Aidha,
Mheshimiwa Waziri wa Katiba na Sheria wakati akiwasilisha Bajeti yake
alifafanua kwa kina Muundo na Majukumu ya Tume na utaratibu wa jinsi
kazi ya kukusanya Maoni itakavyofanyika.
56. Mheshimiwa Spika, napenda
kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, kazi ya kukusanya Maoni inaendelea
vizuri. Hadi sasa Wajumbe wa Tume wamekwisha kamilisha kukusanya maoni
katika Mikoa minane, ambayo ni Tanga, Pwani, Dodoma, Shinyanga, Kagera, Manyara, Kusini Unguja na Kusini Pemba.Awamu ya Pili inaendelea na Wajumbe hivi sasa wanakusanya maoni katika Mikoa ya Lindi, Morogoro, Mbeya, Ruvuma, Katavi, Kigoma na Mwanza. Nachukua fursa hii kuwapongeza Wananchi kwa kutoa Maoni yao kwa amani na utulivu na bila woga.
57. Mheshimiwa Spika,
baada ya kukamilisha kazi za Awamu ya Kwanza, katika Awamu ya Pili,
Tume itaandaa utaratibu wa kukusanya maoni ya Wananchi kupitia Mabaraza
ya Katiba katika ngazi mbalimbali. Mabaraza hayo yatawashirikisha
Wawakilishi kutoka makundi mbalimbali katika Jamii.
58. Mheshimiwa Spika, ninaelewa
zipo changamoto zilizojitokeza kutokana na Jiografia ya Nchi yetu,
hususan ukubwa wake hivyo kuwa na uwezekano wa baadhi ya Wananchi
wasifikiwe na Tume kwa karibu. Kutokana na changamoto hizo, Tume imeweka
taratibu nyingine zitakazowezesha Wananchi kutoa maoni kwa njia ya
barua, tovuti na mitandao ya kijamii. Nawashauri Wananchi watumie njia
hizo bila kusita ili kuwasilisha maoni yao kwenye Tume. Aidha, tatizo la
usambazaji wa Nyaraka kwa wakati nalo linafanyiwa kazi ili nyaraka hizo
zisambazwe kwa kasi zaidi.
59. Mheshimiwa Spika, natoa
wito kwa Wananchi wote kuendelea kutoa ushirikiano kwa Tume pindi
watakapofika katika maeneo yao kwa lengo la kupata maoni. Suala la kutoa
maoni ni wajibu wetu sote. Katiba nzuri itatokana na maoni ya Wananchi
wenyewe. Hii ni fursa pekee kwa Watanzania, hivyo hatuna budi kuitumia
kikamilifu.
UTAMADUNI WA KUPIMA AFYA
60. Mheshimiwa Spika, tarehe
16 Aprili, 2011 wakati nikihitimisha Mkutano wa Tatu wa Bunge lako
Tukufu nilizungumzia hali ya Magonjwa Makuu Nchini. Nilibainisha maradhi
makubwa ambayo yamepewa msukumo mkubwa na Serikali katika kuyatokomeza.
Magonjwa hayo ni Malaria, Kifua Kikuu, Shinikizo la Damu, Kisukari,
Saratani na UKIMWI. Hata hivyo, ilibainika kwamba Magonjwa ya Shinikizo
la Damu, Kisukari na Saratani hayajapata msukumo mkubwa unaostahili
pamoja na kwamba yamekuwa yakisababisha vifo vingi Nchini. Niruhusu
nieleze kwa mara nyingine kwa ufupi kuhusu Ugonjwa wa Saratani, hususan
Saratani ya Tezi ya Kibofu cha Mkojo (Prostate Cancer) ambao unawapata Wanaume zaidi.
61. Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Saratani Duniani (The World Cancer Report) za miaka mbalimbali zinaonesha kuwa Wanaume wawili Duniani wanahitaji kupata matibabu ya Saratani ya Tezi la Kibofu cha Mkojo kila dakika tano. Aidha, ukubwa wa tatizo la Ugonjwa huu umekuwa ukiongezeka kwa kasi na sasa unawapata Wanaume wenye umri wa kuanzia Miaka 45 na kuendelea badala ya Miaka 50 ya Awali hivyo, kupanua wigo wa uwezekano wa Watu wengi zaidi kupata ugonjwa huo. Dalili za Ugonjwa huu katika hatua za mwanzo
kabisa ni pamoja na kushindwa kupata haja ndogo vizuri, kupata haja
ndogo mara nyingi kuliko kawaida, na kuanza kukojoa damu, au haja ndogo
kushindwa kutoka kabisa. Aidha, Vimelea vinapoanza kusambaa, mgonjwa
anaanza kupata maumivu ya mgongo, kuvimba miguu, na baadaye figo kushindwa kufanya kazi.
