|
ZAMA za kidhanifu ambazo zilimchora mwanamke kama kiumbe duni na asiye na uwezo wa kiuchumi na kisiasa, hapana shaka tumezizika. Hilo limedhihirika baada ya wanawake wawili wa kiafrika, Joyce Banda wa Malawi na Sirleaf Hellen Johnson, wa Liberia kushika nyadhifa za urais katika nchi zao na Fatou Bensouda aliyeteuliwa kuwa mwendesha mashtaka wa mahakama ya kimataifa ya kesi za jinai,(ICC) akiwa ni mwanamke wa kwanza duniani kushika wadhifa huo . Hata hivyo hapa Tanzania bado tuna wanawake wenye nguvu na ambao wameshaonyesha uwezo katika ngazi za kitaifa na kimataifa. Ingawa wapo wanawake wengi waliowahi kufanya vyema katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni, lakini leo nitakupa maelezo mafupi ya wanawake watano wa kitanzania, ambao wameonekana kuwa na nguvu kitaifa na kimataifa. Gertrude Mongela Huyu ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa kuwa rais wa Bunge la Afrika(Pan African Parliament) aliteuliwa kushika wadhifa huu mwaka 2004 na kuiwekea Tanzania sifa lukuki duniani kote. Alihitimu shahada ya kwanza katika chuo kikuu cha Afrika Mashariki, mwaka 1970 na alijiunga chama cha mapinduzi mwaka 1977 tangu wakati huo amekuwa akiteuliwa kushika nyadhifa kubwa hasa na mashirika ya nje ya nchi. Baadhi ya taasisi za kimataifa ambazo amewahi kuziongoza ni pamoja na shirika la afya duniani, mkutano wa Beijing, umoja wa nchi huru za afrika(oau) na aliwahi kuwa balozi wa Tanzania nchini india. Mwaka 1982 hadi 1988 Mongela aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu na tangu wakati huo alihama wizara kadhaa ikiwemo ya Maliasili na Utalii na baadaye Waziri asiye na Wizara Maalum. Dk Asha Rose Migiro Inavyoonekana, anga za kimataifa zimegundua kuwa wanawake wa kitanzania wana uwezo wa kipekee katika uongozi. Baada ya Tibaijuka kushika nyadhifa mbalimbali Umoja wa Mataifa, mwaka 2007 baada ya Ban Kimoon kushika madaraka UN alimteua Dk Asha Rose Migiro kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja huo. Hicho ni cheo kikubwa ambacho hakikuwahi kushikwa na mwanamke wa Kiafrika tangu kuanza kwa UN. Kabla ya cheo hicho cha UN, Migiro akiwa ni mwanachama wa CCM, tangu mwaka 1994, aliwahi kuwa Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa nafasi ambayo awali ilishikwa na Rais Jakaya Kikwete kabla ya kuwa rais na ni nafasi ambayo haikuwahi kushikwa na mwanamke yeyote tangu Tanzania ipate uhuru. Miongoni mwa kazi bora za kimataifa alizowahi kufanya ni pamoja na kufanya mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Franco Frattini, na Papa Benedict 19 kwa ajili ya kujadili unyanyasaji wa wanawake. Dk Migiro ameipata shahada ya Sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, na alipata kusomea shahada nyingine katika Chuo Kikuu cha Konstanz Ujerumani. Aidha aliwahi kuwa Mhadhiri mkuu Kitengo cha Sheria, chuoni UDSM. Professa Anna Tibaijuka Profesa Tibaijuka ambaye kwa sasa ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, anatajwa kuwa mwanamke hodari na anayeamika Tanzania. Mwaka 1998 Profesa Tibaijuka aliteuliwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ,(UN) Koffi Annan kuwa Mkurugenzi wa Masuala ya makazi wa UN. Mwaka 1998, Profesa Tibaijuka aliteuliwa kuwa mratibu maalum wa nchi zinazoendelea na visiwa vidogo katika nchi hizo katika mkutano wa biashara na maendeleo wa UN. Alitakiwa kuimarisha uwezo wa nchi hizo katika majadiliano ya kibiashara kwenye Taasisi ya Dunia ya Biashara(WTO) Profesa Tibaijuka ni mtaalamu wa uchumi na kilimo ambaye amenyakua shahada yake kutoka chuo cha kilimo cha Sweden. Ni mjane kwa Wilson Tibaijuka aliyekuwa balozi. Anna Makinda Ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa uspika wa bunge la Tanzania. Nafasi ambayo pengine haikuwahi kuotwa na wanawake wengi, kutokana na kasumba au mfumo dume. Mwaka 2010, Makinda alifungua pazia kwa wanawake Tanzania nzima kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo.. Kabla ya cheo cha uspika, Makinda alipitia nafasi mbalimbali bungeni, alikuwa mbunge wa kawaida kwa miaka nane hadi mwaka 1983 alipoteuliwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Makamu wa Rais. Alichaguliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma mwaka 1995 hadi 2000 na anasema hiyo ni kazi aliyoipenda zaidi kwani alikuwa akifanya kazi kwa ukaribu zaidi na wananchi. Aliwahi kuwa Mwenyekiti wa bunge, akimsaidia spika kuendesha vikao, halikadhalika alikuwa ni mjumbe wa kamati ya kudumu ya bunge ya maliasili, mazingira na kuondoa umaskini. Liberata Mulamula Huyu ni mwanamke aliyepata kushika cheo kikubwa na kuonyesha juhudi za dhati. Machi mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete alimteua Mulamula kuwa msaidizi wa Rais Mwandamizi Masuala ya Diplomasia. Mulamula aliwahi kuwa Katibu Mkuu Mtendaji wa Kongamano la nchi za Maziwa Makuu, (ICGRL) wadhifa alioushika hadi Disemba 2011., Katika nafasi yake hii, Mulamula alitakiwa kusimamia amani, usalama na maendeleo katika nchi za maziwa makuu na aliifanya vyema. Aidha Mulamula aliwahi kuwa mshauri wa mazungumzo ya amani nchini Rwanda tangu 1992 hadi 1994. Umahiri wake katika masuala ya kimataifa ulimuwezesha kuchaguliwa kuwa Balozi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa nafasi aliyoshikilia mwaka 1985 hadi 1992. Aliwahi kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Idara ya Mahusiano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kipindi cha mwaka 2003 hadi 2006 Amewahi kufanya kazi nyingi za kimataifa ikiwemo kuwa balozi wa Canada na Marekani, na kushiriki mikutano ya UN na OAU. source gazeti la mwanainchi. |
No comments:
Post a Comment