Kutokana na hali hiyo, upo umuhimu wa kuongeza nguvu katika kutoa elimu
kuhusu ugonjwa huu na kuhamasisha Wananchi waweze kupima afya zao
mapema.
62. Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwaomba Wanaume wote wenye umri unaofika miaka 45 na
kuendelea kujenga utamaduni wa kupima afya zao mapema ili kubaini hali
ilivyo kuhusu ugonjwa huu wa Saratani ya Tezi la Kibofu cha Mkojo kwa
sababu ugonjwa huu unatibika kama ukibainika mapema. Kwa misingi hiyo,
napenda kuiagiza Wizara ya Afya kuweka utaratibu maalum wa kuelimisha
Wananchi kuhusu ugonjwa huu wa Tezi la Kibofu cha Mkojo.
Bajeti ya Afya kuwa Asilimia 15
63. Mheshimiwa Spika, katika
Mkutano kati ya Mawaziri wa Fedha na Mawaziri wa Afya wa Afrika
ulioandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kwa kushirikiana na
Shirika la Harmonization for Health in Africa (HHA) uliofanyika
Nchini Tunisia tarehe 03 hadi 06 Julai 2012, suala kubwa
lililojadiliwa lilikuwa ni kuendelea kusisitiza Serikali za Nchi za
Afrika kutenga fedha zaidi kwenye Sekta ya Afya. Lengo
likiwa ni kuhakikisha kuwa, Wananchi wanakuwa na Afya nzuri kwa ukuaji
wa uchumi wa Nchi zetu. Mkutano huo ulipendekeza angalauAsilimia 15 ya Bajeti ya Serikali za Nchi za Afrika iende
kwenye Sekta ya Afya. Michango mingi iliyotolewa katika Mkutano huo
ilithibitisha kwamba, Uchumi wa Nchi za Afrika hauwezi kukua na kuwa
endelevu kama Nchi hizi hazina Wananchi wanaopata huduma nzuri za Afya.
64. Mheshimiwa Spika, licha
ya ufinyu wa Bajeti, Serikali imedhamiria kadri ya uwezo wetu kufikia
lengo hilo kama ilivyopendekezwa. Fedha zinazotengwa kwa ajili ya Afya
zimekuwa zikiongezeka mwaka hadi mwaka. Kwa maana hiyo, kiasi
kilichotengwa kimeongezeka kutoka Shilingi Bilioni 365.8 sawa na Asilimia 8.8mwaka 2005/2006 hadi Shilingi Bilioni 1,288.8 sawa na Asilimia 10.0 mwaka 2012/2013. Ni matumaini yangu kwamba, kwa mwelekeo huo Serikali inaamini tutaweza kufikia Asilimia 15 kama
tulivyokubaliana katika Mkutano huo. Aidha, ongezeko hilo linaonesha
jinsi Serikali ilivyoamua kuwekeza katika Sekta hii muhimu ya Afya kwa
manufaa ya Wananchi wake.
AJIRA KWA VIJANA
65. Mheshimiwa Spika, moja
ya changamoto zinazokabili Taifa letu ni kiwango cha juu cha ukosefu wa
Ajira hasa kwa Vijana. Kwa mujibu wa takwimu zilizopo, jumla ya Vijana
wasio na Ajira hapa Nchini ni Milioni 1.4, sawa na Asilimia 13.4 ya
nguvu kazi yote ya Vijana. Kuongezeka kwa kasi kwa ukosefu wa Ajira kwa
Vijana kunachangiwa na mambo kadhaa, ikiwemo uwekezaji mdogo wa ndani
na nje, kasi ndogo ya ukuaji wa Sekta Binafsi Nchini na ukosefu wa elimu
ya ujasiriamali kwa Vijana wengi. Aidha, ukosefu wa Ajira pia
unasababishwa na baadhi ya Vijana kuchagua kazi za kuajiriwa, badala ya
kujiajiri wenyewe hasa kwenye Sekta zenye fursa kubwa kama vile Kilimo,
Mifugo, Uvuvi na Ufugaji Nyuki.
66. Mheshimiwa Spika, katika
Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge mbalimbali walipata fursa ya kutoa
michango mizuri ya mawazo inayoelezea ukubwa wa tatizo la Ajira
Nchini, na namna ya kulipatia ufumbuzi. Aidha, Waheshimiwa Wabunge wengi
waliafikiana na Serikali kwamba changamoto ya upatikanaji wa Ajira
nyingi kwa Vijana inahitaji ushirikiano wa Wadau wengi. Ni dhahiri kuwa,
juhudi za pamoja zinahitajika baina ya Serikali, Sekta Binafsi, Vyama
vya Wafanyakazi na Waajiri, Taasisi Zisizo za Kiserikali na Jamii kwa
ujumla kukabiliana na changamoto hii. Kwa upande wake, Serikali ina
wajibu mkubwa wa kuweka mazingira wezeshi ya kuongeza Uwekezaji na
ukuaji wa Sekta Binafsi ili kuongeza fursa nyingi za upatikanaji wa
Ajira. Hii ni pamoja na kubuni na kuandaa Sera na Sheria Wezeshi za
Uwekezaji, uzalishaji na kufanya biashara. Vilevile, kuhakikisha kwamba
kuna miundombinu muhimu ya usafirishaji, umeme wa kutosha, maeneo ya
kuwekeza na kuzalisha pamoja na Mfumo bora wa elimu utakaowezesha
wahitimu wengi kujiajiri na kushindana katika Soko la Ajira.
67. Mheshimiwa Spika, pamoja
na jitihada za kuvutia uwekezaji, Serikali inaimarisha Mifuko
mbalimbali ya kuwawezesha Vijana ili waweze kujiajiri wenyewe. Kwa
mfano, Mfuko wa Dhamana chini ya Programu ya Taifa ya Kuwezesha Wananchi
Kiuchumi, (Maarufu kama Fedha za JK); Mfuko wa Maendeleo ya Vijana
unaosimamiwa na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo; Mfuko wa
Wajasiliamali Wadogo unaosimamiwa na SIDO; na Vyama vya Akiba na Mikopo
(SACCOS) vimeimarishwa na kuwekewa mazingira mazuri ya kuviwezesha
kufanya kazi kibiashara na kwa ufanisi. Ni matumaini yangu kwamba
tukitumia Mifuko hii vizuri tutaweza kuongeza Ajira kwa Vijana kwa kasi
zaidi. Nasisitiza pia kuwa, ni muhimu kwa vijana wetu na wale wote
wanaopata ajira au kujiajiri wenyewe wawe na nidhamu kazini, wafanye
kazi kwa weledi na kutumia utaalam wao vizuri. Tusiwe wepesi kulalamika
wakati hatutimizi wajibu wetu kama Waajiriwa.
SENSA YA WATU NA MAKAZI
68. Mheshimiwa Spika, takriban
siku kumi zijazo tutakuwa na Sensa ya Watu na Makazi litakalofanyika
kuanzia saa Sita Usiku wa kuamkia tarehe 26 Agosti, 2012 Nchini kote.
Umuhimu wa Sensa hii nimeuelezea katika hotuba zangu za ndani na nje ya
Bunge lako Tukufu zikiwemo hotuba za Bajeti kwa miaka mitatu mfululizo.
Kwa kutambua umuhimu wake maandalizi yaliyoanza mapema mwaka huu sasa
yamekamilika. Kwa vile, Mkutano huu unamalizika siku chache kabla ya
kufanyika kwa Sensa hiyo, napenda kutumia fursa hii kuwashukuru kwa
dhati Watanzania wote waliojitolea kwa hali na mali wakati wa kipindi
chote cha maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi. Tumejitahidi kwa kadri
ya uwezo wetu kujiandaa vizuri na sasa siku imewadia. Wito wangu kwa
Wananchi wote ni kuendelea kutoa ushirikiano kwa Makarani wa Sensa na
kujitokeza kuhesabiwa kuanzia tarehe 26 Agosti, 2012 hadi zoezi hilo
litakapokamilika.
69. Mheshimiwa Spika, kwa
namna ya pekee niwashukuru Viongozi wa Taasisi za Dini ambao kwa pamoja
waliona umuhimu wa Sensa na hatimaye kuwahamasisha Waumini wao
kushiriki katika zoezi zima la Sensa ya Watu na Makazi. Niwashukuru
kwa kuwasaidia Waumini hao kwa kuwapa maelezo yaliyo sahihi kuhusu
zoezi zima la Sensa. Madhumuni ya Zoezi la Sensa ni kuliwezesha
Taifa kupata Takwimu sahihi na za uhakika kuhusu idadi ya Watu ili
ziweze kutumika kutunga Sera za Kiuchumi na Kijamii, pamoja na kuwezesha
kupanga kwa usahihi, kutekeleza na kutathmini Mipango ya Maendeleo ya
muda mfupi na muda mrefu.
70. Aidha, napenda kusisitiza tena kwamba Zoezi la Sensa halitakuwa la siku moja tu, bali siku hiyo ya tarehe 26 Agosti, 2012 itakuwa ndiyo siku ya msingi wa kuhesabu Watu waliolala siku hiyo katika Kaya husika. Kazi yenyewe ya kuhesabu Watu itaendelea kwa siku saba hadi tarehe 2 Septemba, 2012. Hivyo,Nawasihi
Waheshimiwa Wabunge na Viongozi wote katika ngazi zote kusimamia zoezi
hili na kuendelea kuwahamasisha Wananchi kushiriki kuhesabiwa siku ya
Sensa tarehe 26 Agosti 2012.
HITIMISHO
71. Mheshimiwa Spika, kabla
ya kuhitimisha hotuba yangu napenda kusisitiza kuwa tumetekeleza wajibu
wetu kama Wabunge kwa kutoa michango yetu ndani ya Bunge lako Tukufu.
Ni kweli kwamba, tumefanya kazi kubwa inayostahili pongezi. Lakini pia
Bunge kama Chombo cha Uwakilishi, linayo majukumu mengine na moja ni
kuisimamia Serikali iliyoko Madarakani itimize Wajibu wake. Ni wajibu
wetu kama Wabunge kuikosoa Serikali ili kuhakikisha kwamba matatizo na
kero mbalimbali za Wananchi yanatatuliwa. Lakini siyo kuikosoa na
kuishia hapo tu, bali tuna wajibu wa kuishauri na kuielekeza kwa lengo
la kuwaletea maendeleo Wananchi walio tuchagua.
72. Mheshimiwa Spika, ili
yote hayo yafanyike, ni lazima sisi kama Wabunge tuwe Wasafi na wenye
Maadili mbele za Wananchi wetu. Tuhuma za Rushwa zilizojitokeza dhidi ya
baadhi ya Wabunge na hivyo kupelekwa kwenye Kamati ya Maadili, haileti
picha nzuri kwa Bunge letu. Ninachowaomba Waheshimiwa Wabunge ni kwamba
tutambue dhamana kubwa tuliyonayo kwa Wananchi wetu. Ni vizuri tuienzi
dhamana hiyo na kuiheshimu. Hivyo, nawasihi tutumie fursa ya kipindi
hiki kilichobaki cha takribani miaka mitatu kuendelea kuimarisha
utamaduni wa kushirikiana na kuhakikisha kwamba tunawatumikia Wananchi
waliotuchagua kwa bidii zetu zote.
73. Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kuwashukuru tena wote waliosaidia kufanikisha Mkutano huu.
Shukrani za pekee ni kwako wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika
kwa kutuongoza vizuri. Nawashukuru vilevile Wenyeviti wa Bunge wote kwa
msaada mkubwa walioutoa katika kuliongoza Bunge kwenye Mkutano huu. Aidha,
nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao pamoja na
Watumishi wote wa Serikali walioisaidia Serikali kujibu maswali na
kuwasilisha Hoja za Serikali hapa Bungeni. Kipekee namshukuru
Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashilillah pamoja na Watumishi wote wa
Ofisi ya Bunge kwa kufanikisha Mkutano huu. Nawashukuru wale wote
waliokuwa na jukumu la Ulinzi na Usalama ili kuhakikisha Mkutano huu
unafanyika na kumalizika salama. Napenda pia niwashukuru Madereva wote
kwa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi mkubwa. Nawashukuru pia Waandishi
wa Habari kwa kuhakikisha kuwa Habari za hapa Bungeni zinawafikia
Wananchi. Mwisho, niwashukuru Wananchi wa Dodoma kwa ukarimu wao wa
kutupatia huduma zote muhimu na hivyo kukamilisha Mkutano huu wa
mafanikio makubwa.
74. Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja kuwa Bunge lako Tukufu sasa liahirishwe hadi Jumanne, tarehe 30 Oktoba, 2012, litakapokutana saa 3.00 Asubuhi hapa Mjini Dodoma.
No comments:
Post a Comment